Biblia iliandikwa na nani?

  Maswali ya Biblia, Uncategorized


JIBU: Jina la Bwana Wetu na Mungu wetu Yesu Kristo litukuzwe daima, sifa na Utukufu ni vyake milele na milele Amina. 


Hili ni moja ya swali linaloulizwa hasa na watu wasiotaka kusikiliza kabisa habari za Mungu, lakini pia, hata na baadhi ya wasomi wengi duniani kwa kisingizio kuwa, biblia iliandikwa na mtu fulani tu, hivyo mwanadamu hapaswi kuzingatia sana waliyoandikwa humo kama wahubiri wengi wanavyosisitiza leo hii, lakini nataka nikwambie wewe ndugu unayesoma ujumbe huu kuwa, hiyo ni dhana potofu kabisa kutoka kwa adui, amini usiamini, biblia ni kitabu pekee kinachoweza kukupa amani hapa duniani na kukufikisha katika uzima wa milele endapo utayaishi na kuyazingatia yaliyomo humo kikamilifu.

Yoshua 1: 8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. 

Lakini kabla ya kufahamu biblia iliandikwa na nani, ni muhimu kwanza kufahamu biblia ni nini na kwa nini iliitwa hivyo, na je! neno lenyewe BIBLIA linapatikana katika biblia? Sasa Ili kufahamu hilo zaidi unaweza fungua hapa >>>Biblia ni nini? Je Neno hilo lipo katika biblia yenyewe?


Ila kwa ufupi ni kwamba, zamani kabisa jina lililokuwa likitumika ni MAANDIKO MATAKATIFU (yaani maneno ya Mungu na mipango yake), ambayo yaliandikwa na watumishi wake kama walivyojaaliwa, maneno hayo ya Mungu na mipango yake ilikuwepo tangu zamani kabisa kabla ya vitu vyote kuumbwa, lakini ulipofika wakati wa Mungu kutaka kuwajuza wanadamu juu ya mpango wake kwa dunia nzima, ndipo akasema na kuwaonesha kwanza watumishi wake juu ya hiyo mipango yake, yaani mambo yatakayokuja, yaliyopo na yaliyotokea.
Mfano; utaona nabii Yeremia akioneshwa na Mungu nini kilikuwepo kabla ya dunia kuumbwa (Yeremia 4:23), lakini si yeye tu bali na watumishi wengine kadha wa kadha kama Mungu alivyowajaalia, sasa hawa ndio walioyaweka mambo yote waliyoyaona na waliyojuzwa kwenye maandishi. 


KUMBUKA; ni yale tu ambayo Mungu ametaka sisi tuyafahamu ndiyo aliyoyaweka wazi.

Kumbukumbu La Torati 29:29  Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; LAKINI MAMBO YALIYOFUNULIWA NI YETU SISI NA WATOTO WETU MILELE, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii. 

Hii ikiwa na maana kuwa, kuna mambo mengi mno yanayomuhusu Mungu ambayo sisi wanadamu hatuyafahamu, hebu jiulize swali dogo tu, ikiwa mambo yaliyotokea wakati Mungu alipojidhihirisha katika mwili yasingetosha ulimwengu mzima kama yangeandikwa moja moja,

Yohana 21:25 Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; AMBAYO YAKIANDIKWA MOJA MOJA, NADHANI HATA ULIMWENGU USINGETOSHA KWA VILE VITABU VITAKAVYOANDIKWA. 

itakuwaje sasa juu ya mambo yaliyotokea baada ya yeye kupaa na yenyewe yangeandikwa? Au unaanzaje kumuelezea Mtu ambaye hana mwanzo? na tena hana mwisho?  Ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa, na ndio maana yale aliyoyataka tuyajue ndiyo aliyosema na sisi kwa njia watumishi wake na kuyahifadhi katika maandishi ambayo yanadumu hadi leo hii (biblia)

Kuamini kwako biblia au kutokuamini kwako biblia, kamwe hakubatilishi uwepo wa Mungu wala hakumfanyi yeye kutokuwepo, hivyo ni heri uamini leo na kutii kabla ile siku haijafika, kwani wewe na huyo kiongozi wako anayekufundisha upotovu kuhusu biblia kila mmoja atapiga goti mbele Zake (Yesu Kristo) na kumkiri kama yeye ni amini na kweli

Isaya 45:23  Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, YA KWAMBA MBELE ZANGU KILA GOTI LITAPIGWA, KILA ULIMI UTAAPA. 


Hivyo, kwa kuhitimisha ni kwamba, maandiko matakatifu (biblia), yaliandikwa na wajumbe wa Mungu waliochaguliwa na Yeye mwenyewe na kupewa neema ya kufahamu mpango  Wake juu ya wanadamu na ulimwengu mzima (na tena ni kwa sehemu tu) kwa lengo la kuwakomboa wanadamu.

Bwana akubariki, Shalom.

Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.

+255652274252/ +255789001312

Mada zinginezo:

Ni Mtume gani aliyekuwa Mkuu na Wa kwanza  kuliko wote katika biblia?


Makuhani wa Mungu ni watu gani katika biblia?


VIFUNGO VYA WOTE VIKALEGEZWA.


Kwanini watu wa Kanisa la kwanza walionekana kujazwa Roho Mtakatifu zaidi ya Mara moja?


 Je! Ni lazima mgonjwa adongoke chini pale anapoombewa?

LEAVE A COMMENT