VIFUNGO VYA WOTE VIKALEGEZWA.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Shalom, jina la Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristo litukuzwe milele na milele, karibu katika kuyatafakari maneno ya uzima ya Bwana Mungu wetu.

Biblia inasema katika..

Matendo 16:25-26

Matendo 16:25  Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.

 26 Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, VIFUNGO VYA WOTE VIKALEGEZWA

Ulishawahi jiuliza kwanini Mungu aliamua kutetemesha misingi ya gereza wakati Sila na Paulo walipokuwa wakimwomba na kumwimbia usiku wa manane? Au unadhani Mungu alishindwa kuwatoa gerezani Sila na Paulo katika kifungo chao pasipo kutetemesha misingi ya gereza kama vile alivyomtoa mtume Petro gerezani kwa kumtumia malaika na pasipo matetemeko yoyote? (Matendo 12:5-11)

Au unadhani Bwana alishindwa kumpa wokovu yule mlinzi wa gereza kwa njia nyingine, labda kwa mfano kama alivyofanya kwa Kornelio? Jibu ni hapana! Bwana angeweza kutumia njia nyingine yoyote ile kumpa yule mlinzi wokovu, na pia kuwatoa Sila na Paulo mle gerezani kwa njia nyingine tofauti na hiyo, kwani njia za Bwana ni nyingi sana na wala hazichunguziki, ndivyo biblia inavyosema

Warumi 11:33  Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, WALA NJIA ZAKE HAZITAFUTIKANIKI! 

Lakini swali la kijiuliza ni hili, kwanini atetemeshe misingi ya gereza lote na si mahali pale walipokuwa Sila na Paulo tu? 

Jibu ni kwamba, kuna jambo ambalo Mungu anataka kutufunza hapo, na jambo lenyewe ni kuwa, na sisi pia tunapo kesha kumwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu na kumwabudu usiku wa manene, ama kwenye mikesha kanisani, ama sehemu yoyote ile, VIFUNGO VYA WATU WENGINE PIA VINALEGEZWA, Kwa maombi yetu na sifa zetu, Mungu hatetemeshi mahali tulipo sisi tu, bali na kwa wengine, na tena kizuri zaidi ni kuwa, vifungu vyao vya kutokutaka kumjua Bwana kutoka kwa yule adui vinalegezwa pia.

Matendo 16:26 Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, VIFUNGO VYA WOTE VIKALEGEZWA

Watu wanapotusikia tukimwomba Mungu na kumsifu wakati wowote ule, vifungo vyao vinalegezwa taratibu pasipo sisi kufahamu, watu wanaposikia mahubiri kwa mbali, vifungo vyao vinalegwa taratibu kwa kupanda mbegu ndogo sana ndani yao, na mwisho wa siku watataka kusikia zaidi na hapo ndipo inapopatikana nafasi ya kuhubiriwa injili ya wokovu kwa undani zaidi. Tunapomsifu Mungu na kumwimbia, Roho Mtakatifu anashuka mahali tulipo na kupatetemesha hapo katika roho na kufanya mabadiliko makubwa ambayo sisi hatuwezi kuona kwa macho ya nyama. 

Na ndio maana utagundua kuwa, Roho Mtakatifu aliposhuka siku ya pentekoste kama upepo na moto, mahali pale palikuwa patofauti kutokana na uwepo wa wake, hivyo kupelekea vifungo vya mioyo vilimokuwa ndani ya wale watu waliosikia kulegezwa na kutaka kusikia zaidi kuhusu Mungu. Unaona umuhimu wa kukesha na kumwomba Mungu na kumsifu? Si kwa faida yetu tu bali na hata wengine pia.

Lakini ikiwa kwa sifa na maombi, Bwana analegeza vifungo vya mioyo migumu vya wengine, je! Vipi endapo tukiwaweka ndugu zetu na marafiki zetu katika maombi na kumwomba Bwana awape neema ya wokovu? Je si zaidi sana? Jibu ndio na ni zaidi sana, na tena Bwana atafanya tusipokata tamaa kwani yeye mwenyewe anasema mapenzi yake ni ili kila mtu aifikirie toba na kuwa na uzima wa milele.

Hivyo tukiomba sawa sawa na mapenzi yake hayo hakika atatujibu, Hivyo hatuna budi kuwaombea na ndugu zetu na jamaa zetu neema ya wokovu na kuwahubiria habari njema.

1 Yohana 5:14  Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. 

Tafadhari washirikishe na wengine ujumbe huu.

+255652274252/ +255789001312

Bwana akubariki, Shalom.


Mada zinginezo:

Akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya.


KRISTO ALIZICHUKUA VIPI DHAMBI ZA WATAKATIFU WALIOKUFA KABLA YAKE?


ITAMBUE NA KUIFANYA HUDUMA YA YOHANA MBATIZAJI  KATIKA UKRISTO WAKO.


WEWE HU MBALI NA UFALME WA MUNGU.


AKAJIBU AKASEMA, NAENDA, BWANA; ASIENDE.

LEAVE A COMMENT