DAIMA HUWAAMBIA WAO WANAONIDHARAU, BWANA AMESEMA, MTAKUWA NA AMANI.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele, Yeye ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Mungu Mwenye kuhimidiwa milele, Amina.

Biblia inasema katika..

Yeremia 23:16 Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana.

17 DAIMA HUWAAMBIA WAO WANAONIDHARAU, BWANA AMESEMA, MTAKUWA NA AMANI; nao humwambia kila mtu aendaye kwa ukaidi wa moyo wake, Hamtapatwa na ubaya wo wote. 

Moja ya watu ambao Bwana aliwakemea sana katika taifa la Israeli ni manabii wa uongo, manabii ambao walioshindwa kuwa waminifu kwa Bwana na kufuata tamaa zao wenyewe, waliojaa machukizo, wazinzi, watendao maovu na kushindwa kuwakemea watu kuacha njia zao mbaya (Yeremia 23:14).


Katika agano lake, manabii hawa daima walikuwa wakisema maneno ya uongo ya amani kwa watu waovu, watu walio asi maagizo ya Bwana na sheria zake, (watu wanaodharau Bwana), watu waendao katika ukaidi wa njia zao mbaya na za baba zao, kwamba hamtapatwa na ubaya wowote ule, mtaishi kwa amani, Bwana atawafanikisha n.k, maneno ambayo yapo kinyume kabisa na sheria ya Bwana kwa sababu, Bwana Mwenyewe alishawaweka wazi tangu zamani kuwa, endapo wataikataa na kutoifuata sheria yake mabaya na laana zitawapata.

Kumbukumbu La Torati 28:15 Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata. 

Umeona hapo? Hivyo ndivyo walivyokuwa wakifanya manabii hao wa uongo. Lakini hata sasa hivi katika siku hizi za mwisho, Bwana Yesu alishatuonya na kututahadharisha juu ya ujio wa manabii kama hao, ambao daima huwaambia watu wanaomdharau Bwana kuwa, mtakuwa na amani na huku wanawadanganya.

Matayo 24:11 Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. 

Sasa kumbuka, Bwana alioposema manabii wengi wa uongo watatokea alimaanisha pia Waalimu wa uongo, wachungaji wa uongo, mitume na wainjilisti wa uongo, ambao wanakuja kwa kivuli kile kile cha wale wa agano la kale, watu wanaogoshi neno la Mungu kwa kukataa kuwahubiria watu injili ya kweli, Injili itakayowaepusha na Jehanam ya moto.

2 Petro 2:1 Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, KAMA VILE KWENU KUTAKAVYOKUWAKO WAALIMU WA UONGO, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. 

Ndugu mpendwa, ikiwa wewe hadi leo hii bado ni mlevi, mvutaji wa sigara, unaishi na mtu usiyefunga nae ndoa, unaishi na mke wa mtu au mume wa mtu, ni mfiraji na mlawiti, mtukanaji na msengenyaji, mla rushwa na mdhalimu, mtazamaji pornography, una beti, miziki ya kidunia na anasa ni wewe, unazisujudia sanamu za Mariamu na Yesu, unawaomba wafu, unavaa suruali mwanamke, unavaa gauni na sketi mwanamume, unavaa vimini, make ups, hereni, kusuka nywele, mawigi na nywele bandia (rasta), unajichubua ngozi yako, basi tambua kuwa wewe ni miongoni mwa WATU WANAOMDHARAU BWANA (kwa sababu Mungu kakataza yote hayo lakini wewe bado unayafanya), na tena, unahubiriwa uchumi na mchungaji wako, unahubiriwa majumba na mafanikio, (injili ambayo Bwana hajaiagiza), basi lisikie neno hili la Bwana wa Majeshi, “tubu dhambi zako (Matendo 2:38), maana unamdharau Bwana, na tena usiwasikile watumishi wa uongo wanaokufundisha maneno ya ubatili kwamba hutopatwa na mabaya yoyote wakati wewe ni mkaidi

Yeremia 23:16 Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana.

17 DAIMA HUWAAMBIA WAO WANAONIDHARAU, BWANA AMESEMA, MTAKUWA NA AMANI; nao humwambia kila mtu aendaye kwa ukaidi wa moyo wake, Hamtapatwa na ubaya wo wote.

Bwana akubariki, Shalom.

Tafadhari washirikishe na wengine ujumbe huu.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

GEUKA KATIKA NJIA YAKO NA IRUDIE NJIA YA MUNGU.


JE! UMEIAMINI INJILI IPI?


FUNZO KATIKA HABARI YA MFALME AHABU NA NABII MIKAYA


Nini maana ya mstari huu “unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya wanadamu” (2 Petro 2:21) 


AGIZO LA MUNGU KWA WATU WOTE.

LEAVE A COMMENT