AZAZELI NI NANI?

Maswali ya Biblia No Comments

Huyu Azazeli ni Nani tunayemsoma katika walawi 16:8?

Mambo ya Walawi 16:8
[8]Na Haruni atapiga kura juu ya wale mbuzi wawili; kura moja kwa ajili ya BWANA; na kura ya pili kwa ajili ya Azazeli.

Tukiangalia Kwa ufupi habari hii, katika Mambo ya walawi Sura ya 16, tunaona kwamba katika siku ya upatanisho wa Wana wa Israeli, ambayo ilifanyika mara moja tu Kwa mwaka siku ya 10 ya mwezi wa 7 wa kalenda ya kiyahudi. Ambapo katika siku hiyo Wana wa Israeli walitakaswa dhambi zao zote, kuanzia kuhani mkuu na kufuatiwa na waisraeli wote.

Sasa Kwa jinsi upatanisho huu ulivyofanywa, kuhani mkuu ilimpasa Kwanza kujipatanisha yeye mwenyewe na Bwana pamoja na watu wa nyumbani kwake, Kwa kumtolea( kumchinjia) Bwana ng’ombe wake( ndama mume) kwaajili ya dhambi zao. Na akiisha kuwa safi, kumchinjia Bwana mbuzi mmoja Kwa ajili ya dhambi za watu wote.

Sasa ipo namna mbuzi huyu alivyopatika.
Kuhani mkuu aliletewa mbuzi wawili waume toka Kwa waisraeli.
Akawachukua mbele ya mlango wa hema ya kukutania apate kuwapigia Kura mbele za watu. Kwahiyo alitwaa mfano wa mawe wawili yafananayo ila yenye maneno tofauti moja “Kwa Bwana/wa kufa” na lingine ” Kwa Azazeli/ wa Kuishi”

Na mbuzi hawa walichukuliwa wanaofanana kimuonekano ili isiwe rahisi kuwatofautisha.

Mbuzi aliyeangukia Kwa Bwana alichinjwa sadaka ya dhambi na aliyeangukiwa na kura ya Azazeli aliachiwa huru mbali na watu ( jangwani) baada ya kuhani kuungama dhambi za watu juu yake au kumtwika lawama za mkutano mzima.

Zingatia sana hapa: dhambi zimeshalipiwa na mbuzi wa Kwanza aliyechinjwa sadaka ya dhambi, na huyu mbuzi wa pili anaachiwa huru huku kabebeshwa mzigo wa dhambi ambazo zimekwisha samehewa Kwa kifo cha mbuzi wa kwanza.

Kwahyo mbuzi huyu wa Azazeli alibeba ujumbe kuwa, shetani Hana nguvu tena juu ya Wana wa Israeli na dhambi zao Kwa maana, zilishasamehewa/ kulipiwa. Kwamba shetani huwezi kuwashutumu mbele ya Mungu kwavile dhambi zao zimeshalipiwa.

Sasa changamoto kubwa inakuja katika kutafsiri Neno azazeli, maana waalimu wa zamani hizi wanalichukulia Kama Jina, tena la Pepo mchafu aishiye jangwani. Lakini azazeli Kwa asili ni Neno la kiebrania lililounganisha maneno mawili mbuzi +huru yaani mbuzi wa kuachiwa huru.
Hivyo hapo Bwana hakugawana mbuzi na shetani, wote ni wa Bwana.

Na Neno hili Azazel Kwa kiingereza linatafsiriwa Kama mtu anayetupiwa lawama hata kama yeye Hana kosa( scapegoat)

Jambo hili ni fumbo kubwa sana ambalo Tunaliona tena katika agano jipya.

Ni katika kifo cha Bwana Yesu, ambacho tunakisoma katika mathayo 27
Pilato alipowawekea wayahudi wachague ni Nani aachiwe huru Kama ilivyo desturi yake ya kuwaachia mfungwa mmoja kila pasaka.
Lakini tunaona makuhani wakuu waliwashawishi watu waombe afunguliwe muhalifu Baraba na Bwana Yesu auawe.

Yaani makuhani waliwekewa watu wawili (sio mbuzi tena) Kati ya Baraba na Bwana Yesu.

Wakachagua Bwana Yesu atolewe sadaka ya dhambi na muhalifu Baraba aachiwe huru kabisa pasipo ya kulipia makosa yake.

Baraba anamuwakilisha Nani?
Anatuwakilisha Mimi na wewe, watu ambao tulikua na dhambi au pengine bado tupo dhambini (Kwa wasiompokea Kristo bado). Lakini Kristo ambaye hakuwa na kosa lolote akatufia ili Sisi tusihesabiwe dhambi wala kupokea adhabu yoyote, tuwekwe huru kwelikweli.

Ni vema sana tukifahamu kuwa, hii mizigo ya dhambi tunayoibeba, ilishalipiwa na kwamba shetani Hana uwezo wa kutushitaki, tupo huru.

Lakini ni sharti kwetu kuukubalii na kuupokea wokovu huo, Kwa kumkiri Kristo kuwa ni mwokozi wetu, ili Yeye mwenyewe aibebe mizigo ya dhambi zetu, na hata shetani akitaka kutushutumu makosa, Kristo ndani yetu asimame kututetea kwamba alitufia ili tusihesabiwe dhambi.

Shalom

Kwa Maombezi/Ushauri/Maswali/Ratiba za Ibada Wasiliana nasi Kwa namba hizi
+225789001312/ +225693036618.

Pia unaweza kujiunga na channel yetu ya mfundisho ya NURU YA UPENDO” Kwa kubofya hapa>> WhatsApp: https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10<< 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *