NIKAWAONA WAFU, WAKUBWA KWA WADOGO, WAMESIMAMA MBELE YA KITI CHA ENZI.

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

Je! Wafu wakubwa na wadogo ni wapi hao? 

Ufunuo 20:12 Nikawaona wafu, WAKUBWA KWA WADOGO, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. 

JIBU: Hapo tunaona makundi mawili


kundi la kwanza “WAFU WAKUBWA”

Wafu Wakubwa wanaozungumziwa hapo sio vikongwe, bali ni wafu waliokuwa mashuhuri sana duniani au maarufu, watu waliokuwa na vyeo au ngazi za juu sana wakati walipokuwa hapa duniani, na Mfano wa watu hawa ni kama vile Wafalme, ma-Malkia, ma-Rais, mawaziri, wakuu wa majeshi na majemedari wa vita, ma papa, na watu wengine wote mashuhuri na maarufu unaowafahamu wewe duniani leo hii. Wafu hawa wakubwa (mashuhuri), mtume Yohana aliwaona wamesimama mbele ya kiti cha enzi, wakahukumiwa na kutupwa kwenye ziwa la moto milele na milele kwa sababu hawakutaka kumtii Mungu.


Inawezekana jambo hili likawa ni gumu  kidogo kulisikia lakini ukweli ndivyo ulivyo, kwa sababu kama Mungu malaika zake watakatifu tu! huwahesabia upuzi, Je! si zaidi sana Mfalme wako mdhalimu na mwenda kwa waganga? au malkia wako anayefanya machukizo? Si zaidi sana Majemedari wetu wa vita wavuta sigara, wala rushwa, na watukanaji? Si zaidi sana ma-Rais na mawaziri wetu waongo na waabudu Sanamu? Si zaidi sana huyo mwanamziki wako mwasherati, mlevi na mvaa nusu uchi?

Ayubu 4:18 Tazama, yeye hawategemei watumishi wake; Na malaika zake huwahesabia upuzi; 

19 Je! Si zaidi sana hao wakaao katika nyumba za udongo, Ambazo misingi yao i katika mchanga, Hao waliosetwa mbele ya nondo! 

Kwa sababu neno la Mungu lipo wazi kabisa kuwa, kila afanyaye hayo sehemu yake ni katika ziwa kiwakalo moto na kiberiti, bila kujali yeye ni nani (ufunuo 21:8)

Hivyo, ikiwa na sisi ni miongoni mwa watu wakubwa (mashuhuri) hapa duniani, basi tunapaswa tutambue kwamba, Mungu hashawishiwi na umaarufu wetu, pesa zetu, vyeo vyetu, au shahada na stashahda zetu, bali kwa jinsi tunavyotii maagizo yake na kuishi maisha ya utakatifu kwani ipo siku moja atatuita hukumuni, TUJITATHMINI


Kundi la pili “WAFU WADOGO”

Wafu wadogo wanaozungumziwa hapo ni watu waliokuwa wakishi maisha ya kawaida tu, pasipo umaarufu wala umashuhuri wowote duniani kama ilivyokuwa wale wa kundi la kwanza, na mfano wa wafu hawa ni wafanyakazi wa kawaida tu walioajiliwa sehemu mbali mbali, wakulima, wafugaji, omba omba n.k watu hawa pia mtume Yohana aliwaona wamesimama mbele ya kiti cha enzi, wakahukumiwa sawasawa na matendo yao na kutupwa katika ziwa la moto kwa sababu hawakumtii pia Mungu bali walifanya maovu mbele zake.


Hii inatupa picha kuwa, Mungu hashawishiwi pia na hali zetu za kimaisha kwamba sisi ni maskini sana, au sisi ni yatima, sisi ni wabeba mizigo masokoni, sisi ni wapambanaji wa maisha n.k, hapana! bali kwa jinsi tunavyotii maagizo yake na kuishi maisha ya utakatifu. MKUMBUKE LAZARO


Hivyo, hatuna budi kumpendeza Mungu hata katika unyonge wetu na umaskini wetu kwa kujitenga na kila aina ya uovu, vinginevyo tutaishia Jehanam hata kama sisi ni mayatima, wajane na maskini wa kutupwa, kwa sababu biblia inasema, dhiki na shida juu ya kila nafsi ya mwanadamu itendayo uovu, kwa Myahudi kwanza na Myunani pia, kwa tajiri kwanza na fukara pia, bila ubaguzi

Warumi 2:9 dhiki na shida juu ya kila nafsi ya mwanadamu atendaye uovu, Myahudi kwanza na Myunani pia; 

Bwana atusaidie kuyatambua haya. Shalom.

Tafadhari, washirikishe na wengine ujumbe huu.


Mada zinginezo:

Ni hukumu ipi ya Ibilisi inayozungumziwa katika Waraka wa (1 Timotheo 3:6?)


ONYO..!! EPUKA KUTOA MANENO YA UONGO KATIKA SALA ZAKO.


Tabia moja ya unafiki unayopaswa kuiepuka.


UNAKO BISHA HODI NDIKO UTAKAKO FUNGULIWA, UNACHOKITAFUTA, NDICHO UTAKACHOKIONA


DUMU KATIKA FUNDISHO LA MITUME.

One Reply to “NIKAWAONA WAFU, WAKUBWA KWA WADOGO, WAMESIMAMA MBELE YA KITI CHA ENZI.”

LEAVE A COMMENT