JIBU: Katika biblia, kuanzia kitabu cha mwanzo hadi cha ufunuo, hakuna sehemu yoyote ile iliyorekodiwa kuwa, Mariamu mama yake Bwana Yesu alipalizwa mbinguni. Ukimtoa Yesu Kristo, aliyechukuliwa juu katika Utukufu, maandiko matakatifu yanarekodi watu wawili tu wasioonja mauti, ambao ni Henoko na nabii Eliya, hao ndio watu ambao biblia inawataja kutokufa kabisa bali waliepushwa na mauti.
Fundisho hili la Mariamu kupalizwa mbinguni lilitoka wapi?
Fundisho hilo liliingizwa na kiongozi wa kanisa katoliki, Papa Pius au Pio wa 12 na kulipitisha rasmi katika waraka wake unaosema, Tunatangaza na kufafanua kuwa ni fundisho la sharti lililofunuliwa na Mungu kwamba, Mama wa Mungu asiye na doa, Maria ambaye ni bikira milele, wakati maisha yake ya kidunia yalipokamilika, alichukuliwa juu MWILI NA ROHO HADI KWENYE UTUKUFU WA MBINGUNI.
Ikiwa na wewe unayesoma ujumbe huu unaamini hivyo hadi sasa, basi tambua kwamba, huyo kiongozi wako aliyekufundisha hivyo ni kipofu na wala hajui maandiko, na kama anayajua, basi, anakuficha ukweli na kukupotosha. kwanza fahamu neno hili, hakuna Mwili wa damu na nyama utakaoweza kuurithi ufalme wa Mungu, tunalithibitisha hilo Katika..
1 Wakorinto 15:50 Ndugu zangu, nisemayo ni haya, YA KUWA NYAMA NA DAMU HAVIWEZI KUURITHI UFALME WA MUNGU; wala uharibifu kurithi kutokuharibika.
Mtume Paulo alipoandika maneno hayo kuwa, mwili wa damu na nyama haviwezi urithi ufalme wa Mungu, sio kwamba alikuwa hafahamu kuwa, Henoko na Eliya hawakuonya mauti, hapana! Alifahamu hilo sana, na katika mafundisho yake hakuna alichofundisha tofauti na kile ambacho kiliandikwa na Musa na manabii (ikiwemo na habari za Henoko na Eliya) kama alivyosema katika..
Matendo 26:22 Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, WALA SISEMI NENO ILA YALE AMBAYO MANABII NA MUSA WALIYASEMA, kwamba yatakuwa;
Lakini kwanini aseme damu na nyama haviwezi urithi ufalme wa Mungu wakati alijua kabisa kuwa Henoko hakuonja mauti? Jibu ni kwamba, mtume Paulo alikuwa na kitu ambacho huyo kiongozi wako aliyekufundisha Mariamu kapalizwa mbinguni hana, na kitu hicho ni ufunuo, hicho ndicho huyo kiongozi wako hana.
Wagalatia 1:12 Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.
Lakini pia, wanasema Mariamu mama yake Bwana Yesu, alipalizwa mbinguni kwa sababu Kwa kukingiwa dhambi mama Maria hahusiki katika hukumu ya mwisho. Kwa kutokuhusika katika hukumu ya mwisho, basi hakustahili mwili wake ukae kaburini kungojea ufufuko siku ya mwisho. Kitu ambacho si sawa kabisa kulingana na biblia, biblia inasema kila mtu atasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Yesu Kristo kupokea malipo yake.
2 Wakorinto 5:10 Kwa maana imetupasa SISI SOTE kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.
Mbali na hivyo, pia husema “Zaidi ya hayo, kwa kuwa Biblia inamtaja Maria kuwa mfuasi wa kwanza Mkristo, inafaa kwamba awe wa kwanza kupokea baraka za kumfuata Kristo” kitu ambacho sio sahihi kabisa kulingana na maandiko matakatifu, mfuasi wa kwanza na mtu wa kwanza kusadiki habari za Bwana Yesu Kristo sio Mariamu, biblia inasema hivi.
Matayo 5:11 Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, KWA AJILI YANGU.
12 Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; KWA MAANA NDIVYO WALIVYOWAUDHI MANABII WALIOKUWA KABLA YENU.
Umeona hapo? Kumbe hata manabii waliokuwepo tangu mwanzo walikuwa ni wafuasi wa Yesu Kristo na waliudhiwa kwa ajili ya Yesu Kristo Kama vile tu mitume na wafuasi wengine akiwemo na Marimu mama yake Bwana Yesu Sasa unawezaje kusema kuwa, Mariamu alikuwa ni mfuasi na mtu wa kwanza kutii neno la Kristo?
Hivyo mafundisho hayo sio sahihi kabisa, ni ya kimapokeo na hakuna mtume aliyefundisha hivyo, kwahiyo wewe kiongozi wa dini ukijiona unafundisha vitu ambavyo havikuhubiriwa na mitume, na unapokea pokea tu na kukubari kila mafundisho kutoka kwa wakubwa wako hata kama hayatokani na maandiko, basi fahamu kuwa, unahubiriwa na kuhubiri injili nyingine, hivyo toka huko kwa usalama wa nafsi yako na anza kuitii injili ya kweli ya uzima.
Tafadhari washirikishe na wengine ujumbe huu
Bwana akubariki, shalom.
+255652274252/ +255789001312
Mada zinginezo:
Je! Bikira Maria ni mkamilishaji wa mahitaji yetu pale tunapokwama? (kulingana na Yohana 2:3-5)
Mama kanisa ni nini? Na Je! bikira Maria ni mama wa kanisa la Kristo?
MADHARA YA KUTOKUSOMA BIBLIA YAKO.
Biblia imeruhusu ubatizo wa vichanga? (kulingana na matendo 16:33)