GEUKA KATIKA NJIA YAKO NA IRUDIE NJIA YA MUNGU.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Jina la Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele, Yeye ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Mungu Mkuu na Mwokozi Wetu, sifa na Utukufu ni vyake milele na milele, Amina. 

Sababu ya Kristo kuja duniani na kufa msalabani, ilikuwa ni kuwakusanya wanadamu wote waliopotea katika dhambi kama kondoo na kuwaleta pamoja, na lengo la kuwaleta pamoja ni kwamba, kila kila mtu alikuwa akitembea katika njia yake mwenyewe gizani, huyu katika njia hii na huyu katika njia ile, ndipo sasa Kristo alipokuja kama mchungaji kwa lengo la kutukusanya kutoka katika njia hizo na kuwaleta wanadamu pamoja, ndivyo maandiko yanasema.

Ezekieli 34:12 Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; NDIVYO NITAKAVYOWATAFUTA KONDOO ZANGU; NAMI NITAWAOKOA KATIKA MAHALI POTE WALIOPOTAWANYIKA, katika siku ya mawingu na giza. 

Lakini sio tu kutukusanya na kututoa katika njia zetu, bali pia na kutuepusha kutoka katika hukumu ya Mungu, na kutupatia uzima wa milele, na tena tuwe nao tele.

Yohana 10:10 Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; MIMI NALIKUJA ILI WAWE NA UZIMA, KISHA WAWE NAO TELE.

Na ndio maana utaona Wakati Bwana alipokuwa duniani, Watu wengi sana waliokuwa wakitembea katika njia zao tofauti tofauti hapo mwanzo, waligeuka katika hizo, na kuanza kuifuata njia ya sahihi ya Mungu ambayo ni Yesu Kristo (Yohana 14:6), Kwamfano; Utaona watoza ushuru na matajiri kama Zakayo, ambao hapo mwanzo walikuwa wanyang’anyi na  watu wa dhuruma, waliacha njia zao hizo zisizo za haki na kurudi katika njia ya Mungu 

Luka 19:8 Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.

9 Yesu akamwambia, LEO WOKOVU UMEFIKA NYUMBANI HUMU, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. 

Lakini si hivyo tu, hata Mafarisayo na watu wa mabaraza, pia nao waligeuka kutoka katika njia zao na kumfuata Kristo njia ya Mungu, mfano Nikodemo na Yusufu wa Armathaya (Yohana 19 :38-39), mbali na hao, walikuwepo pia Wanawake makahaba, Maakida, Vipofu, ndugu za wafalme, na wengine, wote hawa waligeuka katika njia zao na kuifuata njia ya Mungu, kwa sababu Kristo alikuja kwa kusudi la kuwatoa watu katika njia zao na kuwaleta katika njia ya kweli na ya haki, njia ielekeayo uzimani, Hiyo ndio kanuni ya Kristo, kwamba akija katika maisha yako ni lazima akutoe katika njia yako isiyo sahihi na kukuleta katika njia iliyo sahihi, njia ya Uzima, kwani alikuja kutafuta kilichopotea. 

Luka 19:10 KWA KUWA MWANA WA ADAMU ALIKUJA KUTAFUTA NA KUOKOA KILE KILICHOPOTEA.

Sasa Inawezekana na wewe leo hii Kristo amekuja kwako (kwa kupitia injili), wakati ambao wewe tayari upo katika njia yako kama ilivyokuwa kwa wanyang’anyi na makahaba, ambayo katika hiyo, umetembea kwa muda mrefu sana, labda miaka kadha, na pengine njia yako hiyo imekunufaisha au inakunufaisha na kukupa faida nyingi sana, au sifa na umaarufu fulani, lakini Kristo anapokuja katika maisha yako kanuni yake ni ile ile, ni  kukutoa katika hiyo njia yako ambayo mwisho wake ni Jehanam na kukuleta katika njia ya Uzima, hivyo huna budi KUGEUKA KATIKA HIYO NJIA YAKO bila kujali gharama na kuanza kutembea katika njia ya Mungu (Yohana 14:16) 


Labda wewe ni mwanamziki wa kidunia mwanamke, unavaa nusu uchi katika kazi yako hiyo, na tena kupitia hiyo unapata umaarufu na faida nyingi sana. Au pengine wewe ni mwanamziki wa kidunia mwanamume, unatangaza ufalme wa giza kwa kuimba mapenzi, uhuni, na nyimbo zinazosifia pombe, unachora tattoos, n.k, fahamu kwamba, Kristo anataka kukuokoa, hivyo huna budi KUGEUKA KATIKA HIYO NJIA YAKO bila kujali gharama na kuanza kutembea katika njia ya Mungu (Yohana 14:16), ili uokolewe.


Wewe ni binti, upo katika njia yako ambayo ni kufanya kazi inayokulazimu kwa namna yoyote ile kuvaa mavazi ya kikahaba (Suruali na vimini, nguo zinazochora maungo yako), na umedumu katika hiyo kwa muda mrefu sana na kujipatia faida, na Kristo amekuja kwako kupitia mahubiri, unachotakiwa kufanya ni KUGEUKA KATIKA HIYO NJIA YAKO bila kujali gharama na kuanza kutembea katika njia ya Mungu (Yohana 14:16), ili uokolewe.


Binti/mama unayesoma ujumbe huu, umetoa mimba hujatubu, unavaa nusu uchi, mpenda fasion na anasa, unaishi na mwanamume usiyefunga nae ndoa, umemwacha mumeo na kuolewa na mwanamume mwengine, unaishi na mume wa mtu, tambua unatembea katika njia ya kikahaba, GEUKA NA IRUDIE NJIA YA MUNGU. 


Wewe ni kijana, unatembea katika njia yako ya uasherati, utukanaji, uvutaji sigara, unavaa milegezo, unabeti, mtazamaji wa picha za ngono, mfanyaji musturbration, mtu mwenye kutamani, GEUKA NA IRUDIE NJIA YA MUNGU, Bwana hapendi upote.


Upo katika njia yako ya uchawi na uganga, msujudia sanamu na muomba wafu, mpenda rushwa, GEUKA NA IRUDIE NJIA YA MUNGU, Bwana hapendi upote vinginevyo utaangamia.

Yeremia 18:11 Haya! Basi, ukawaambie watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, ukisema, Bwana asema hivi, Tazama, ninafinyanga mabaya juu yenu, na kuwaza mawazo juu yenu; RUDINI SASA, KILA MMOJA NA AIACHE NJIA YAKE MBAYA; zitengenezeni njia zenu, na matendo yenu. 

Tafadhari washirikishe na wengine ujumbe huu.

Bwana akubariki, Shalom.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

Kwanini Sanduku la Mungu lilitwaliwa na Wafilisti huko shilo? (1 Samweli 4:11)


Je! Agizo la Bwana kwa mitume wake la kufufua wafu lilikuwa ni kwa baadhi ya mitume tu?


NIKAWAONA WAFU, WAKUBWA KWA WADOGO, WAMESIMAMA MBELE YA KITI CHA ENZI.


MCHUNGAJI WAKO NI NANI?


Kwanini Bwana Yesu alijeruhiwa ubavuni pale msalabani?

5 thoughts on - GEUKA KATIKA NJIA YAKO NA IRUDIE NJIA YA MUNGU.

LEAVE A COMMENT