SWALI: kulingana na andiko la kitabu cha Waefeso 5:24 je! Ni sawa kwa mke kumtii mume katika kila jambo ata kama ni uovu? Kwa sababu mume ndiye kichwa cha familia.
Waefeso 5:24 Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo WAKE NAO WAWATII WAUME ZAO KATIKA KILA JAMBO.
JIBU: Ni kweli kabisa kuwa, mume ni kichwa cha familia na mke anapaswa amtii mumewe kama kanisa linavyomtii Kristo, na mume pia anapaswa kumpenda mkewe kama Kristo anavyolipenda kanisa.
Lakini ni tofauti na inavyodhaniwa na wengi kuwa, mke anapaswa kutii kila kitu kutoka kwa mumewe hata kama ni vitu viovu, hivyo kupelekea wake wengi katika ndoa zao kufanya dhambi mbele za Mungu kwa sababu tu wanataka kutimiza na kuwalidhisha waume zao kwa tamaa zao mbaya na ovu mbele za Mungu. Wewe kama mke tambua kuwa, unapaswa kumtii mumeo katika mambo yote YANAYO MPENDEZA MUNGU TU! hupaswi kumtii mume wako katika mambo machafu na maovu.
Wakolosai 3:18 Ninyi wake, watiini waume zenu, KAMA IPENDEZAVYO KATIKA BWANA.
Umeona? Unapaswa kumtii mumeo kama ipendezavyo katika Bwana na wala si katika matakwa ya mumeo, matakwa ya mumeo yanapaswa yasipingane na mapenzi ya Mungu. Mke, hupaswi kutii tamaa mbaya za mume wako kwa kufanya tendo la ndoa kinyume na isivyopaswa, kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unatenda dhambi na kumchukiza Mungu, kwani hilo jambo halipendezi mbele za Bwana.
Mke, tambua kuwa, hupaswi kumtii mume wako, pale anapokwambia na wewe uweke make up, lipstick, kujichubua na kuweka manywele bandia na makucha bandia, au uvae mtaani mavazi ambayo ni machukizo mbele za Mungu kama vile suruali, taiti, vimini, nguo za migongo wazi na kifua wazi ili uendane na wakati na uwe kama wanawake wa kisasa, hupaswi kumtii katika hivyo kabisa, hivyo vitu havipendezi mbele za Mungu, wewe unapaswa umtii Mungu anayesema mwanamke avae mavazi ya kujisitiri na adabu nzuri, si kwa kusuka nywele wala kujipamba kwa dhahabu na lulu.
Hupaswi kumtii mume wako anayekwambia twende kwa mganga wa kienyeji au twende ukatoe hii mimba au twende ukaweke vitanzi vya kuzuia mimba kwenye mfumo wako wa uzazi au twende kunywa pombe, hupaswi kumtii kwani, hayo yote hayapendezi mbele za Bwana, kinyume chake unapaswa umwelekeze na kumwambia kwa heshima, busara, na upendo wote kuwa, hivi vitu si sawa mbele za Mungu na ni machukizo. Haijalishi unampenda kiasi gani na unataka umridhishe kiasi gani, katika mambo hayo maovu hupaswi kumtii yeye bali Kristo, kwani yoyote apendaye kufanya mapenzi maovu ya mama yake au mume wake hamstahili Kristo.
Na wewe mume uliyeokoka, hupaswi kumshawishi mke wako kufanya mambo maovu kwa sababu ya tamaa zako, kama Kristo asivyo taka kanisa kufanya matendo maovu yasiyo mpendeza Mungu, na waume nao vivyo hivyo, hawapaswi kuwafanya wake zao wawati katika matendo maovu.
Hivyo kwa kuhitimisha ni kuwa, mwanamke aliyeokoka anapaswa kumtii mume wake katika mambo yote lakini yampendezayo Bwana tu na wala si vinginevyo.
Bwana akubariki, Shalom.
Ikiwa bado hujampa Kristo maisha yako, basi, jua kwamba neema hii haitadumu milele, hivyo amua leo kumpokea Kristo ili uwe na uhakika wa uzima wa milele.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
+255652274252/ +255789001312
MADA ZINGINEZO:
Je! Waraka wa mtume Paulo kwa Wakorintho, ulikuwa ni kwaajiri ya Wakorintho pekee?
BWANA ALIMAANISHA NINI ALIPOSEMA “HAPA YUPO ALIYE MKUU KULIKO HEKALU?”