SWALI: Je! Ni lazima mtu afahamu au akajifunze kidogo lugha ya Kiebrania ili aweze kuelewa maandiko matakatifu na Kumfahamu Bwana?
JIBU: Ili kuelewa maandiko matakatifu na kumfahamu Bwana hakuna ulazima wowote ule wa kusoma wala kujifunza lugha ya kibrania, kigiriki au lugha ya kirumi, kwa sababu ili kumwelewa Bwana na maandiko matakatifu inamchukua Bwana Mwenyewe kujifunua kwa mtu husika na kumfundisha kwa njia zake kama atakavyo Yeye. Unaweza ukawa unajua lugha ya kiebrania au ukajifunza kiebrania na ukaishia kutokuelewa maandiko kabisa kama Mafarisayo na kutomfahamu Bwana hata kidogo.
Kwamfano, mtume Paulo, Mwebrania wa Waebrania (Wafilipi 3:5), aliyejua lugha ya kibrania tangua kuzaliwa kwake, alishindwa kuelewa ufunuo wa maandiko ya Torati na manabii (kabla ya kumkiri Kristo na kubatizwa), na tena, alishindwa kumfahamu Bwana siku ile alipomtokea njiani ingawa alikitambua hicho kiebrania tangu utoto wake.
Matendo 26:14 Tukaanguka nchi sote, NIKASIKIA SAUTI IKISEMA NAMI KWA LUGHA YA KIEBRANIA, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo.
15 Nami nikasema, WEWE U NANI, BWANA? BWANA AKANIAMBIA, MIMI NI YESU, ambaye wewe unaniudhi.
Umeona hapo? Ijapokuwa Paulo alikijua kiebrania lakini alishindwa kumfahamu Bwana hadi akamuuliza WEWE U NANI BWANA?…hiyo ni kuonesha kwamba, unaweza ukakijua kiebrania lakini usimfahamu Bwana kama mtume Paulo hapo.
Wapo wetu wengi leo hii kwa kuikosa kweli wanaamini kwamba, ni lazima mtu usome kiebrania kidogo au kigiriki kidogo ili uweze kuelewa maandiko, au ni lazima uende chuo fulani cha biblia ili uelewe maandiko kitu ambacho si sawa hata kidogo (huo ni uongo wa shetani).
Mtume Petro hakwenda chuo chochote kile cha Torati na sheria, mtume Yohana hakwenda chuo chochote kile cha Torati na sheria, wala mtume Tomaso, Andrea, Mathayo, n.k, bali Bwana Mwenyewe Ndiye aliyewafundisha na mengine kuwafunulia kwa Roho wake Mtakatifu. Lakini hata mtume Paulo hakwenda chuo chochote cha sheria baada ya kuitwa bali kutoka kwenye Bwana ndiye alimfunulia yote asiyoyajua kutoka kwenye torati na manabii kama tu anavyotaka leo hii akufunulie wewe usiyoyajua na uongo uliofundishwa kwenye theologia yako na falsa yako uliyoisomea.
Hivyo, kuelewa maandiko matakatifu inamchukua Mungu Mwenyewe kujifunua kwa mtu husika na kuufungua uelewa wake kwa Roho na sio kukijua kiebrania wala kigiriki.
1 Wakorinto 2:10 Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.
Na Roho Mtakatifu unampata kwa kutubu dhambi zako na kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na Kwa jina La Yesu Kristo sawasawa na
Matendo 2: 38 Petro akawaambia, Tubuni MKABATIZWE KILA MMOJA WENU KWA JINA LAKE YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, NANYI MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU.
Bwana akubariki, Shalom.
Tafadhari washirikishe na wengine ujumbe huu.
+255652274252/ +255789001312
Mada zinginezo:
Je! Vazi takatifu kwa Mkristo ni kanzu kulingana na (Luka 9:3)?
Je! Ni sawa kwa Mkristo kuomba mababu zake waliofariki zamani?
Ishara ya msalaba ni nini? Na je! Ni wapi biblia ilipoagiza mkristo kupiga ishara ya msalaba?
NIFANYE NINI KAMA MKRISTO ILI MUNGU ANIONGEZEE IMANI KWAKE?
Kuuza cheni na hereni ni sawa kwa Mkristo?
Je! Agizo la Bwana kwa mitume wake la kufufua wafu lilikuwa ni kwa baadhi ya mitume tu?