Nini maana ya neno kijicho kibiblia?

Maswali ya Biblia No Comments

Kwa jamii nyingi za watu wa zamani walikuwa na imani kuwa mtu akikutazama au kukuangalia kwa macho yake basi inaweza kukuletea madhara au laana juu yako, ikiwa amekusudia au hajakusudia kufanya hivyo,

Imani hii hata kwa wakati huu ipo kwa jamii na watu wengi,wakiendelea kuamini kwamba kupitia jicho la mtu anaweza kukuloga, au kupitia jicho la mtu linaweza kukuletea mikosi na magonjwa,kwa kufahamu hivyo mtu anajiwekea ulinzi kwa kuvaa hirizi au kufanya matambiko..

Je Marko 7:22, Bwana Yesu alimaanisha nini?

Marko 7:21-23

[21]Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati,

[22]wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.

[23]Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi..

Bwana Yesu hakumaanisha hivyo kama wengi wanavyoamini, bali alimaanisha JICHO OVU, jicho la ubaya, jicho la husuda,jicho la uchoyo…

Alisema hapa..

Mathayo 20:15 “Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema”?

Kauli hiyo aliitoa pale alipotoa mfano wa Yule mtu aliyewaajiri wafanyakazi Katika shamba lake, na mwisho wa kazi akawalipa kila mmoja sawa sawa bila kujali huyu alifanya kazi sana au huyu alifanya kidogo,iwe huyu alichelewa au aliwahi, na sisi tunaweza kuwa na jicho ovu kwa mwingine kupewa upendeleo sawa na wetu..

Katika kampuni yupo mfanyakazi mpya amekuja na analipwa mshahara mkubwa tofauti na wewe uliyekaa miaka mingi kwenye ofisi hiyo,ikiwa jambo hilo utalionea wivu ndani yako na kutaka apewe mshahara mdogo, sasa hapo hicho ndicho kijicho ambacho Bwana Yesu anakizungumzia kinachomfanya mtu hata ajichafue kwa kujitia unajisi…

Pengine maandiko yanasema…

Kumbukumbu 15:9 “Jitunze, msiwe na neno lisilofaa moyoni mwako, kusema, Umekaribia mwaka wa saba, mwaka wa maachilio; JICHO LAKO LIKAWA OVU juu ya nduguyo usimpe kitu; naye akamlilia Bwana juu yako, ikawa ni dhambi kwako”.

Aina nyingine umeiona hapo, kumbe hata kumdhulumu mwingine haki yake ili aendelee kukutumikia au hata kwa wivu asipate kuendelea ili aweze kujitegemea kwa kudhamiria kumdhulumu haki yake kwa utumishi kwako, inawezakuwa ni mdada wa kazi (house girl) au house boy, unamnyima au kumdhulumu malipo yake, hicho ni kijicho ambacho mwisho wa siku kitakufanya hata wewe mwenyewe usikubaliwe na Mungu na kukutia unajisi..

Bwana Yesu anasema..

Mathayo 6:22 “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru”.

Hivyo kwa pamoja hatuna budi kuondoa kijicho ndani yetu, na hii inatokana na kuushinda wivu, ukifanikiwa kuushinda wivu hautaona uchungu wowote ndani yako pale mwingine anapofanikiwa, hutakuwa na sababu za kumdhulumu mfanyakazi wako, wala kuunda kisasi kwa majirani zako, bali kijicho kitaanza kufa ndani yako..

Bwana Yesu atusaidie kushinda kijicho ili tupate kibali mbele zake na kuyatendea kazi hayo yote,ili nafsi zetu zizidi kuwa safi pasipo kunajisika..

Shalom..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *