Jina la Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristo litukuzwe, sifa na Utukufu ni vyake milele na milele, Amina. Ulishawahi kujiuliza Kwanini mtume Paulo kwa uweza wa Roho aliandika “BWANA NDIYE ROHO”?
2 Wakorintho 3:17 BASI ‘BWANA’ NDIYE ROHO; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru.
Wakristo wengi sasa hivi kutokana na uchanga wa kiroho (Waebrania 5:13), wanapitia shida katika kumwelewa Mungu na kudhani kuwa Kuna Mungu watatu au Mungu amegawanyika katika sehemu tatu, na wengine kupelekea kupata shida ya kutokujua ni nani wa kumwomba kati ya hao watatu, Je! Baba, Mwana au Roho Mtakatifu. Nakumbuka hata mimi katika safari yangu ya kumjua Mungu, nilishawahi pitia hali kama hii kutokana na mapokeo niliyokuwa nayo tangu utotoni mwangu kwamba, Mungu ana nafsi tatu, kitu ambacho si sahihi hata kidogo, Mungu ni mmoja na ana nafsi moja tu (Isaya 45:23), Naye ndiye Yesu Kristo, Bwana wa mabwana, Mfalme wa wafalme, Mwenye uweza peke yake, Mungu Mwenye kuhimidiwa milele, Amina.
Warumi 9:4 ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake;
5 ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka KRISTO KWA JINSI YA MWILI. NDIYE ALIYE JUU YA MAMBO YOTE, MUNGU, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.
Yeye ndiye Bwana na pia Ndiye Roho, Sasa ili tuelewe Kwanini Bwana ndiye Roho (na Kumbuka Bwana ni mmoja tu, na ndiye Mungu wa Israeli) Tusome vifungu vifuatavyo.
Marko 13:11 Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lo lote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu.
Harafu soma tena..
Luka 21:14 Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu;
15 kwa sababu MIMI NITAWAPA KINYWA NA HEKIMA ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga.
Umeona hapo? Bwana aliwaambia wanafunzi wake kuwa, watakapo chukuliwa mbele ya mabaraza na wafalme, wasifikiri fikiri jinsi watakavyosema kwa sababu YEYE MWENYEWE (Bwana), atawapa kinywa cha kusema, harafu sehemu Nyingine anasema mtakalopewa mbele ya mabaraza semeni mlilopewa kwa sababu ROHO MTAKATIFU (Roho), kawapa hilo, sasa ni nani aliyewapa neno la kusema? Ni Bwana au Roho? Unaona hapo? Hivyo utakuja kugundua kuwa, ni Mmoja tu huyo huyo na si wawili (Siri ya Uungu ni Kuu mno), na ndio maana mtume Paulo alisema
2 Wakorintho 3:17 BASI ‘BWANA’ NDIYE ROHO; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru.
Na ROHO ndiye Mungu ambaye ndiye Bwana Yesu Kristo, ambaye atakapodhihirishwa tutafanana naye kwamaana tutamwona kama alivyo.
1 Yohana 3:2 Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.
Bwana akubariki, Shalom.
Mada zinginezo:
FAHAMU NINI MAANA YA MUNGU NI ROHO (Yohana 4:24)
Ni tabia ipi ya Uungu tutakayoshiriki (kulingana na 2 Petro 1:4)
Bwana Yesu si Mungu mweza yote (Baba) kulingana na Yohana 14:28?
Ni Mungu gani tutakayemwona na kufanana nae atakapodhihirishwa? (1 Yohana 3:2)