JE! KUNA TOFAUTI GANI KATI YA MTU WA MUNGU NA MTOTO WA MUNGU?

SWALI: Bwana Yesu asifiwe wapendwa,  naomba msaada wa kujua jibu la swali hili, je! kuna tofauti gani kati ya mtu wa Mungu na mtoto wa Mungu?

JIBU: Mtu mmoja anaweza kusema kuna tofauti kati ya mtu wa Mungu na mtoto wa Mungu, na mwingine akasema hakuna tofauti, na wote wakawa sawa. 

Wote waendao katika njia ya Bwana ni watoto wa Mungu, yaani wote walio mpokea Yesu, hao ni watoto wa Mungu. Tunalithibitisha hilo katika…

Yohana 1:12 BALI WOTE WALIOMPOKEA ALIWAPA UWEZO WA KUFANYIKA WATOTO WA MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;

13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. 

Hivyo mtu aliyesema hakuna tofauti kati ya mtu wa Mungu na mtoto wa Mungu anakuwa sawa Kabisa.

Lakini ukienda mbele kidogo, utagundua utofauti mkubwa, Kwa mfano; tunaposema kwamba, mtu fulani ni mwanaume, kila mtu atafahamu ni kwa sababu ya jinsia yake. Lakini pia inaweza kutokea mtu akaitwa mwanaume kwa sababu nyingine kabisa. 

Mfano, mwalimu shuleni anakuagiza ukamuitie wanaume watano waje kunyanyua gogo kutoka sehemu moja kwenda sehemu anayoitaka, kwa namna ya kawaida wanaume ulioambiwa hapo sio kila mwanaume bali wanaume wenye nguvu(walioshiba)

ukileta walio dhaifu atakushangaa na kukurudisha. 

Siku moja wakati tunasoma, kuna rafiki yetu alifanya jambo la kishujaa sana shuleni. Wakati tunarudi tukiwa kundi la wanaume zaidi ya watano njiani, mmoja wetu akasema, “Katika wote hapa tuliopo mwanaume ni mmoja tu” yaani huyo aliyefanya  lile jambo la kishujaa. Sasa hapo hamaanishi sisi wengine sio wanaume ila anamsifu rafiki yetu kwa lile tendo na kana kwamba anatuambia sisi kama ni wanaume kweli tuige mfano wake.

Hivyo maumbile pekee hayatoshi kumwelezea Mwanaume; Nguvu, uwezo, mamlaka vinamkamilisha zaidi.

Hivyo hivyo na MTU WA MUNGU, yeye ni mtoto wa Mungu, lakini anamjua Mungu katika viwango vikubwa, katika maarifa, hekima, busara, matendo ya haki, saburi, utauwa na mienendo yake inathibitisha hayo. Pia anaaminiwa na Bwana kuwa mtumishi wake, si kigeu kigeu tena,  kama ilivyo kwa watoto wa Mungu waliozaliwa punde. ANAIJUA MISINGI YA BWANA VIZURI.

Kumbukumbu la Torati 33:1 Hii ndiyo baraka ya Musa, HUYO MTU WA MUNGU, aliyowabarikia wana wa Israeli kabla ya kufa kwake.

Israel wote walikuwa watoto wa Mungu lakini kulikuwa na utofauti mkubwa kati ya Musa na Israel wote. Musa hakunung’unika lakini wao walinung’unika. 

Paulo pia akimwandikia ndugu Timotheo  alisema..

1 Timotheo 6:10 Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.

 11 Bali wewe, MTU WA MUNGU, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole.

Timotheo alikuwa amekwishathibitika kwa mambo mengi kabla hajapewa jukumu na Paulo la kusamamia wengine, ila akimsihi tu aimarike yeye mwenyewe, pia katika kufundisha kwake, asije akapenda fedha na kuigeuza injili ya Kristo kwa ajili ya kujipatia faida.

Mathayo 11:12 Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni HUPATIKANA KWA NGUVU, nao wenye NGUVU wauteka.

Hapo maandiko yametuonya sisi pia, tusiishie kuita wengine tu watu wa Mungu, bali tuitwe watu wa Mungu.  Ni sawa na kusema “Tangu siku za Yohana mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana KIUME, nao WANAUME wauteka”. Sio wanaume kwa jinsia bali mashujaa, wanawake kwa wanaume. 

Ubarikiwe

+255755251999


Mada zinginezo:

UMESHAIFAHAMU NA KUIPOKEA BARAKA YA IBRAHIMU KATIKA MAISHA YAKO .


Mjumbe wa agano la kwanza alikuwa ni nani?


Lumbwi ni kiumbe gani kwenye maandiko?


Makuhani wa Mungu ni watu gani katika biblia?


KUFANYA MATENDO MEMA HAIMAANISHI KUWA UMESHAUPATA WOKOVU

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *