UMEFUNGULIWA KAMA BARABA?

Shalom, karibu tuyatafakari maneno ya uzima ya Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo. 

Maandiko yanasema kuwa, Baraba alikua ni mfungwa mashuhuri sana katika uyahudi 

Matayo 27:16  Basi palikuwa na mfungwa MASHUHURI siku zile, aitwaye Baraba. 

Alifanya fitina yeye pamoja na wenzake, na kibaya zaidi walifanya uuaji hivyo kupelekea kufungwa yeye pamoja na wenzake 

Marko 15:7   Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, amefungwa pamoja na watu waliofanya fitina, na kufanya uuaji katika fitina ile. 

Inawezekana hii ndio ilikua ni tabia yake katika maisha yake kufanya unyanganyi na hata uuaji ilipombidi na hivyo kupelekea kufungwa kifungo cha kimwili yeye na hao wenzake. Lakini tunakuja kuona kuwa, kipindi akiwa katika hicho kifungo, katika siku asiyo dhani anatangaziwa uhuru wake, anaambiwa kuwa sasa wewe si mfungwa tena, na sababu ya yeye kuwa huru ni kuwa Bwana Yesu alitolewa kufa ili yeye apate kuwa huru. 

Hichi kitu kinafunua nini katika roho? Watu wengi leo hii ni kama huyu Baraba, wapo katika vifungo vya kiroho walivyofungwa na ibilisi ama kwa kufahamu au kwa kutokufahamu, kutokana na uzinzi/uasherati, uchawi/ushirikina, uuaji, mikataba na mashetani, kujichua kwa vijana n.k   tena wengine ni mashuhuri katika vifungo vyao zaidi ya hata alivyokuwa Baraba. Ndugu yangu fahamu kuwa Bwana Yesu alishatolewa kwa ajiri yako ili uwe huru katika hivyo vifungo vya kiroho ulivyofungwa na shetani na ndio maana alisema

Luka 4:18   Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma KUWATANGAZIA WAFUNGWA KUFUNGULIWA KWAO, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, 

Hivyo haijalishi kama wewe ni kahaba mashuhuri kiasi gani, haijalishi kama wewe ni mlevi mashuhuri kiasi gani mtaani kwako, haijalishi kama wewe ni mchawai mashuhuri kiasi gani mtaani kwako, haijalishi kama wewe ni mganga wa kienyeji nguli kiasi gani mtaani kwako, fahamu kuwa Bwana Yesu aweza kukupa huru wako kama huyu mfungwa mashuhuri Baraba.

Lakini huyu Mfungwa Baraba alikua na wenzake ila yeye pekee ndiye aliyefunguliwa kufunua kwamba, suala la kufunguliwa (wokovu) ni jambo la mtu mmoja mmoja, hivyo usijipe moyo kusema mbona tupo wengi tunaoabudu sanamu, mbona tupo wengi tunao enda kwa waganga, mbona tupo wengi tunaofanya uasherati, ndugu yangu uhuru uliotangazwa unakuhusu wewe kwanza hivyo tii hiyo nafasi. Kristo ameshatolewa na kufa kwaajiri yako, ameshakutangazia uhuru wako kutoka katika hivyo vifungo vya kiroho, hivyo ni suala la wewe kutoka huko na kuwa huru.

Sasa uhuru wako utaupataje kama Baraba? Uhuru wako utaupata kwanza kwa kumuamini Bwana Yesu kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yako na kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu ( matendo 10:48 ) na kisha kupata nguvu ya Roho mtakatifu ambayo itakuwezesha kuishi maisha ya utakatifu na kuyafanya mapenzi ya Mungu.

Amua leo ndugu yangu kuwa huru kwani wakati bado upo na mlango wa neema wa wewe kuwa huru haujafungwa.

Bwana akubariki. Shalom 


Mada zinginezo:

Waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi. 


VIFUNGO VYA WOTE VIKALEGEZWA.


DAMU YAKE NA IWE JUU YETU.


Ufisadi ni nini katika maandiko?(Waefeso 5:18)


Ni maneno yapi ya unabii yaliyotangulia juu ya Timotheo? (Kulingana na 1 Timotheo 1:18)


AKAJIBU AKASEMA, NAENDA, BWANA; ASIENDE.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *