INJILI YA KRISTO HAIENDI NA WAKATI


Katika dunia hii tuanayoishi, vitu vingi vilikuwapo na vikapita kulingana na maendeleo fulani katika jamii, hata sasa, vitu vingi vipo na vitapita kulingana na ukuaji wa maendeleo katika jamii fulani, sheria na katiba za nchi mbali mbali zilikiwepo na kubadirishwa, na zitaendelea kubadirishwa kulingana na ukuaji wa tekinolojia na maendeleo katika sehemu husika. Hayo yote yanatokea ili wanadamu waweze kwenda na wakati.


Lakini Neno la Mungu ni kinyume chake, lenyewe lipo vile vile, haijarishi dunia nzima inafanya nini ili kwenda na wakati, haijarishi wanadamu wataamini nini ili kuendana na wakati, lenyewe litabaki vile vile kama biblia inavyosema katika….

Isaya 40:8  Majani yakauka, ua lanyauka; BALI NENO LA MUNGU WETU LITASIMAMA MILELE. 

Sasa neno la Mungu ni Yesu Kristo, ambaye alihubiriwa habari zake tangu zamani na manabii watakatifu  na  mitume wake, yaani ile INJILI YAKE INAYOOKOA ROHO ZA WATU. HIYO NDUGU YANGU HAIENDI NA WAKATI.

2 Petro 3:2  mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu. 

Njia za kuihubiri injili hii zinaweza badilika kulingana na wakati, lakini si injili yenyewe. Mfano; matumizi ya magari na ndege badala ya farasi katika kupeleka injili sehemu za mbali, matumizi ya intaneti katika kusambaza injili hii kwa kasi zaidi badala ya kutumia merikebu na usafiri wa miguu. Hizo zinaweza badilika kulingana na wakati lakini si INJILI YENYEWE, injili yenyewe itabaki kuwa ile ile, ikufikie kwa njia ya intaneti, au kwa njia ya kipeperushi, yenyewe itakuwa na ujumbe ule ule wala haiwezi badilika na kwenda na wakati.

Watu wengi leo hii tunataka kuifanyia  marekebisho injili  ya Kristo kwa sababu tu inakinzana na wakati tuliopo, hivyo kupelekea uvuguvugu na udunia katika makanisa, kupeleka waumini kunyoa viduku na kuvaa milegezo Kanisani ili kwenda  na wakati, kupelekea wanawake kuvaa suruali na nguo zisizo sitiri miili yao makanisani ili kwenda na wakati, wanawake kuweka makucha bandia, manywele bandia, ili kwenda na wakati, kwa sababu tu sasa hivi unyoaji wa viduku ni kitu cha kawaida, uvaaji suruali kwa wanawake ni kitu cha kawaida. Ndugu nataka nikwambie kuwa, injili hii ya Kristo kamwe haiwezi kwenda na wakati ili kutii  matakwa yako wewe, bali wewe  ndo unapaswa ujikane nafsi yako na kuitii yenyewe.

Injili inayosema…

1 Timotheo 2:12  Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu.

 13 Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.

 14 Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa. 

Haiwezi Kwenda na wakati kwa kusema kuwa, sasa hivi ni haki sawa, hivyo mwanamke pia anaruhusiwa kumiliki kanisa na kuwa mchungaji kama mwanaume tu. 

Injili inayosema kuwa…

Waefeso 5:5  Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna MWASHERATI wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. 

 Haiwezi Kwenda na wakati kwa kusema kuwa, sasa hivi mambo si kama zamani, unaweza kuishi na boyfriend au girlfriend na hakuna shida. Hiyo injili inautambua huo ni kama uzinzi tu, yenyewe haiendi na usasa wako.

Injili inayosema…

1 Wakorinto 11:12……….Hukumuni ninyi wenyewe katika nafsi zenu.

 13 Je! Inapendeza mwanamke amwombe Mungu asipofunikwa kichwa? 

 Haiwezi Kwenda na wakati kwa kusema kuwa, kufunika kichwa ni uzamani na utamaduni wa watu fulani bali, yenyewe itabaki hivyo hivyo.

Injili inayosema….

Marko 16:16  Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. 

Haiendi na wakati kwa kusema kuwa, sasa watoto wachanga nao wanatakiwa  wabatizwe? Ndugu hao hawabatizwi kwani hawawezi amini na injili ndo inasema hivyo, labda ukaondoe huo mstari kwenye biblia.

Maneno ya Kristo ni amini na kweli, na kamwe hayawezi kubadilika badilika ili kwenda na wakati, mbingu na nchi zitapita lakini maneno yake hayatapita kamwe

Matayo 24:35  Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe. 


Hivyo acha kuangalia dunia inaendaje na kufanya nini, wewe itii injili ya Kristo kwa wokovu roho yako.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Bwana akubariki, Shalom.

 +255652274252/ +255789001312


MADA ZINGINEZO:

NA HAPA YUPO ALIYE MKUU KULIKO YONA.


Je! Hadi sasa kuna manabii wa Mungu?


Kulingana na Mathayo 5:29, Je! viungo vyetu vikitukosesha tuvikate?


Je! Ni kweli Bwana Yesu alishika sabato kuninganana luka 4:16?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *