SWALI: Naomba kufahamishwa maana ya huu mstari?
Mithali 19: 4 “Utajiri huongeza rafiki wengi; Bali maskini hutengwa na rafiki yake”
JIBU: Katika mstari huu mwandishi(Sulemani), halengi kwamba tuwe matajiri ili tuongeze marafiki wengi.. Hapana bali alikuwa anaeleza uhalisia ulivyo katika huu ulimwengu wa dhambi.
Kwamba mali ndio imekuwa kiunganishi cha watu, tabia ambayo Kristo hana. pale mtu anapokuwa na mali nyingi, watu ndio watamsogolea na kumpenda na kumthamini zaidi, lakini huyo huyo akipungukiwa nazo kidogo hukimbiwa.
Mwigizaji mmoja maarufu wa Marekani, alisema siku alipochaguliwa kuwa Gavana wa jimbo la Kalifonia, alishangaa kuona watu wengi wakimkaribia na kumnyenyekea, na hata wakimwalika kushiriki naye kifungua kinywa kila asubuhi, lakini alipostaafu kazi ile, wale watu waliokuwa wakimfanya kama mfalme, wengi wao walitoweka, na cha ajabu hata alipopishana nao barabarani walijifanya kama hawamjui.
Biblia ilitabiri kuwa katika sikuhizi za mwisho, tabia hiyo itazidi ndani ya watu;
2 Timotheo 3:1 “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.
2 Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, WENYE KUPENDA FEDHA, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi”
Na Mungu akatutahadharisha sisi watakatifu wote tusiwe na tabia hiyo(Waebrania 13:5), akasema pia na kwa maaskofu na mashemasi na wazee wa kanisa wajiepushe nayo(1Timotheo 3:1-8, 1Petro 5:1-2)..Kwasababu tukiwa na tabia ya kupenda fedha tutajenga ubaguzi, vilevile upendeleo. Kama mtume Yakobo alivyoandika katika;
Yakobo 2:1 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.
2 Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu;
3 nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu,
4 je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? 5 Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? 6 Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu”?
Bwana atupe tabia kama yake, ya urafiki, kwa kipimo cha haki, na sio kwa kipimo cha mali.
Shalom.