FUNDISHO MAALUMU KWA WALIOMWAMINI NA KUMPOKEA YESU KRISTO.
Jina la Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristo lihimidiwe milele na milele, hii ni sehemu ya pili ya fundisho maalumu linaloangazia kazi nyingine ya maandiko matakatifu kwa wafuasi wa Yesu Kristo (wote waliomwamini Yesu), katika sehemu ya kwanza tulitazama sifa na vigezo vya mfuasi wa Yesu Kristo kulingana na maandiko matakatifu (na sio kulingana na dini yako, wala dhehebu lako, bali kulingana na maandiko matakatifu), hivyo ni wajibu wako wewe kujihakiki vyema ili kuona kama umekuwa mfuasi wa Yesu Kristo kweli Kweli kulingana na maandiko matakatifu, tofauti na hapo umedanganywa, unajidanganya na utaendelea kudanganywa kama usipotaka kuitii Injili ya kweli.
Na hii ni Sehemu ya pili. Karibu!
Mtu yo yote yule anapozaliwa mara ya pili kwa maji na Roho kulingana na maandiko matakatifu, haina maana kuwa ndio ameshamaliza kila kitu, hapana! Bali ipo kazi nyingine ya maandiko matakatifu juu ya mtu huyo, na kazi hiyo sio nyingine zaidi ya kumtakasa na kumkamilisha mtu huyo ili apate kuwa kamili, hiyo ndio kazi nyingine ya maandiko matakatifu kwako wewe mtu wa Mungu.
2 Timotheo 3:16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu MAKOSA YAO, NA KWA KUWAONGOZA, NA KWA KUWAADIBISHA KATIKA HAKI;
17 ILI MTU WA MUNGU AWE KAMILI, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.
Lakini kinachoendelea leo hii miongoni mwa watu wa Mungu ni tofauti kabisa, hatutaki kuonywa makosa yetu kwa maandiko matakatifu, tunapoona jambo fulani tulilokuwa tunaliamini au kulifanya kwa muda mrefu linapingana na maandiko, basi inakuwa ni ngumu kwetu kulitupilia mbali na kutii maandiko matakatifu, hivyo tunaanza kutanguliza mbele akili zetu, mawazo yetu, na maoni yetu, kusudi tusijiumize hisia zetu.
Au inakuwa ni ngumu kukubali kuwa, kwa muda wote huo hatukuwa sawa hivyo Mungu kwa upendo Wake kwetu sisi watoto wake, anatusahihisha, kutuonya na kutukamilisha kwa maandiko Yake hivyo tunakuwa wagumu kwa sababu tu maandiko hayo yanaumiza hisia zetu.
Ndugu mpendwa, ikiwa kazi moja ya maandiko matakatifu ni kukuonya makosa yako (mtu wa Mungu), ili upate kuwa kamili, basi tegemea pia kuumizwa hisia zako kwa sababu ukweli wa neno (maandiko), siku zote haufurahishi tu unapousikia, bali unaumiza pia na kuchoma, kukata kata na kuvunja vunja vitu vitu vinavyopingana na Mungu ndani yetu.
Waebrania 4:12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Soma tena.
Yeremia 23:29 JE! NENO LANGU SI KAMA MOTO? Asema Bwana; NA KAMA NYUNDO IVUNYAYO MAWE VIPANDE VIPANDE?
Hivyo fanyia kazi vyote unavyorekebishwa na Mungu kwa kupitia maandiko matakatifu unayoyasoma, pasipo kujali kama maandiko hayo yanapingana na mawazo yako na kukuumiza hisia zako, wewe litii neno, bila kujali hapo mwanzo ulikuwa unaamini, kwani kwa kufanya hivyo ndivyo utakavyozidi kuwa mkamilifu na kutakaswa kwa maandiko matakatifu (neno) kama Bwana alivyosema katika.
Yohana 17:17 UWATAKASE KWA ILE KWELI; NENO LAKO NDIYO KWELI.
Bwana akubariki, Shalom.
Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.
+255652274252/ +255789001312
Mada zinginezo:
IJAPOKUWA NALIWAUZUNISHA KWA WARAKA ULE, SIJUTI
KAZI NYINGINE YA MAANDIKO MATAKATIFU KWA WAFUASI WA YESU KRISTO (SEHEMU YA KWANZA).
Mjumbe wa agano la kwanza alikuwa ni nani?
Bawabu ni nani na hufanya kazi gani?
JE! KUNA SIRI GANI KWENYE NAMBA AROBAINI (40) KATIKA BIBLIA?