Ishara ya msalaba ni nini? Na je! Ni wapi biblia ilipoagiza mkristo kupiga ishara ya msalaba? 


JIBU: Ishara ya msalaba ni kitendo cha mtu kugusa paji la uso, kifua na mabega kwa kutumia mkono wa kulia na kutamka ‘Kwa Jina la Baba” anapogusa paji la uso, “na la Mwana” anapogusa kifua, “na la Roho Mtakatifu” anapogusa bega la kulia na kushoto na kisha kumalizia neno Amina. 


Ishara ya msalaba hufanywa kabla ya sala na baada ya sala, lakini pia tendo hilo linaweza kufanyika katikati ya sala kulingana na sala husika.


Kulingana na wakatoliki, Ishara ya msalaba hutaja nafsi tatu za Mungu ambazo ni Mungu baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu kitu ambacho sio sahihi (Mungu ni mmoja, ana nafsi moja, naye ni Yesu Kristo, ambaye kila goti litapigwa mbele zake na kila ulimi utakiri ya kuwa yeye ni Mungu)

Isaya 45:23  KWA NAFSI YANGU NIMEAPA, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa. 


Lakini ni sehemu gani ambapo maandiko matakatifu yameagiza mkristo kufanya ishara ya msalaba?

Jibu ni kwamba, hakuna sehemu yoyote ile kwenye maandiko matakatifu ambapo imeelekeza mkristo kufanya ishara ya msalaba kabla na baada ya sala kwa kutamka kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, kinyume chake ni kwamba, biblia inamuelekeza mkristo wa kweli kuwa, kwa chochote kile afanyacho, kwa neno au kwa tendo, akifanye kwa JINA LA YESU KRISTO.

Wakolosai 3:17  Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, FANYENI YOTE KATIKA JINA LA BWANA YESU, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye. 

Hii inamaanisha kuwa, tukisali, ni kwa jina la Yesu Kristo, tukibatiza na kubatizwa ni kwa jina la Yesu Kristo(matendo 2:38 matendo 19:5 matendo 8:16), tukikemea pepo ni kwa jina la Yesu Kristo (matendo 16:18) tukiponya viwete ni kwa Jina la Yesu Kristo (Matendo 3:6)


Mafundisho hayo ya kupiga ishara ya msalaba sio mafundisho ya imani ya Kikristo yaliyoletwa na Bwana Wetu Yesu Kristo na mitume wake, hayo ni mapokeo ya wanadamu ambayo yaliingizwa kwa welevu katika imani ya Kikristo kwa lengo la kuwapoteza watu kama yalivyo na mapokeo mengine mengi..

2 Petro 2:1   Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako WAALIMU WA UONGO, WATAKAOINGIZA KWA WEREVU UZUSHI WA KUPOTEZA, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. 

Kumbuka, tunaishi katika siku za mwisho na muda wowote Kristo anakuja kuwanyakua watu wake kama alivyoahidi katika..

Yohana 14:3  Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, NITAKUJA TENA NI WAKARIBISHE KWANGU; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. 


Jiulize, wakati huo Kristo akija kuwanyakua watu wake wewe utakuwa wapi? Hivyo, ikiwa na wewe ulikuwa ni miongoni mwa watu wanaoamini hivyo, basi acha mara moja na umgeukie Mungu kwa kutubu dhambi zako na kumwamini Yesu Kristo, kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kimaandiko ambao ni wa maji tele kwa jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako na kupokea Roho Mtakatifu ambaye atakufundisha kweli na kukufanya uishi maisha ya utakatifu.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Bwana akubariki, Shalom.

 +255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

MMEKWISHA KUSHIBA, MMEKWISHA KUPATA UTAJIRI, MMEMILIKI PASIPO SISI.


JIHADHARI NA WAKINA BALAAMU WA NYAKATI ZA SASA.


UMEFUNGULIWA KAMA BARABA?


Je! Ni dhambi kwa mwanamke wa Kikristo kuvaa suruali?


Ni maungamo gani aliyoyaungama Yesu Kristo mbele ya Pilato?


Ni tabia ipi ya Uungu tutakayoshiriki (kulingana na 2 Petro 1:4)


Nondo ni kitu gani katika biblia?(Mathayo 6:19)


SABURI NI NINI KATIKA BIBLIA?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *