YOSHUA MWANA WA NUNI.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Tunaposoma habari za Yoshua Mwana wa Nuni, wa kabila la Efraimu, ambaye alikuwa ni mmoja wa wapelelezi kumi na wawili (12) waliotumwa kwa mara ya kwanza kwenda kuipeleleza nchi ya kaanani, kuna jambo kubwa au funzo muhimu sana ambalo sisi kama kanisa la Kristo tunapaswa kulifahamu kutoka kwake kwenye nyakati hizi za mwisho ambazo zimejaa watumishi wengi mno wa uongo (Wachungaji, waalimu, wainjilisti n.k). Kwani, sababu moja wapo ya habari za Shujaa huyo na mtumishi huyo wa Bwana kuandikwa, ni ili na sisi pia tujue wajibu wetu kwa Mungu katika neema ya wokovu aliotupatia bure kabisa.


Tunaposoma maandiko, yanatuambia kwamba, Yoshua Mwana wa Nuni aliyekuwa mtumishi wa Musa tangua ujana wake, alikuwa amejaa roho ya hekima ndani yake (Yaani Roho Mtakatifu), kwa sababu Musa mtumishi wa Mungu alimwekea mikono juu yake.

Kumbukumbu La Torati 34:9 NA YOSHUAMWANA WA NUNIALIKUWA AMEJAA ROHO YA HEKIMAMAANA MUSA ALIKUWA AMEMWEKEA MIKONO YAKE JUU YAKE; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Musa. 

Ingawa Yoshua alikuwa amejaa roho ya hekima ndani yake (Roho Mtakatifu), kwa sababu Musa alimwekea mikono yake juu yake, lakini jambo la kushangaza ni kuwa, bado Bwana hakuishia hapo tu katika kutembea na Yoshua na wala hakumuacha hivyo hivyo, bali aliendelea mbele zaidi na kumwambia hivi.

Yoshua 1:7 Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, UANGALIE KUTENDA SAWASAWA NA SHERIA YOTE ALIYOKUAMURU MUSA MTUMISHI WANGUUSIIACHEKWENDA MKONO WA KUUMEAU WA KUSHOTO, upate kufanikiwa sana kila uendako.

KITABU HIKI CHA TORATI KISIONDOKE KINYWANI MWAKOBALI YATAFAKARI MANENO YAKE MCHANA NA USIKU, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. 

Sasa katika mtazamo wa kawaida tu unaweza jiuliza, mtu kama huyo aliyejaa Roho Mtakatifu ya nini tena kujitaabisha kutii kile ambacho kimeandikwa au kilichoamriwa? Jibu ni kwamba hiyo ndiyo kanuni ya Mungu kutaka utii maagizo yake.

Leo hii Wapo wakristo wengi tu waliopokea karama ya Roho Mtakatifu (kama Yoshua), kwa njia yo yote ile, iwe kwa kuwekewa mikono au vyovyote vile, wananena kwa lugha, wanatabiri, wanasikia sauti ya Mungu, wanafanya miujiza na ishara, wanaponya wagonjwa, n.k, lakini hawataki kutii maagizo ya Mungu, wanataka kufanya wanachotaka, wanataka kuvaa wanavyotaka, wanataka kwenda wanapotaka, wanataka kusikia wanavyovitaka (visivyoumiza hisia zao), Kwa sababu unaona maono Mwanamke basi unataka kuwa askofu au mchungaji (na huku maandiko yamekukataza wewe mwanamke kumtawala mwanamume katika kanisa)


Ndugu mpendwa, habari hiyo ya Yoshua Mwana wa Nuni inatuhusu na sisi pia, wewe kupokea karama ya Roho Mtakatifu sio kwamba ndio basi, Mungu hajaishia hapo tu, bado anakuamuru hivi, “UANGALIE KUTENDA SAWASAWA NA SHERIA YOTE ALIYOKUAMURU MUSA MTUMISHI WANGU” ambaye kwa sasa ni Yesu Kristo, kwani Musa alisema 

Matendo Ya Mitume 3:22 Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi.

23 Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake. 

Na tena bado anakuagiza hivi “KITABU HIKI CHA TORATI KISIONDOKE KINYWANI MWAKOBALI YATAFAKARI MANENO YAKE MCHANA NA USIKU” na kitabu hiko cha torati sio kingine zaidi ya maandiko matakatifu (yaani biblia), agano la kale na agano jipya, kwa sababu agano jipya ni Torati na manabii ambayo iliyohubiriwa kwetu na mitume kama Paulo alivyosema.

Matendo ya Mitume 26:22  Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, WALA SISEMI NENO ILA YALE AMBAYO MANABII NA MUSA WALIYASEMA, kwamba yatakuwa;

Bwana akubariki, Shalom.

Tafadhari washirikishe na wengine habari hii njema.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

KAMA YOSHUA ANGALIWAPA RAHA, ASINGALIINENA SIKU NYINGINE BAADAE. 

YEROBOAMU MWANA WA NEBATI.


FUNZO KATIKA HABARI YA MFALME AHABU NA NABII MIKAYA


NI BWANA GANI HUYO AMBAYE MANABII WALITABIRI KWA JINA LAKE NA KUTESWA KWA AJILI YAKE?


MALEZI YA WATOTO (SEHEMU YA PILI). 

LEAVE A COMMENT