MALEZI YA WATOTO (SEHEMU YA PILI). 

  Uncategorized, Watoto

FUNDISHO MAALUMU KWA MZAZI / MLEZI.

Shalom, jina la Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristo litukuzwe, karibu katika sehemu ya pili ya fundisho maalumu kwa wazazi na walezi ambapo tunajifunza juu ya malezi ya watoto, kama ulipitwa na sehemu ya kwanza ya fundisho hili, basi unaweza tembelea www.Rejeabiblia.com au unaweza tuma ujumbe kwenda mamba  +255652274252 au +255 756 884 547

Katika sehemu ya kwanza tulitazama malezi ya mtoto mwenye umri kuanzia mwaka 0 hadi miaka 03, lakini katika sehemu hii tutaendelea kutazama malezi ya  mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka 03 hadi 10 kwa vipengele vifuatavyo.

  
1. Mchape fimbo

Mtoto anapoanza tu hatua za kukua  huwa anajikuta mchoyo, mwenye hasira, kiburi, mwaribifu na mchafu asiyependa hata kuoga, asiye penda shule, asiye na utulivu katika ibada kanisani au wakati wa maombi, sasa endapo utamwacha pasipo kumfundisha kwa upole, ukali, na fimbo (inapobidi), maana yake ni kuwa, huyo mtoto ataendelea kukua na tabia hizo chafu na kuona kuwa ni kitu cha kawaida tu, kwani hakuna anayemkanya, hivyo, mzazi au mlezi unapoona mtoto ameshaanza tabia hizo unapaswa utumie fimbo kama haelewi kwa njia ya kawaida ili kuuondoa ujinga akilini mwake.

Mithali 23:13 USIMNYIME MTOTO WAKO MAPIGOMAANA UKIMPIGA KWA FIMBO HATAKUFA.

14 UTAMPIGA KWA FIMBONAKUMWOKOA NAFSI YAKE NA KUZIMU.

    
2. Mfundishe mtoto kuomba, kusoma vifungu vya biblia, na kumwimbia Mungu

Miongoni mwa vitu ambavyo ni vya msingi sana kuzingatiwa pia katika suala la malezi ni hapa pia katika maombi, kusoma  vifungu vya biblia, na kumwimbia Mungu. 

Mazazi au mlezi, hakikisha kila siku nyumbani kunakuwa na utaratibu wa ibada ya maombi ya pamoja kama familia  ambapo mnakutana pamoja kuomba, kusoma Neno, kusifu na kuabudu, kwa kufanya hivyo, utamfanya mtoto wako kuwa mtu wa ibada tokea akiwa mdogo kabisa. 

Mfundishe maandiko kwa kumuhadithia matukio yaliyomo ndani ya biblia na hiyo itamsaidia sana kujua maandiko tangia udogo wake kama ilivyokuwa kwa Timotheo 

2 Timotheo 3:14 Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; 

15 NA YA KUWA TANGU UTOTO UMEYAJUA MAANDIKO MATAKATIFU, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. 

    
3. Mvalishe mavazi ya adabu 

Katika ukuaji wa mtoto hapa ni eneo muhimu sana la kuzingatiwa kwasababu katika siku za leo linapuuziwa sana na halichukuliwi umakini. Kama mzazi au mlezi, hakikisha unamvalisha mtoto wako mavazi ya kumsitiri mwili wake na yawe yenye adabu, kama mtoto wako ni wa kike usimvalishe vimini, suruali, na wala usimpake malipstick, wanja, nywele bandia na kope bandia, kumtoboa pua na masikio, kumvalisha hereni au kumpaka rangi vidole vya kucha zake, na wala usimvalishe Mavazi yampasayo mwamume, kwani kwa kufanya hivyo utakuwa wewe mwenyewe mzazi kwa mikoni yako unamfanya mtoto wako awe machukizo kwa Bwana.

Kumbukumbu la Torati 22:5 Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako.

Kama mtoto wako ni wa kiume, vivyo hivyo mvalishe mavazi ya heshima, kataa milegezo kwa mtoto wako, kataa modo na nguo zilizochanika chanika na zenye michoro na maneno ya ajabu ajabu, usimnyoe kiduku kama wahuni na wavuta bangi, usimnyoe kimitindo kwa kuwatazama wasanii fulani ukiisi unamfanya mwanao kuwa wa kisasa, mazazi /mlezi, Mungu anachukia udunia na anataka kila mwanadamu awe Mtakatifu Kama Yeye Alivyo, nje na ndani.

1 Petro 1:15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu KATIKA MWENENDO WENU WOTE

16 kwa maana imeandikwa, MTAKUWA WATAKATIFU KWA KUWA MIMI NI MTAKATIFU

     
 4. Kuwa makini na matumizi ya simu, vipindi vya televisions, na redio.

Mbali na kumwekea umakini katika mavazi yake, pia unapaswa kama mzazi kuchukulia umakini sana katika vipindi vya televisions, redio na matumizi ya simu kwani katika siku hizi za leo shetani anautumia sana mlango huu kufanya uharibifu kwa watu wa lika zote katika jamii, hivyo kama mzazi au mlezi unapaswa kumwekea mipaka mtoto wako katika vitu hivyo, mwepushe na magemu ambayo yana roho za kipepo nyuma yake. Mwepushe na vipindi vya television vilivyojaa maongezi ya uzinzi na uasherati, matusi, ukahaba, ushoga, n.k, kwani usipofanya hivyo mtoto wako ataona vitu kama hivyo sio dhambi na ni kawaida tu, ataona hata kutazama uchi wa Mwanamke na mwanamume sio jambo la kutisha sana, kitu ambacho sio sahihi , hivyo kama mzazi unapaswa kuhakikisha unamlinda mtoto wako katika umri mdogo juu ya hivyo vitu, ili awapo mtu mzima atembee katika njia hiyo Mungu na sio njia ya duniani.

Mithali 22:6 Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.

Shalom.

Tafadhari Shea na Wazazi / Walezi wengine ujumbe huu.


Mada zinginezo:

MALEZI YA WATOTO (SEHEMU YA KWANZA) 


JE! KAMA BWANA YESU NDIYE MUNGU, KULE MLIMANI ALIENDA KUMUOMBA NANI? (Luka 6:12)


BASI ‘BWANA’ NDIYE ROHO.Kwanini Bwana Yesu alijeruhiwa ubavuni pale msalabani?

LEAVE A COMMENT