Na wewe umefuata uzushi ulioingizwa kwa werevu? 

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Bwana Yesu asifiwe ndugu yangu mpendwa katika Bwana, karibu tena tuyatafakari maandiko ya Mwokozi wetu Yesu Kristo katika safari yetu hii ya kuelekea nchi ya ahadi yaani Mbinguni.

Neno uzushi kwa tafsiri isiyo rasmi sana ni ile hali ya kueneza habari zisizo na ukweli au habari za uongo kabisa kwa lengo la kuwafanya watu wasiufahamu ukweli wenyewe wa jambo husika.  Sasa katika imani yetu ya kikristo tuliyoipokea kwa mitume wa Bwana kuna kitu kilitabiriwa na mitume na moja wapo ni hiki tunachokisoma katika

2 Petro 2:1   Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. 

Umeona hapo? Mtume petro aliliona jambo ambalo lingekuja kutokea katikati ya wakristo wa miaka ya baadae, na jambo hilo si lingine bali ni la kutokea kwa waalimu wa uongo ambao kazi yao ni kuwadanganya watu kwa kuingiza habari za uzushi kwa werevu katika ile imani tuliyoipokea kutoka kwa mitume ambayo itatupa wokovu wa roho zetu

1 Petro 1:9   katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu. 

Sasa fahamu kuwa katika mpango huo yupo shetani nyuma yake, kwani yeye ndiye ambaye hataki watu wapate wokovu wa roho zao, hivyo akaamua kuingiza mafundisho ya UZUSHI katika ile imani tuliyoipokea kusudi imani ya kweli ichanganyikane na huo uzushi wake ili watu wasipate wokovu wa roho zao kwani anafahamu kuwa NENO LA MUNGU halitiwi chachu yaani kugoshwa

Sasa huu mpango ulifanywa kwa ustadi wa hali ya juu kiasi kwamba kwa haraka haraka huwezi tambua na ndio maana mtume petro alisema kuwa wataingiza uzushi kwa WEREVU kumaanisha kuwa, kama na wewe ukiwa mjinga utachukuliwa na huu uzushi.

Mafundisho yoyote ambayo hayapatani na yale yaliyofundishwa na mitume wa Bwana Yesu huo ni UZUSHI ulioingizwa kwa werevu ndugu yangu.

Leo utaambiwa katika litania ya bikira Maria kuwa yeye ni malkia wa malaika kitu ambacho hakipo kwenye maandiko na wala hakijawahi hubiriwa na mitume na wala hakipo katika maandiko na wewe ndugu yangu mkristo unakubali, basi fahamu kuwa huo ni uzushi ulioingizwa kwa werevu na lengo lake ni kukupa hasara ya roho yako.

Utaambiwa kusali rosari hakuna shida na utapewa sababu zitakazopendezesha masikio yako kuwa huo ni muunganiko wa sala ya baba yetu na salamu Maria pale Mariamu alipotembelewa na Elizabeth mama yake Yohana mbatizaji lakini nakuambia hicho kitu hakipo kwenye maandiko wala katika imani ya kweli ya kikristo, hakuna mkristo alisali rosari katika maandiko wote waliomba kwa BWANA,  hivyo acha ndugu yangu mpendwa kwani huo ni uzushi ulioingizwa kwa WEREVU wenye lengo la kupoteza nafsi yako.

Utaambiwa kuwa kuna misa ya kutembeza sanamu la bikira maria katika jumuiya yenu na wewe unakubari na kushiriki hizo inada za sanamu, fahamu kuwa wa ni machukizo kwa Bwana ndugu yangu akina petro wala paulo hawajawahi kufanya kitu kama hicho na wala kuagiza kitu kama hicho, huo ni UZUSHI ulioingizwa kwa WEREVU katika imani ya kikristo kwasababu bikira maria alikua ni mshirika wa kanisa la kwanza la mitume yeye na watoto zake wa kiume na wakike na siku ya pentekoste ya yeye alipokea roho mtakatifu kama wanafunzi wengine wa Bwana Yesu 

Matendo Ya Mitume 1:14   Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake. 

Na hawa ndio waliopokea roho mtakatifu siku ya pentekoste 

Matendo Ya Mitume 2:1  Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. 

2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. 

Utaambiwa kuwa ubatizo sio muhimu sana cha muhimu ni kumwamini Bwana Yesu tu basi, ndugu yangu fahamu kuwa huo ni UZUSHI ulioingizwa kwa WEREVU wenye lengo la kukupoteza

Utaambiwa kuwa ni lazima upitie mafundisho fulani ya ubatizo kisha ndo ukabatizwe, wakati kwenye maandiko walioamini tu walibatizwa na baadae kukaa katika fundisho la mitume.

Utaambiwa kuwa kushiriki meza ya Bwana si lazima, ilikua ni ishara tu, ndugu fahamu kuwa huo ni UZUSHI ulioingizwa kwa WEREVU wenye lengo la kukupoteza, Bwana alisema tufanye hivi kwa ukumbusho wake.

Utaambiwa kuwa kutawadhana miguu kwa watakatifu hakupo sasa hivi, ndugu yangu fahamu kuwa huo ni UZUSHI ulioingizwa kwa WEREVU wenye lengo la kukupoteza

Utaambiwa kuwa Mungu haangalii mwili bali roho hivyo jipodoe tu sura yako, vaa mawigi, makucha ya bandia, lipstick mbona hata mtumishi fulani anafanya, utaambiwa vaa tu vimini suruali kwa wanawake wala haina shida na wewe unakubali. Ndugu yangu fahamu kuwa, huo ni UZUSHI ulioingizwa kwa WEREVU.

Ndugu yangu maandiko yanasema katika 

Warumi 2:16  katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu. 

Mungu atakuhukumu wewe sawasawa na injili ya paulo, sasa injili ya paulo ndio injili ya petro ndio injili ya mitume ndio injili ya Bwana Yesu, hutohukumiwa kulingana na mafundisho ya huyo kiongozi wako hapo Kanisani wala mafundisho ya huyo mchungaji wako hapo Kanisani wala hutohukumiwa kulingana na mawazo au mtazamo wa mtu fulani.

Na wewe kiongozi, mchungaji, nabii, au mwalimu unayefundisha injili nyingine tofauti na ile iliyohubiriwa na mitume fahamu kuwa umeshalaaniwa na upo chini ya laana hata kama ukijiona umefanikiwa kiasi gani katika mwili kama maandiko yanavyosema katika

Wagalatia 1:8  ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. 

9 Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. 

Na pia fahamu kuwa ulishapewa onyo na Bwana Yesu, kuwa unawafungia watu ufalme wa Mbinguni kwa kufundisha  injili nyingine, na wewe mwenyewe huingii na pia unajiletea uharibifu usiokawia hivyo tubu leo.

Matayo 23:13  Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie. 

Hivyo ndugu yangu tubu leo dhambi zako zote na uachane na huo uzushi ulioingizwa katika ukristo na kumwamini Bwana Yesu na kisha kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu sawasawa na maandiko 

Bwana akubariki. Shalom


Mada zinginezo:

Je! Umeiamini Injili Ipi?


Je! Ni kweli mshahara wa dhambi ni mauti na si moto wa milele?


JIHADHARI NA WAKINA BALAAMU WA NYAKATI ZA SASA.


BASI WAKIWAAMBIA, YUKO JANGWANI, MSITOKE; YUMO NYUMBANI, MSISADIKI. 
Nini maana ya kuokoka katika biblia?

LEAVE A COMMENT