Shalom, jina la Bwana lipewe sifa milele na milele. Karibu tuyatafakari maneno ya Mungu ya maandiko matakatifu ya biblia ili tuweze kutenda sawa kwa neema ile tuliyoipokea kwa Bwana Yesu kama alivyoambiwa mtumishi wa Mungu Yoshua.
Yoshua 1:8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.
Nataka leo tujifunze tabia ya mtu mmoja katika biblia, ambayo itatutia nguvu za kutufanya tusonge mbele zaidi katika safari yetu ya wokovu hapa duniani, na mtu huyu ambaye tutajifunza kutoka kwake si mwengine bali ni KORNELIO. Kama wewe ni msomaji wa biblia, utagundua tabia moja ambayo mtu huyu alikuwa nayo katika maisha yake ambayo ni KUMWOMBA MUNGU DAIMA. Mtu huyu alikuwa akimwomba Mungu daima katika maisha yake, sasa unaweza jiuliza ni kwa namna gani? Inawezekana alikuwa anatenga muda peke yake na kumwomba Mungu huko, au alikuwa akikusanyika na ndugu wengine, lakini daima alimwomba Mungu, na inawezekana si kila alipoomba, basi, Mungu alimjibu hapo hapo, hapana. Inawezekana kabisa kuna wakati aliomba lakini hakuona chochote, lakini hicho kitu hakikumzuia yeye KUMWOMBA MUNGU DAIMA. Hakujali kuwa anapoteza muda mwingi katika kumwomba Mungu, yeye aliendelea tu na tabia yake hiyo hiyo, hebu vuta picha, unatumia nusu saa au zaidi kuwa uweponi mwa Mungu na huoni badiliko lolote la kimwili katika maisha yako, ni wazi kuwa, utaona kama unachokifanya hakina faida. Lakini wazo kama hilo halikuwepo katika akili ya Kornelio, yeye alidumu katika kumwomba Mungu daima na hadi kuna siku malaika alimtokea katika maono wazi wazi, tena mchana na kumfunulia siri ya maombi yake aliyokuwa akiyafanya daima ya kwamba, maombi yake yamekuwa ukumbosho mbele za Mungu.
Matendo Ya Mitume 10:1 Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,
2 mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, NA KUMWOMBA MUNGU DAIMA.
3 Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio!
4 Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, SALA zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.
Ndugu yangu uliyeokoka, wewe unaweza usitokewe na malaika katika maono na kupewa siri ya maombi yako unayoyafanya kila siku, lakini fahamu kuwa, maombi yako unayoyafanya mbele za Mungu kila siku katika maisha yako, Mungu anayatazama kwa namna nyingine kama yalivyokuwa ya Kornelio, inawezekana kila jumapili unaenda kanisani, kila ijumaa unaenda kwenye mkesha wa maombi, unashiriki ibada zote kanisani lakini usione chochote, usikate tamaa, endelea KUMWOMBA MUNGU DAIMA, maombi yako yanafanyika kuwa ukumbusho mbele za Mungu na ndio maana maandiko yanasisitiza kuwa tuombe, tena bila kukoma.
1 Wathesalonike 5:17 ombeni bila kukoma;
Inawezekana unajitolea kufanya kitu fulani kwaajiri ya Mungu na huoni chochote, usikate tamaa, Mungu anakitazama hicho kwa namna nyingine.
Lakini katika kuomba kwetu tunapaswa tuwe watakatifu, na wacha Mungu, tuwe watakatifu katika miili yetu na roho zetu ili maombi yetu yampendeze Mungu, kwani, kwani pasipo huo utakatifu ndani ya Yesu Kristo, hakuna mtu atakaye mwona Mungu, tupaswa tumwabudu Mungu katika uzuri wa utakatifu. Hivyo nikutie moyo ndugu yangu unayetoa muda wako kwa Mungu aliye hai na kuishi misha ya utauwa katika Yesu Kristo kuwa, hujapoteza kitu.
Na pia kama bado hujamwamini Bwana Yesu na kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu, fanya hivyo kama Kornelio alivyoamini injili na kubatizwa.
Bwana akubariki. Shalom.
Mada zinginezo:
Kusaga meno, ni nini kama inavyozungumziwa katika maandiko?
Bawabu ni nani na hufanya kazi gani?