HAPANA HATA MMOJA ALIYETHUBUTU KUAMBATANA NAO; ILA WATU WALIWAADHIMISHA

  Maswali ya Biblia

Je Biblia ina maananisha nini kusema maneno haya kwa habari ya mitume? Matendo 5:13 “hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha;

”JIBU: Tusome mstari huo;

Matendo ya Mitume 5:12-16

[12]Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani;

[13]na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha;[14]walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake;

[15]hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao.

[16]Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu. wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.

Ijapo kuwa Mungu alionyesha uweza wake mwingi , maajabu pamoja na ishara mbalimbali kwa mitume wake, lakini kulikuwa namna ya maisha na mwenendo ambao haukuwa rahisi kwa watu wengine kupenda kuufuata pamoja na mitume.
Ndio maana maandiko yanasema hapo “hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao, ljapokuwa walikuwa wanawaadhimisha, yaani wanajivunia wao kama maaskari wema na waaminifu wa Bwana Yesu Kutokana na utumishi wao na namna walivyomtumikia Mungu kwa moyo wa umoja kwa pamoja.

Na namna pekee ya mwenendo ambao uliwafanya watu wasiweze kuambatana nao, ndio huo wa kutokuogopa vifo, mapigo, mabaraza ya makuhani, mashutumu, na sura za watu. Yaani walikuwa tayari kumtumikia Mungu kwa hali yeyote ile, bila kujali mazingira yanayowazunguka yanataka nini. Ikumbukwe kuwa mitume walipoitwa kumtumikia Mungu hawakutumwa kwanza kuitangaza injili katika nchi za mbali, bali waliagizwa waanzie kwanza pale pale Yerusalemu ambapo palikuwa na ukinzani mkubwa sana kutoka kwa wafalme na viongozi wa kidini, na kitu cha hatari zaidi mitume walikuwa wanaongozwa kwenda kuhutubu katika hekalu ambalo, Bwana wetu Yesu Kristo alipindua meza zao, baada ya kuona nyumba yake ya ibada imegeuzwa na kuwa ya wanyanganyi Hivyo hata na baada ya muda kidogo kupita Petro na Yohana walipofungwa, kwasababu ya kuhutubia watu, mule hekaluni..utaona malaika aliwatoa na kuwaaagiza warudi kule kule hekaluni kuhutubu.

Matendo ya Mitume 5:18-21
[18]wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza;[19]lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema,

[20]Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu.

[21]Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha.Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete
Unaona, Hata wakati kanisa linapitia dhiki Yerusalemu, na kuwafanya watakatifu wote watawanyike, ni mitume peke yao waliendelea kubaki Yerusalemu.

Matendo ya Mitume 8:1
[1]Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume.

Hivyo kwa kumtumikia Mungu kwa namna hiyo na kupelekea hata kuhatarisha maisha ya mitume, haikuwa swala jepesi kwa akili na kwa namna ya kibinadamu hivyo watu wengi, kuufuatana kwamba walikuwa wapo pamoja nao, wakifurahia ushujaa wao katika utumishi wao wakitamani pia waendelee kumtumikia Mungu kwa ujasiri huo ili injili iweze kuenea mahali pote.

Utumishi kama huu tunaushuhudia pia katika huduma ya Bwana Yesu , hatavl Biblia inasema wengi wa wakuu wa kidini walisadiki maneno aliyohubiri lakini hawakuweza kumkiri na kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Hii ni kutokana na hofu ya kutengwa na watu.

Tusome pia maandiko ;

Yohana 12:42

[42]Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.

Watu wengi hawakuweza kuambata na Yesu katika mapito yake lakini aliaminiwa na wengi.Watu wengi hawakuweza kuambata na Yesu katika mapito yake lakini aliaminiwa na wengi.
Hii ni kufunua nini kwa watumishi wa Mungu? Ikiwa umeitwa / umechaguliwa na Mungu kama mtumishi wake.
Ni lazima na ni muhimu sana maisha yako yajikite katika utumishi wa Mungu kwelikweli, yaani viwango vyako vya kujikana nafsi lazima viwe juu zaidi ya watu wengine..Ndivyo ambavyo Mungu atakavyokutumia na ndivyo watu watakavyokuadhimisha kama ilivyokuwa kwa mitume.Chachu yetu ni lazima izidi ya watu wengine. Bwana Yesu atusaidie sana kwa hili ilituwe watumishi wake kwelikweli

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

LEAVE A COMMENT