Je! tunawezaje kufahamu kuwa mtu ana Roho Mtakatifu ndani yake?

Biblia kwa kina, Uncategorized 1 Comment

Nakusalimu kwa jina la Yesu Kristo aliye Bwana na Mwokozi wetu. Karibu tuzidi kupeana maarifa ya Elimu ya Ufalme wa Mungu kama tulivyo amriwa na Bwana katika Mithali 4:13.

unaweza kufahamu kama mtu ana Yesu ndani yake kwa mambo makuu mawili SIFA na MATUNDA yake

Tukianza na Sifa; hizi ni zile Sifa za Roho Mtakatifu alizonazo ambazo humuambukiza mtu aliye mpokea. Roho Mtakatifu ana sifa nyingi ila anazo kuu mbili nazo ni UTAKATIFU na UPOLE (unyenyekevu)

Tukianza na UTAKATIFU: Neno linasema;

1 Wakorintho 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana HEKALU LA MUNGU NI TAKATIFU, ambalo ndilo ninyi.”

Roho Mtakatifu hakai sehemu isiyo takatifu. Kama mtu anasema ameokoka lakini bado ni msengenyaji, muongo, mzinzi wa sirisiri, mtukanaji, mtu wa visasi, si mwepesi wa kusamehe, anavaa sawa na watu wa kidunia (suruali kwa wadada, mavazi yasiyousitiri mwili wake wote na kuacha baadhi ya sehemu wazi kama mapaja, matiti, kitovu au tumbo, mgongo, na nguo zinazoonesha ndani), mlevi na mengine kama hayo basi jua hana Roho wa Mungu ndani yake.

Wakristo wengi leo wanajihesabia kuwa ni wa Kristo na wataenda Mbinguni kisa amemkiri Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wake na anaenda Kanisani, anatoa sadaka, anaimba kwaya, anafanya uinjilisti (anahubiri), anajihusisha na shughuli za Kanisani au kupost akiwa anaimba nyimbo za injili kwenye status zake za WhatsApp, Facebook na Instagram. Au kupost mahubiri na mistari ya Neno la Mungu kutoka kwenye Biblia takatifu.

Ni kweli hayo mambo ni mema ila bila kuwa mtakatifu ndugu yangu Mbinguni utapasikia tu, tubu dhambi leo na mruhusu Yesu akupe Roho wake Mtakatifu akubadilishe maisha yako. Kumbuka Bwana Yesu alisema haki yetu isipozidi ya mafarisayo hatutoingia kamwe Mbinguni (Mathayo 5:20) sasa kama ni msomaji wa Biblia utaona jinsi Mafarisayo walivyokuwa wanalisoma Neno (maana walikuwa walimu wa torati), watoaji wa sadaka na waombaji wazuri ila shida ni hawakuwa watakatifu mbele za Mungu, wanatenda dhambi kisirisiri.

Waebrania 12:14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;

Sifa nyingine ya Roho Mtakatifu ni UPOLE

Ametumia ishara ya Hua/Njiwa kiumbe mpole/mtulivu kama ishara ya Yeye kuwa hivyo MPOLE/Mtulivu (Mathayo 3:16). Kama tunavyomfahamu njiwa ni ndege mtulivu sana na hakai sehemu yenye fujo na siku zote ukiona njiwa anatua juu ya mtu ujue huyo mtu ni mtaratibu hana vurugu.

Hukaa kwa mtu mwenye asili ya Upole.

Mathayo 11:29 “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

Mtu akiwa hawezi kujishusha hata kidogo muda wote yeye yuko juu, yeye ndiye anajua kila kitu, yeye ndie anaweza kila kitu, yeye ndiyo yuko sahihi kila wakati, si mwepesi wa kusamehe mtu wa visasi na ugomvi si mpenda amani ujue huyo hana Roho wa Kristo ndani yake.

Angalizo: kama mtu hana hizo sifa mbili za Roho Mtakatifu hata kama ananena kwa lugha masaa 24 hana Roho wa Mungu ndani yake kwani hata mapepo nayo yananena kwa lugha. Mfano mzuri waganga wa kichawi nao si wananena kwa lugha wakizama rohoni wakiwa wanaagua. Bwana amesema zichunguzeni hizo roho maana si kila roho yatoka kwa Mungu >(1 Yohana 4:1)

Jambo la pili ni MATUNDA

Pia tutamjua mtu alie na Roho wa Kristo kwa matunda yake sawasawa na Neno la Mungu katika;

Wagalatia 5:22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.

Umeona kama mtu hana Upendo wa kiMungu ndani yake (soma: 1wakorintho 13:4-8 kwa ufafanuzi juu ya upendo wa kweli ni upi), si mtu wa furaha ni mtu wa gubu tu, si mpenda amani mtu wa mafarakano tu, si mtu wa subira (hawezi kuvumilia), si mtu wa fadhiri (mchoyo), wala si mtu wa kuaminika huyo hata kama anakesha Kanisani kuomba au hata kama ndiye muhubiri wa Kanisa ujue hana Roho wa Kristo ndani yake.

Je, tunampataje Roho Mtakatifu?

Jibu: tunampokea Roho wa Kristo kwa kufuata hatua hizi tatu muhimu kwa uaminifu wa mioyo yetu.

  1. Kumuamini Yesu Kristo kuwa ndiye Bwana na Mwokozi wako na kuwa alikufa kwa ajili ya dhambi zako na kuwa tayari kumpa maisha yako na kuachana na mambo maovu ya duniani
  2. Kutubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha (kumbuka toba sio yale maneno unayoongozwa useme na Mtumishi, hapana, bali uamuzi wako wa ndani wa kuacha dhambi na kumgeukia Mungu ndiyo toba yenyewe yale maneno ni udhihirisho wa toba yako)
  3. Kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo.

Ukikamilisha hizo hatua tatu basi utaanza kuona udhihirisho wa Roho Mtakatifu ndani yako sawa sawa na tuliyoyajadili leo.

Matendo ya Mitume 2:38 Petroakawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, NANYI MTAMPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU.

KUMBUKA: Bwana Yesu yu karibu kurudi na anakuja kuchukua walio wake na bila kuwa na Roho wa Mungu wewe si wa Mungu (warumi 8:9)

Bwana akubariki.


Mada zinginezo:

Je! Yohana mbatizaji alibatizwa na nani?


Je! Kuna Mungu wawili? (Kulingana na Yohana 1:1)


ITAMBUE NA KUIFANYA HUDUMA YA YOHANA MBATIZAJI  KATIKA UKRISTO WAKO.


Je! Bwana Yesu alikuwa ni mdhambi kulingana na Mathayo 3:6? 

Kwanini wale askari hawakumvunja miguu Bwana Yesu?(Yohana 19:36)

One Reply to “Je! tunawezaje kufahamu kuwa mtu ana Roho Mtakatifu ndani yake?”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *