FUNZO KATIKA HABARI YA MFALME AHABU NA NABII MIKAYA

Biblia kwa kina, Uncategorized 3 Comments


Lipo funzo katika habari ya mfalme Ahabu na nabii wa Mungu Mikaya mwana wa Imla, ambalo na sisi watu wa kizazi hiki tunapaswa pia kujifunza na kujirekebisha pindi tusikipo kwa sababu maandiko yanasema, mambo hayo yaliandikwa kwa jinsi ya mifano, ili kutuonya sisi watu wa sasa (1 Wakorintho 10:6).

Lakini endapo tusipotaka kujifunza mifano hiyo na maonyo hayo ya Mungu kwa kubadilika, basi Mungu Naye atatucheka na kutudhihaki siku ile atakapotukataa.

Mithali 1:25 Bali mmebatilisha shauri langu, WALA HAMKUTAKA MAONYO YANGU; 

26 MIMI NAMI NITACHEKA SIKU YA MSIBA WENU, NITADHIHAKI HOFU YENU IFIKAPO; 

Maandiko matakatifu yanasema kuwa, mfalme Ahabu alikuwa anamchukia sana nabii wa Mungu Mikaya, na sababu ya yeye kumchukia nabii huyo ni kuwa, siku zote nabii huyo alikuwa akimtabiria Ahabu mambo mabaya tu (mambo yaliyo kinyume na mapenzi yake).


Sasa siku moja mfalme Ahabu alikusudia kwenda kuupiga Ramoth-gileadi, hivyo akamshawishi Yehoshafati mfalme wa Yuda ambaye alikuja kumtembelea Samaria kama wangepanda pamoja huko Ramoth-gileadi, Yehoshafati mfalme wa Yuda alikubali lakini alisema waulize kwanza kwa Bwana, kwamba waende au la, ndipo Ahabu akaita manabii mia nne (watu wasio mtabiria mabaya), ambao Mungu alitia pepo wa uongo viywani mwao (1 Wafalme 22:23) kwani hawakuwa wakamilifu kwa Mungu, na manabii wote hawa mia nne (400) walimtabiria Ahabu sawasawa na mapenzi yake na tamaa yake.

2 Mambo ya Nyakati 18: 3 Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwambia Yehoshafati, mfalme wa Yuda, Je! Utakwenda nami mpaka Ramoth-gileadi? Akamjibu, Mimi ni kama wewe, na watu wangu kama watu wako; nasi tutakuwa pamoja nawe vitani.

4 Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la Bwana.

5 Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya manabii, watu mia nne; akawaambia, Je! Tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Wakasema, KWEA; KWA KUWA MUNGU ATAUTIA MKONONI MWA MFALME.

Watu hawa wote mia nne walimtabiria mfalme sawa sawa na mawazo yake yeye kama ilivyo kwa watumishi wa uongo wanavyowatabiria na kuwahubira watu kulingana na tamaa zao leo hii, kitu ambacho si sawa hata kidogo, yaani watu wote mia nne wakunenee mema tu wakati wewe ni muovu? Jambo hili lilimshangaza na kumstaajabisha kidogo Yehoshafati mfalme wa Yuda na kuona shaka, hivyo akauliza tena kama hakuna nabii mwengine wa Bwana tofauti na hao mia nne ili waulize kwake, ndipo Ahabu akwamwambia yupo mmoja ila amachukia KWA SABABU HUWA HAMTABIRII MEMA.

2 Mambo ya Nyakati 18: 6 Lakini Yehoshafati akasema, JE! HAYUPO HAPA NABII WA BWANA TENA, ili tumwulize yeye?

7 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, YUPO MTU MMOJA, ambaye tungeweza kumwuliza Bwana kwa yeye; LAKINI NAMCHUKIA; KWA SABABU HANIBASHIRII MEMA KAMWE, ILA SIKU ZOTE MABAYANAYE NDIYE MIKAYA MWANA WA IMLA. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi. 

Na ni kweli kabisa, nabii huyu mwaminifu wa Mungu alipoitwa, alisema kile ambacho Bwana alichomwagiza, bila kupunguza wala kuongeza, kwamba Bwana ametia pepo wa uongo katika vinywa vya manabii wako wote hawa na tena amenena mabaya juu yako (1 Wafalme 22:23), na si hivyo tu, lakini hata pale nabii huyo aliposhawishiwa na mjumbe aliyemfuata kuzungumza mema mbele za mfalme ili kumridhisha na kumfurahisha kama wale wengine, yeye alikataa.

2 Mambo ya Nyakati 18:12 Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, ANGALIA, MANENO YA MANABII KWA KINYWA KIMOJA YAMESEMA MEMA KWA MFALME; NENO LAKO BASI NA LIWE KAMA MOJAWAPO LAO, UKASEME MEMA.

13 Mikaya akasema, Kama aishivyo Bwana, NENO LILE ATAKALOLINENA MUNGU WANGU, NDILO NITAKALOLINENA.

Kwa urefu wa habari hii unaweza soma peke yako katika (2 Mambo ya Nyakati 18:1-34), au (1 Wafame 22:1-17).


NINI TUNATAKIWA KUJIFUNZA HAPO?


Kwa upande wa Ahabu:

Watu wengi leo hii duniani ni kama mfalme Ahabu, wanawachukia watumishi wa Mungu wanaowaambia ukweli na kibaya zaidi wanachukia pale wanapoambiwa ukweli juu matendo yao ya giza, wanapenda kuhubiriwa mafanikio na amani wakati hawataki kuacha maisha ya dhambi, wametelekeza wake zao na waume zao wa ndoa, wanabudu sanamu na waomba wafu, wanashikamana na udunia, vimini kwa wanawake na masuruali, make ups, kucha bandia, kope bandia, n.k. Na huku wanataka kutabiriwa mema na kuhubiriwa kufanikiwa.


Ndugu mpendwa, kama wewe ni mzinzi na mwasherati, muongo na msengenyaji, mtukanaji na mvutaji sigara, mtu wa kupenda anasa na starehe za dunia hii, pombe ni wewe, miziki ya kidunia ni wewe, unavaa kikahaba, unaishi na mume au mke wa mtu, harafu unahubiriwa na mamia ya wamtumishi kwamba utafunguliwa kiuchumi, Bwana atatenda, mwaka huu ni wako, maji na chumvi za upako, utapata hiki na kile, Mungu atakubariki, utafanikiwa (kama tu alivyohubiriwa Ahabu), basi jiulize mara mbili mbili kwa sababu unadanganywa, Mungu anataka wewe utubu dhambi zako na kuiamini injili ili upate wokovu wa roho yako, kwani hakuna amani kwa wabaya.

Isaya 48:22 Hapana amani kwa wabaya, asema Bwana.

Hivyo tubu leo dhambi zako mapema kwa kumwamini Kristo na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi, ambao ni wa kuzamishwa katika maji tele na kwa jina la Yesu Kristo sawasawa na (Matendo 2:38), Maana Bwana amekusudia mabaya juu yako usipotii.


Kwa upande wa nabii Mikaya

Kama wewe ni Mkristo unayeishi kulingana na maagizo ya Mungu, unayesema na kusimama katika neno lake bila kuongeza wala kupunguza, tegemea kupatwa na kile kilichompata nabii Mikaya, yaani kuchukiwa na watu unaowaambia ukweli.


Kama wewe ni kijana mkristo, usitegemee kupendwa na vijana wenzako utapokataa kwenda nao night clubs na sehemu za anasa, usitegemee kupendwa na vijana wenzako unapojitenga na maongezi yao machafu machafu yasiyofaa, watakutenga tu na kukuona waajabu, tegemea kuchukiwa na wenzako unapowaambia uasherati ni dhambi na madhara yake ni moto wa milele, weka hilo akilini.


Kama wewe ni binti mkristo tegemea kuchukiwa na mabinti wenzako unapokataa kuwa kama wao, unapokataa vimini, mapambo, suruali, kuvaa nusu uchi, tegemea tu dhihaka kutoka kwao, kama wewe ni mfanyakazi mkristo tegemea kuchukiwa na bosi wako unapokataa rushwa, tegema kuchukiwa na ndugu zako unapowaambia kuabudu sanamu na kuomba wafu ni machukizo kwa Mungu, kama wewe ni mkristo thabiti tegemea kuwa adui wa ndugu zako unapowaambia ukweli kwamba, kwenda kwa waganga ni dhambi. Simama imara na Bwana kwani ndivyo ilivyo.

Wagalatia 4:16 Je! Nimekuwa adui wenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli? 

Umeona? Hivyo unachopaswa kufanya ni kudumu katika Neno la Mungu (mafundisho ya manabii na mitume watakatifu wa Yesu Kristo), kwani kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na moto wa milele 

Bwana akubariki, Shalom. 

Tafadhari washirikishe na wengine ujumbe huu.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

FUNZO KATIKA HABARI YA DANIELI NA MAANDISHI YALIYOANDIKWA NA VIDOLE VYA MWANADAMU KATIKA UKUTA WA ENZI YA MFALME


Ni mambo ya nyumba ipi ambayo mfalme Hezekia aliambiwa kuyatengeneza? (Isaya 38:1)


YEROBOAMU MWANA WA NEBATI.

KWA SABABU NALIWAOGOPA WALE WATU, NIKATII SAUTI YAO. 


Nini maana ya mstari huu “Hatukuja na kitu duniani, na tena hatuwezi kutoka na kitu? (1 Timotheo 6:7)

3 thoughts on - FUNZO KATIKA HABARI YA MFALME AHABU NA NABII MIKAYA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *