HATARI YA KUSIKIA NENO NA KUTOKULIFANYIA KAZI.

  Biblia kwa kina

Shalom nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Iko hatari kubwa sana kwa watoto wa Mungu tunapolisikia Neno na tukashindwa kulifanyia kazi na tukalipuuzia tu ama tukatamani kuliishi lakini tusichukue hataua zozote.

Yakobo 1:22-25″Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.23 Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.25 Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.”

Leo hii kila siku watu wengi wanakwenda kanisani tena wanabidii kila jumatano, ijumaa na jumapili, wanakwenda wanasikiliza Neno linawagusa kweli na wanasema “kuanzia leo nimebadilika nitatembea katika njia anayoitaka mwokozi wangu” lakini baada ya kutoka tu ibadani wanarudi kuwa wale wale hawatendei kazi kile walichokisikia lakini si hivyo tu pia wanasahau  hata walisema nini muda kidogo uliopita hii ni hatari kubwa sana.

Leo hii kumekuwa na kundi kubwa sana la wakristo ambao wanavijua vifungu vya Biblia, wanajua kuvichambua kwa namna mbali mbali lakini hawayafanyi yale ambayo Mungu anawaagiza kuyafanya kama walivyokuwa Mafarisayo, makuhani na wandishi ambao walikuwa ni wepesi wa kuwahukumu watu wengine wanapokosea kupitia sheria ile iliyokuja kwa mkono wa Musa wakati nao walikuwa hawaishiki Sheria.

Luka 6:47”  Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo?”

sasa tutakwenda kutazama kwa undani hatari kubwa iliyopo pale tunaposikia Neno na tukabaki vile vile bila kulifanyia kazi.

Luka 6:47 “Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake.”

Ukisoma kwa makini hapo kuna jambo utaliona hebu tutazame hii sentensi kwa makini zaidi. Anaanza kwa kusema “KILA MTU AJAYE KWANGU..”  maana yake kila alieokolewa maana hakuna mtu awezae kwenda kwa Yesu pasipo kuvutwa na Mungu (Yohana 6:44). Sasa huyo mtu anapokwenda anakwenda kufanya nini? Anaendelea kusema “NA KUYASIKIA MANENO YANGU” kumbe mtu anaekwenda anakwenda kuyasikia maneno ya uzima kila  mmoja mmoja wetu anakwenda kusikia Neno lakini je ni kusikia tu?? Jibu ni LA! Anaendelea kusema “ NA KUYATENDA” kumbe sio kwenda na kusikia tu nakuondoka kwenda nyumbani na kuendelea na mambo mengine kumbe ni kuyatendea kazi pia yale tuliyoyasikia!.

MTU ANAYEENDA, NA KUSIKIA NA KUTENDA ANAFANANISHWA NA NINI?

Mtu huyu anafananishwa na mtu aliechimba msingi wa nyumba akauchimba ukafika chini sana na kisha ile nyumba akaijenga au kuishikamanisha na ule msingi na nyumba, na gharika na kila aina ya dhoruba vilipokuja kuipiga ile nyumba ili ianguke wala haikuanguka ikabaki kuwa salama.

Luka 6:48 “ Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri’

Maana yake ni nini? Kumbe tunapolitenda(kulileta katika maisha yetu) Neno lile linafanyika kuwa msingi kwetu na kadili tunavyozidi kulifanyia kazi kwa bidii bila kulipuuzia ndio msingi unavyozidi kuimarika zaidi unazidi kwenda chini zaidi, HALELUYA!

Ndipo hapo ibilisi anataleta machafuko ya kila namna ili kutuangusha dhoruba nyingi ibilisi ataziachilia wala hatutaanguka kwa sababu Msingi(NENO) umeenda chini sana(Wakolosai 3:16) kiasi cha kutokutikiswa na jambo lolote wala kuchukuliwa na Mafundisho ya uongo, nk kama vile Ayubu alivyosimama na Bwana hata asianguke katika mambo yote yale yaliyompata kwa sababu kila siku alikuwa ni mtu wa kujiibidiisha kwa Bwana ndio maana akweza kustahimili Mungu ameruhusu tumsome hata leo. “JE! unajiibidiiisha kwa Bwana au mpaka usimamiwe na mchungaji wako?”.

Maana Neno la Mungu ni hai (Waebrania 4:12) ni tofauti na maneno mengine hivyo tunavyolifanyia kazi ndivyo linazidi kutupa uhai zaidi ndani yetu na nguvu ya kuendelea kusimama katika hali yoyote ile na kushinda.

MTU ANAYEENDA, NA KUSIKIA LAKINI HATENDI  HATARI YAKE NI IPI?

Mtu wa namna hii anafananishwa na mtu aliejenga nyumba juu ya ardhi pasipo msingi nyumba hio itadumu kwa kitambo kidogo sana zikivuma pepo kwa nguvu na mvua na mafuriko yakaja haitaweza kustahimili. Ni lazima itaanguka tu. Na si kuanguka tu bali kusambalatika kabisa.

Luka 6:49  “Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa”

Unaona hapo! “MTO UKAISHUKIA KWA NGUVU” shetani kamwe haji nusunusu kukuangusha anakuja na silaha zote na kila aina ya mbinu ili kukuangusha ndugu kama msingi wako haujenda chini sana nakuhakikishia utaanguka tu. Penda kufanyia kazi Neno unapolisikia. Na ndio maana unajikuta unarudi kwenye uzinzi tena, tamaa, unaanza kuipenda dunia na kuizoelea,umeanza kudanganya na kujichua kwa siri siri huku unasema unampenda Yesu ndugu shetani atakupepeta jinsi apendavyo kama hutaamua kuchukua hatua ya kujikana.

paia anasema “MAANGAMIZI YAKE NYUMBA ILE YAKAWA MAKUBWA!” ndugu utaangamia vibaya mno usipoamua kuchukua hatua leo hii nakuombea kwa jina la Yesu unaposoma ujumbe huu ubadilike sasa uanze kupiga hatua.

Kumbuka hizi ni siku za Mwisho unyakuo ni siku yoyote hebu fikilia Kristo anakuja leo anakukuta katika hali hiyo uliyonayo, umefollow account za watu wa kidunia, umeokoka miziki ya kidunia inayohamasisha uzinzi tu imejaa kwenye simu yako, nk, utapona? Utaondoka nae? Acha kujitumainisha wakati huu ni wa kudhamilia kweli kweli kuuacha ulimwengu kubali kuonekana ni mshamba waachie wenye dunia yao wewe una ulimwengu mpya wa milele acha haya yapite jitaabishe kwa huu muda mchache uliosalia.

Ubarikiwe sana

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

LEAVE A COMMENT