Fahamu maana ya nguo za magunia katika maandiko.

Maswali ya Biblia No Comments

Shalom!, Nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Nguo za magunia katika maandiko ni nguo zilizotengenezwa kwa manyoya ya mbuzi. Ambazo zilikuwa zikitumika kuwakilisha jambo fulani katika agano la Kale.

Ni tafauti na inavyoweza kudhaniwa labda ni mifuko hii ya salfeti. Inayotumika kuhifadhia nafaka kama maharage,mahindi nk sivyo.

Sasa zilikuwa zinavaliwa kuashiria jambo fulani hazikuwa ni za kuvaa vaa tu kama fasheni. Bali zilitengenezwa mahususi kwa ajili ya MAOMBOLEZO na TOBA.

1. Maombolezo.
Israeli walipopelekwa utumwani kule Babeli maandiko yanasema iliwapasa wavae nguo za magunia kwa ajili ya kuomboleza juu ya kile kilichowapata maana Mungu aliwaonya sana lakini hawakutaka kusikia.

Yeremia 4: 8 “Kwa sababu hiyo jifungeni NGUO ZA MAGUNIA; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya Bwana haikugeuka na kutuacha”

Lakini ukiendelea kusoma Biblia inaendelea kusema…

Yeremia 6:26 “Ee binti wa watu wangu, ujivike NGUO YA MAGUNIA, na kugaagaa katika majivu; fanya maombolezo, kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, maombolezo ya uchungu mwingi; maana mwenye kuteka nyara atakuja juu yetu ghafula”.

Hata watu wa Ninawi baada ya kuhubiliwa injili na Yona nao vivyo hivyo walivaa nguo za magunia wakiomboleza na kujuta kwa yale walioyafanya.

Ukisoma pia Rispa nae alivaa nguo za magunia akiomboleza kwa kufiwa na wanawe.

2Wafalme 21:10 “Naye Rispa, binti Aya, akatwaa nguo ya magunia akajitandikia mwambani, tangu mwanzo wa mavuno hata waliponyeshewa mvua toka mbinguni; wala hakuacha ndege wa angani kukaa juu yao mchana, wala wanyama wa mwitu usiku”

Hivyo magunia zilikuwa si nguo za kuvaa wakati wa furaha bali wa huzuni na machozi wakati mwingine.

2. Toba.

Watu  wa agano la Kale pia walipokuwa wakitaka kusogea mbele za Bwana walikuwa wakivaa nguo za magunia kuomba toba mbele za Bwana kuonesha wao si kitu mbele za Bwana. Huku wakitaka rehema.
Moja wapo ni wale watu wa Ninawi nilivyosema hapo mwanzo.

Yona 3: 5 “Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, WAKAJIVIKA NGUO ZA MAGUNIA, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo.

6 Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, AKAVUA VAZI LAKE, AKAJIVIKA NGUO ZA MAGUNIA, na kuketi katika majivu”

Lakini pia Danieli alipokuwa akisogea mbele za Bwana kuwaombea ndugu zake Toba mbele za Bwana alivaa nguo za magunia kuonyensha unyeyekevu mbele za Bwana.

Danieli 9:3 “Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na KUVAA NGUO ZA MAGUNIA na majivu.

4 Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake”

Je?, na sisi katika agano jipya tunapopita katika shida kama misiba,au kuomba rehema mbele za Bwana na sisi inatupasa kuvaa nguo za magunia?.

Jibu ni la!, hakuna mahali biblia imetuagiza na pia si kosa kama mtu akiamua kuvaa ama kutokuvaa ni uchaguzi  wake yeye mwenyewe wala hatapungukiwa na kitu wala haitakuongezea kitu rohoni.

Yoeli 2:12 “Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea;

13 RARUENI MIOYO YENU, WALA SI MAVAZI YENU, MKAMRUDIE BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya”

Unaona hapo!, anasema “rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu,mkamrudie Bwana….”

Sasa mavazi yaliyokuwa yakizungumziaa hapo ni yale ya magunia na si mengineyo. Toba yetu na maombolezo yetu halisi yako rohoni/ mioyoni mwetu.

Je!, umemwamini Yesu? Unateswa na dhambi na uchawi na ushirikina, njia ni moja tu ya kuepukana na hayo na wewe kuwa salama nayo ni wewe kurarua moyo wako kwa Bwana yaani mrudie Bwana. Leo hii wala hujachelewa!!

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *