Bwana Yesu asifiwe. Karibu tujifunze Maneno ya Uzima!..
Swali: Yesu alikuwa na maana Gani kumwambia yule mwanamke chakula Cha watoto hawapewi Mbwa?
Jibu: Habari hiyo inayopatikana katika injili yaani mathayo 15:21, Marko7:24-30 unaweza kupitia sehemu zote kwa uchambuzi sahihi zaidi, ni habari inayohitaji umakini mkubwa katika kujifunza.
Karibu tutafakari kwa pamoja mazungumzo haya..
Mathayo 15: 21 “Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni.
22 Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.
23 Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.
24 Akajibu, akasema, SIKUTUMWA ila kwa KONDOO WALIOPOTEA WA NYUMBA YA ISRAELI.
25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.
26 Akajibu, akasema, SI VEMA KUKITWAA CHAKULA CHA WATOTO [ISRAEL]na KUWATUPIA MBWA [MATAIFA].
27 Akasema, NDIYO, BWANA, LAKINI HATA MBWA HULA MAKOMBO YAANGUKAYO MEZANI PA BWANA ZAO.
28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile”.
Kwanza kabisa kipaumbele cha huduma ya Yesu duniani ilikuwa ni kwa taifa la Mungu Israeli, ambalo walikuwa wakimtumainia kama Ahadi tangu enzi za Baba zao[Ibrahimu, isaka na Yakobo], ambapo Ujio wa Kristo ulikuwa ni utimilifu wa ahadi ya Mungu kwa Israeli. Lakini ni tofauti kidogo kwa Mataifa ambao walikuwa mbali na Mungu,walifanya ibada za sanamu na upagani kwa ujumla, mara nyingi utaona wakifananishwa na unajisi au Mbwa , mbwa-mwitu n.k(wafilipi 3:2, mathayo 7:6, matendo 20:29, Luka 10:3, Mithali 26:11 n.k).
Katika Mfano huu ukiangalia katika lugha halisi ya agano jipya yaani kigiriki, Bwana Yesu anatumia neno ‘kunarion’ Ambayo ni mbwa anayefugwa nyumbani, badala ya ‘kuon’ ambae ni mbwa mwitu au asiye na makazi maalum. Mwanamke yule ambaye SI myahudi, anaonekana kuelewa vyema kuwa Bwana alimaanisha Nini, ndio maana alimjibu bila shaka na kwa upole kabisa..
Mathayo 15:27″ Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.”
Unaona, mwanamke alimuelewa kuwa bwana aliongea kwa maana nzuri, na Yesu anamjibu kwa furaha baada ya kugundua mwanamke yule ameelewa Mithali yake..
Mathayo 15:28 “Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.”
Hivyo inaonesha jinsi neema ya Mungu ilivyokuja kwetu Mataifa tuliokubali na kumwamini Yesu kama masihi au mwana-kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya Ulimwengu(watu wote), (Yohana 1:29) ambaye kwa kumwagika damu yake msalabani tumehesabiwa haki Bure kwa kumwamini yeye kama Mwokozi/Bwana na si Tena kwa matendo ya Sheria(Warumi 3:27, 28,Galatia 2:16, Galatia 3:2,2petro 2:8) kama wokovu wa Zamani kabla ya upendo wa Mungu kufunuliwa katika Mwana.
Mtume Paulo anaandika kwa Waefeso..
Waefeso 3: 4 “Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.
5 Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;
6 ya kwamba MATAIFA NI WARITHI PAMOJA NASI WA URITHI MMOJA, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili;”
Tunajifunza Nini kwa Mwanamke mkananayo?
Tunajifunza kuomba kwa bidii. Hata kama tunajiona kuwa si watu wanaostahili kupata majibu, au tumeomba kwa muda mrefu bila majibu mazuri TUSIKATE TAMAA! Tujifunze kwa Mwanamke huyu ambaye Yesu alikuwa na uwezo wa kumponya lakini alitamani kusikia au kutambua Imani yake kwanza.
Kuomba kwa Bidii tunapata hata katika Mfano wa kadhi dhalimu na mwanamke mjane, ambapo alipata majibu yake kutokana na bidii yake, kwa undani zaidi wa habari hii soma (Luka 18:1-8). Mungu ni mwema na mkarimu kwa watu wote, tumwombe bila kukata tamaa pasipo na mashaka, Pia anapendezwa tukiomba kwa Imani.(Yakobo 1:1-8)
Umebarikiwa sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.