KWANINI BIBLIA INAMFANANISHA IBILISI NA SIMBA ANGURUMAYE?

  Maswali ya Biblia, Uncategorized

Biblia inasema katika 

1 Petro 5:8 Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa MSHITAKI WENU IBILISIKAMA SIMBA ANGURUMAYE, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. 

SWALI: Kwanini maandiko yaseme ibilisi, kama Simba angurumaye?

JIBU: Ipo sababu kwa nini maandiko yamfananishe ibilisi na simba angurumaye, na sio simba angurumaye tu, lakini pia zipo sehemu zingine ambazo maandiko yanamfananisha ibilisi na joka.

Ufunuo 12:7 Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na YULE JOKAYULE JOKA naye akapigana nao pamoja na malaika zake; 

Sehemu zingine ibilisi anafananishwa na nyoka.

Ufunuo 12:9 Yule joka akatupwa, yule mkubwa, NYOKA WA ZAMANIAITWAYE IBILISI NA SHETANI, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. 

Na sifa nyingine nyingi na kadha wa kadha unazozisoma kwenye biblia yako ambazo ibilisi anafananishwa kwazo. 

Lakini hii haina maana kwamba ibilisi ni hicho kiumbe, au ibilisi JOKA, au ibilisi ni NYOKA, au ibilisi ni SIMBA, au ibilisi ana mapembe makubwa na mkia mrefu kama wa kenge, la hasha! Haina maana hiyo hata kidogo, Mungu hakumuumba ibilisi harafu baadae akambadilisha na kuwa nyoka au joka au simba, sivyo hata kidogo, bali ibilisi alikuwa ni Kerubi hapo mwanzo kabla ya kuasi (Ezekiel 28:14). Hivyo Shetani ni kerubi aliyeasi, na  anaweza hata akajibadilisha na kujifanya malaika wa Mungu kabisa na kuwadanganya watu (ndivyo maandiko yanavyosema).

2 Wakorinto 11:14 Wala si ajabu. MAANA SHETANI MWENYEWE HUJIGEUZA AWE MFANO WA MALAIKA WA NURU

Lakini Kwanini maandiko yamlinganishe ibilisi na viumbe hivyo? 

Jibu ni kwamba, ibilisi amefananishwa na viumbe hivyo ili sisi tulio ndani ya Kristo tupate kuzijua janja, mbinu, na hila za ibilisi kwa kupitia sifa walizonazo viumbe hao. 

Ibilisi anapofanishwa na joka, maana yake ni kuwa, kwa kuzitambua sifa za joka, basi tutaweza kumtambua ibilisi na mbinu zake, pia ibilisi anapofananishwa na nyoka, maana yake ni kuwa, kwa kuzichunguza sifa za nyoka tutaweza kuzijua hila na mbinu za ibilisi anazozitumia pale anapotaka kuwaangusha watu. Hivyo ndivyo ilivyo na kwa simba angurumaye pia anapofananishwa na ibilisi, maana yake ni kwamba, tukizijua sifa za simba angurumaye ndipo tutakapojua mbinu na hila za ibilisi juu yetu.

Sasa katika hali ya kawaida, ngurumo ya simba lengo lake kubwa siku zote huwa ni kuleta hofu kwa maadui zake au adui yake, adui yo yote yule wa simba, pindi anaposikia ngurumo ya simba, kitu cha kwanza anachoingiwa nacho ni hofu na uoga, haijalishi hata kama mtu huyo yupo kwenye nyumba iliyofungwa milango vizuri, na tena kama mtu huyo ni muoga kupitiliza, basi anaweza kimbia kabisa na kuzitupa hata silaha ambazo alizokuwa nazo. Pia hata na wanyama mfano swala, kwa ngurumo hizo za simba tu wanaweza ingiwa hofu na woga na kila mtu kukimbia njia yake, hivyo kumpa nafasi nzuri ya simba angurumaye kufanikisha lengo lake kiurahisi.

Maana yake ni nini? Kwa kupitia sifa hiyo ya simba angurumaye, tunaweza tambua mbinu moja wapo ya ibilisi anayoitumia pindi anapotaka kummeza mkristo au wakristo, kwamba, huwa anakuja kwa kumpelekea Mkristo au Wakristo vitisho fulani na hofu fulani (ndizo hizo ngurumo), ili kumfanya mkristo husika au wakristo husika kuogopa na kutawanyika huko na huko kama swala kwa vitisho hivyo tu, hivyo kumpa ibilisi nafasi ya kuwashambulia Vizuri baada ya kutawanyika kwa ngurumo zake (vitisho).

Au kumfanya mkristo fulani kuingiwa na hofu (na kutupa silaha), kwa kusahau kabisa nguvu na mamlaka aliyopewa.

Luka 10:19 Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. 

Hivyo basi, tukiijua mbinu hii moja wapo anayoitumia ibilisi dhidi ya watu wa Mungu, basi itakuwa haina madhara kwetu pale tutakapoletewa ngurumo za namna Mbali mbali (vitisho) pale tunapojitwika misalaba yetu na kumfuata Kristo kila siku. 

Hivyo tukeshe, tuombe, tuvae silaha zote za Mungu, ili tuweze kuzishinda ngurumo hizo za Shetani (vitisho), na hila zake.

Waefeso 6:10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 

11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. 

ANGALIZO: Kama upo nje ya Kristo, basi maisha yako yapo hatarini sana, kwani kwa nguvu zako na akili zako huwezi shindana na ibilisi, (haijalishi wewe ni nani), ibilisi hatishwi na cheo chako, wadhifa wako, elimu yako, umaskini wako, ufukara wako, wala uyatima wako, kazi yake ni kuhakikisha unakufa pasipo kuitii injili ya Mungu na kwenda nae kwenye moto wa milele. 

Hivyo yasalimishe maisha yako leo sehemu salama, kwa Yesu Kristo, kwa kutubu dhambi zako zote kwa kudhamiria kuziacha na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi, ambao ni kuzamishwa mwili wako wote na kwa jina la Yesu Kristo sawasawa na maandiko Ili uwe na uhakika huu…

Yohana 6:37 Wote anipao Baba watakuja kwangu; WALA YE YOTE AJAYE KWANGU SITAMTUPA NJE KAMWE

Bwana akubariki, Shalom.

Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

Mkia wa joka kubwa jekundu anaoutumia kuziangusha nyota chini ni nini? (Ufunuo 12:4)


Ni hukumu ipi ya Ibilisi inayozungumziwa katika Waraka wa (1 Timotheo 3:6?)Nini maana ya mstari huu “Mwenye kutawala akisikiliza uongo; Basi watumishi wake wote watakuwa waovu” (Mithali 29:12)


MAKANISA NA MAFUNDISHO YA UONGO YANAYOPOTOSHA WATU WENGI NYAKATI HIZI ZA MWISHO (sehemu ya 08)


Je! Mtu anaweza kuwa na kipawa cha Mungu kabisa na Bado akawa mtumishi wa uongo?

LEAVE A COMMENT