Elewa Mithali 10:12 Tafsiri yake kuchukiana huondokesha fitina.

Maswali ya Biblia No Comments

Kitabu cha Mithali kimejaa mafundisho mengi ya kutuonya sisi lakini pia kutufundisha kama tukiyasoma na kuyafanyia kazi.

Mstari huu umebeba siri kubwa sana ambayo sisi kama watoto wa Mungu tukiielewa itatusaidia sana katika safari yetu hii ya wokovu hapa duniani mahali palipo na machafuko ya Kila namna.

Mithali 10:12 Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote.

Ukisoma hapo anasema ” kuchukiana huondokesha fitina……” yaani wivu,hasira, uchongezi,usingiziaji,faraka nk maana yake kuchukiana kunatengeneza/kuzaa fitina wala hakuna kitu zaidi ya hapo ambamo ndio uovu wa kila namna uko watu wanapochukiana.

Lakini ukiendelea kusoma anamalizia kwa kusema “…….Bali kupendana husitiri makosa yote.”

Sasa anaposema yote ni kweli kabisa na inawezekana pasipo unafiki wowote kama ilivyokuwa kwa Bwana wetu Yesu Mwokozi wetu ambapo hata hakuwa na chuki hata na wale waliompeleka pale msalabani na kumsulubisha kwa aibu(akiwa uchi kama alivyozaliwa na wakawa wanamdhihaki na kumcheka) lakini hakuwachukia tunaona anawaombea kwa Baba yake awasamehe maana hawajui walitendalo.

Lakini hii inawezekana endapo tu Upendo utatoka kweli kweli ndani ya mtu pasipo kujilazimisha au kuigiza.  Upendo unapofikia katika kilele chake yote yanawezekana. Huo ndio upendo na ndio sifa yake unapojaa kweli kweli unasitiri wingi wa dhambi na si hivyo tu bali pia hauhesabu mabaya. Hii ndio sifa kuu ya upendo na ndio alio nayo Bwana wetu. Si imani,si unabii,uchungaji,uinjilisti unaweza kusitiri wingi wa dhambi ila upendo tu ndio unaoweza wala hakuna kitu kingine.

Neno hili limerudiwa tena katika agano jipya na mitume wa Bwana

1Petro 4:8  Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi

Ukisoma torati yote na manabii, agano jipya pia kiini chake ni upendo. Na ndio maana Bwana Yesu anasema

Luka 6:31“Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo. ”

Ukitaka kushinda wivu,hasira,usengeny’enjaji,wizi,utukanaji watendee watu kama jinsi nafsi yako unavyotaka kutendewa, utaanza kuona kimoja baada ya kingine vinaondoka ndani yako. Kwa sababu umejua kuwa kumbe mwenzako pia ni kama wewe vile usivyopenda kuibiwa,kutukanwa,kudharauliwa, hivyo hivyo naye hapendi.

Jinsi unavyopenda kufanikiwa vivyo hivyo usichukie unapoona mwenzako anafanikiwa na ukaanza kumfanyia fitina usifanye hivyo mpende.

Ziko kanuni/njia tatu za kufuata ili jambo hili liweze kutokea ndani yetu.
Njia ya kwanza ni kujazwa Roho Mtakatifu,  kama maandiko yanavyosema tunda la Roho ni Upendo (Wagalatia 5:2).  Hivyo unapojijengea tabia ya kuwa muombaji sana, si kidogo Bali sana si chini ya masaa kadhaa
Roho Mtakatifu unampa nafasi ya kujaa ndani yako zaidi.
Hivyo inakuwa kwako ni rahisi kuona upendo unatoka ndani yako wala hutaulazimisha kutoka.

Njia ya pili ni kuwa msomaji wa Neno, maombi bila Neno ni sawa na gari lenye mafuta lisilokuwa na mwelekeo na zaidi sana maombi yatakuwa ni mazito kwako. Unapokuwa msomaji wa Neno kila siku unampa nafasi Roho Mtakatifu ya kutufundisha na kukujenga kupitia Neno maana Neno la Mungu ni hai (Waebrania 4:12). Hivyo unavyokuwa msomaji sana Neno la Kristo linajaa ndani yako hata unapopatwa na hasira Neno linakurejeza lililoko ndani yako kwa haraka unarudi katika mwelekeo ulio sahihi na unakuwa ni mwepesi wa kuachilia.

Jambo la tatu na la Mwisho ni kukitendea kazi kile unachokisoma na kufundishwa na Roho Mtakatifu. Unaanza hatua ya kushindana na kupingana na vipimgamizi vyote vinavyokuja mbele yako usiruhusu chochote kibaya kikutawale. Hivyo kuwa muombaji,kusoma Neno peke yake pasipo kutendea kazi inakuwa ni sawa na gali lililo jazwa mafuta lakini halina pa kwenda lipo tu, maana yake itakuwa ni uharibifu wa fedha hivyo ili hayo yote yatendeke ndani yetu tunatakiwa kuwa na nguzo hizi kuu Tatu muhimu na kila kitu kitawezekana maana tunae Roho Mtakatifu anatuwezesha mahali tunaposhindwa.

Hivyo kama wana wa Mungu hatuna budi kila siku kujitwika msalaba wetu bila kuchoka wala kukata tamaa ili tuufikie ule Upendo wa Ki-Mungu ndani yetu kama maandiko yanavyosema katika (2 Petro 1:5-11).

Ubarikiwe sana!.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *