UMEMWAMINI YESU KRISTO KWA NAMNA GANI?

Biblia kwa kina, Uncategorized No Comments

Umeshawahi kujiuliza kwanini Bwana Yesu alisema “amuaminiye yeye haukumiwi (Yohana 3:18)” harafu baadae anakuja na kusema tena “ANIAMINIYE MIMI KAMA VILE MAANDIKO YALIVYONENA? Umeshawahi tafakari kwa umakini maneno hayo ya Bwana?

Yohana 7:38  ANIAMINIYE MIMI, KAMA VILE MAANDIKO YALIVYONENA, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. 

Bwana alisema hivyo kusudi kabisa kwa lengo la kutupa onyo sisi watu wa siku hizi za mwisho, kwani alifahamu kabisa kuwa, kutatokea watumishi wengi wa uongo watakaohubiri na kufundisha kwa jina lake na kuwafanya watu wengi wamwamini Yeye lakini kwa lengo la kuwadanganya, na ndio maana Bwana akaweka msisitizo kwa kusema, ANIAMINIYE MIMI, KAMA VILE MAANDIKO YALIVYONENA, ikiwa na maana kwamba, unaweza mwamini Yesu Kristo ila kivingine kabisa, tofauti kabisa na maandiko yalivyosema, na mwisho wa siku ukaishia kukataliwa.

Leo hii watu wengi tunamwamini Kristo lakini si kama vile maandiko yalivyonena, tunamwamini Yesu Kristo kama mawazo yetu yanavyonena, kama elimu zetu na tamaa zetu zinavyonena, tunamwamini Yesu Kristo kama maaskofu wetu na viongozi wetu wanavyonena na sio kama maandiko yanavyonena.

Kwa mfano; vijana wengi leo hii wanamwamini Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao lakini bado wanapenda starehe na anasa za dunia hii, bado wapapenda party na night clubs, miziki ya kidunia na fashion za kila namna,  tofauti kabisa na maandiko yanavyosema…

1 Petro 4:2  Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani.

 3 Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali; 

Watu wengi wanamwamini Kristo kwa dhati, na kukesha na kuomba, lakini wanafundishwa na viongozi wao chuki, wivu, na visasi juu ya majirani zao na ndugu zao, tofauti kabisa na maandiko yanavyosema..

Walawi 19:18  Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana. 

Wengi wanafundishwa na kufundisha kupigana na kuwapiga adui zao kwenye maombi ya vita kwa jina la Yesu, kitu ambacho ni tofauti kabisa na maandiko yanavyosema na huku wanadai wamemwamini Kristo. Wengine wanachonga masanamu na kuyaabudu kinyume ma maandiko, wanawaomba watu waliokufa kinyume na maandiko. Lakini wamemwamimi Kristo na wana juhudi sana kwenye hivyo ila si katika maarifa kama biblia inavyosema…

Warumi 10:2  Kwa maana nawashuhudia kwamba wana JUHUDI KWA AJILI YA MUNGU, LAKINI SI KATIKA MAARIFA.

Wengine wamemwamini Kristo lakini wanavaa mavazi ya kikahaba (suruali na nusu uchi kwa wanawake, mavazi ambayo ni machukizo kwa Mungu), tofauti kabisa na maandiko yanavyosema na viongozi wao wanawaficha ukweli.

Wengine wanapinga maagizo ya Mungu kama ubatizo, kushiriki meza ya Bwana, kutawadhana miguu, wanawake kufunika vichwa wakati wa ibada na wanadai wamemwamini Kristo.

Ndugu unayesema umemwamini Kristo, chunguza mara mbili mbili ni kwa namna gani umemwamini Yesu Kristo, je! Ni kama dini yako na dhehebu lako linavyosema au ni kama maandiko yanavyosema? Huna budi kuchunguza na kuona ni kwa jinsi gani umeaminishwa Kristo katika maisha yako, hebu watafakari watu wa Beroya waliohubiriwa injili na Paulo pamoja na Sila nabii, hawakujali Kama Sila ni nabii wala hawakujali kama Paulo alitokewa na Bwana hadi kupofuka macho, vyote walivyohubiriwa kuhusu Kristo walitazama kama vinaendana na maandiko..

Matendo Ya Mitume 17:11  Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. 

Sasa inakuwaje wewe ambaye kwa sababu tu kiongozi wako anafanya miujiza, au kasomea biblia miaka kadhaa, au anavaa joho kubwa na msalaba mkubwa shingoni hutaki kuchunguza maandiko ili uone ni kwa jinsi gani umeaminishwa Yesu Kristo katika maisha yako?

Kumbuka: Dhehebu lako au miujiza ya nabii wako haiwezi kukupa wokovu. Hivyo basi, ni muhimu sana imani yako kwa Yesu Kristo iwe kama maandiko yanavyosema, kwani kwa hivyo tutaweza upata wokovu.

2 Timotheo 3:15  na ya kuwa tangu utoto umeyajua MAANDIKO MATAKATIFU, AMBAYO YAWEZA KUKUHEKIMISHA HATA UPATE  WOKOVU KWA IMANI ILIYO KATIKA KRISTO YESU.      

Bwana akubariki, Shalom.

Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.

+255652274252/ +255789001312


Mada zingizeno:

LAKINI KWA NENO LAKO NITAZISHUSHA NYAVU.


HULITUMA NENO LAKE, HUWAPONYA, HUWATOA KATIKA MAANGAMIZO YAO.


Je! ni kweli karama ya kunena kwa Lugha haikupewa kipaumbele na mtume Paulo kama yafanyavyo baadhi ya makanisa leo hii?


Jifunze tabia hii kutoka kwa mtume Paulo.


UNAKO BISHA HODI NDIKO UTAKAKO FUNGULIWA, UNACHOKITAFUTA, NDICHO UTAKACHOKIONA


UMEFUNGULIWA KAMA BARABA?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *