Bado Bwana Yesu anasema nawe kwa mifano?

Shalom, karibu tuyatafakali maneno ya uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kuna siku wanafunzi walimuuliza Bwana Yesu swali kuwa, kwanini anaongea na makutano kwa kutumia mifano?

Matayo 13:10   Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? 

Sasa utagundua kwamba kwa hiyo mifano, Bwana Yesu alisema na watu wote waliokuwapo hapo yaani, wakati aliposema kwa mifano si kwamba mitume wake waliondoka la! Na wao walikuwepo hapo hapo. Lakini utofauti ni kuwa, mitume na baadhi ya wanafunzi walielewa ile mifano kwa ufafanuzi wa Bwana mwenyewe lakini makutano hawakuelewa kitu, kwao ile mifano ilikuwa ni kama hadithi tu. Na ndio maana sasa wanafunzi wake wakaamua kumuuliza hili swali “kwanini unasema nao kwa mifano?” Lakini jibu la Bwana lilikua ni hili

Matayo 13:11   Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. 

Kumbe ile mifano na hadithi zilikua na Siri zinazohusu ufalme wa Mbinguni na si wote waliojaliwa kuzifahamu, sasa utauliza mbona Mungu anaupendeleo? Jibu ni hapana. Utagundua kuwa shida haipo kwa Mungu bali kwetu sisi wanadamu kwasababu hatutaki kumcha Bwana, tunamfuata Bwana ili tupate kazi, pesa, wenzi, uponyaji n.k kisha baada ya hapo tunaendelea na uzinzi wetu, ulevi wetu, n.k kama hao makutano. Na ndio maana Kuna sehemu Bwana aliwaabia zahiri makutano kuwa, mnanifuata kwasababu mlishiba mikate

Yohana 6:26  Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 

Na ndio sababu ya wao kuona kama Bwana alikua anasimilia hadithi fulani tu, walikua hawataki kusikia habari za wokovu bali habari za kula mikate, kuponywa kisha kurudia maisha yao ya udunia.

Matayo 13:15  Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. 

Hawataki kusikia habari za wokovu wa roho zao na ndio maana mioyo yao imekua mizito. Lakini Maandiko yanasema kuwa, mtu yeyote ambaye ataamua kumchwa Bwana kwa moyo wake wote, kuutafuta uzima wa milele kwa nguvu zote basi, huyo mtu atamfahamu Mungu kwasababu siri zake zipo kwa watu wanaomcha yeye na kumtafuta kwa bidii tu katika neno lake na si madhehebu wala mapokeo fulani.

Zaburi 25:14  Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake. 

Umeona hapo? Kumbe hii siri ipo kwa watu wanaomcha Mungu tu, kwa watu ambao wamejitoa maisha yao kumtafuta Mungu katika Roho na kweli, katika neno lake na si mapokeo ya dini fulani au elimu fulani.

Sasa hadi leo hii kuna watu ambao bado ni kama hawa makutano, kuna watu ambao biblia kwao ni kama hadithi tu, neno la Mungu kwao ni kama mifano tu, Yesu Kristo kwao ni kama mtu tu ambaye aliyekuwepo kipindi cha nyuma tu (historical man)  watu kama hawa hawana tofauti na wale makutano, wengi leo hii wanaenda Kanisani kutafuta uponyaji na si kuacha dhambi zoa na kuishi maisha ya utakatifu, wengi wanaenda kutafuta kazi na akipata anaendelea na uzinzi kama kawaida, sasa mtu kama huyu hana tofauti yoyote na hawa makutano.

Wengine ni watumishi wa Mungu lakini neno la Mungu kwao bado ni giza, wengine wanafika hadi hatua ya kumkana Bwana Yesu na kusema kuwa huyo ni mtu wa kawaida, inasikitisha sana, Wengine  hadi inafika hatua ya kukana maagizo yake kama ubatizo, kushiriki meza ya Bwana, kutawadhana miguu, wanawake kufunika vichwa wakati wa ibada n.k  ndugu yangu, dhamiria leo kujiingiza katika kundi hili la wamchao Bwana ili maneno ya Bwana yasiwe kama mifano kwako.

Siri za Bwana hatuzifahamu kwa elimu zetu tulizozisomea miaka kadhaa la! Bali kwa msaada wa Roho mtakatifu tu,na ndio maana utagundua kuwa petro ambaye alikuwa mvuvi tu alifahamu kuwa kristo ni nani lakini makuhani na waandishi  waliosomea torati walishindwa. Utaona kuwa Tomaso ambaye alikuwa ni mvuvi ( Yohana 21:1-3) aliweza pata ufunuo na kumwita Yesu “Bwana wangu na Mungu wangu” wakati waandishi na mafarisayo walimtukana.

Sasa Roho mtakatifu unampataje? unampata kwa kumwamini Bwana Yesu kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yako na kudhamiria kuziacha dhambi zako zote na kisha kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa kina la Yesu sawasawa na matendo 10:48  matendo 19:5 matendo 8:16

Bwana akubariki. Shalom 


Mada zinginezo:

Na wewe umefuata uzushi ulioingizwa kwa werevu? 


KWANINI MNANIITA BWANA, BWANA, WALAKINI HAMYATENDI NISEMAYO?


NAO WATAJIEPUSHA WASISIKIE YALIYO KWELI


INJILI YA KRISTO HAIENDI NA WAKATI


NA HAPA YUPO ALIYE MKUU KULIKO YONA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *