Je! Hazina za gizani ni zipi?

Isaya 45:3 “nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli”.

Hazina za giza ni baraka zilizoshikiliwa na adui shetani, ambazo zinapaswa kuwa zetu.Mfano wa hazina za gizani ni zile wana wa Israeli walizozipata kutoka katika jeshi la Washami.

Wakati ule ambao Israeli walikuwa wana njaa kali, hata kufikia hatua watu kula mavi ya njiwa, na kichwa cha punda…na wakati huo huo mji wote ulikuwa umezungukwa na jeshi la Washami pande zote. Mungu akayasikilizisha majeshi ya washami mishindo ya farasi, na kwa hofu kubwa wakaacha vyakula vyao vyote na kukimbia kutoka katika zile kambi zao walizokuwepo, na wana wa Israeli wakaenda kuzitwaa zile Nyara na vile vyakula.. Hivyo wakawa wamepewa na Bwana hazina zilizikuwepo gizani.

2 Wafalme 7:5

 “Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu.

6 Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi.

7 Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao.

8 Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha.

9 Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme.

10 Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha.

11 Na mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme.

12 Mfalme akaondoka usiku, akawaambia watumishi wake, Sasa nitawaonyesha ninyi walivyotutendea Washami. Wanajua ya kuwa tuna njaa; basi wametoka kituoni, ili kujificha kondeni, wakisema Watakapotoka mjini, tutawakamata hai; tena tutapata kuingia mjini.

13 Na mmojawapo wa watumishi wake akajibu, akasema, Kunradhi; baadhi ya watu na watwae farasi watano katika hao waliosalia, waliobaki ndani ya mji (tazama wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli waliobaki ndani yake; tazama, wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli walioangamia), tukawapeleke tukaone.

14 Basi wakatwaa magari mawili na farasi zake; mfalme akawatuma kuwafuata Washami, akasema, Enendeni, mkaangalie.

15 Wakawafuata mpaka Yordani; na kumbe! Njia yote ilikuwa imejaa mavazi na vyombo, walivyovitupa Washami, wapate kukimbia upesi. Watu wale waliotumwa wakarudi, wakamwambia mfalme.

16 Basi watu wakatoka, wakaziteka nyara hema za Washami. Ikawa kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, sawasawa na neno la BWANA”.

Andiko hilo linaonyesha dhana ya hazina zilizoshikiliwa na adui, ambazo baadaye zilichukuliwa na kupewa watu wa Mungu.

Hazina nyingi, bado zipo, watu na vitu vingi vimetekwa na adui, Imani inaweza kusaidia kukamata hazina hizi.                                                                                                                 

Maandiko yanasema..

2 Wakorintho 10:4 “maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)

5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; NA TUKITEKA NYARA KILA FIKRA IPATE KUMTII KRISTO”.

Andiko hilo linaeleza kwamba kwa kuvaa silaha za Mungu, tunaweza kukamata hazina za giza, na kutuwezesha kuwaokoa walio gizani na kuwarudisha wale walio gizani. Silaha saba zinazotajwa katika Waefeso 6:10-18 ni WOKOVU, KWELI, HAKI, IMANI, UTAYARI,NENO, na MAOMBI.. Silaha hizi ni muhimu kwa kukamata mali na hazina zilizofichwa gizani, kama inavyosemwa katika Isaya 45:3.

Je! Umeokoka?, Je! Unatambua kuwa Bwana Yesu yupo mlangoni kurudi. Umejiwekaje tayari? Fahamu kuwa hata kama utazipata hazina zote za gizani, ikiwa Kristo hayupo moyoni mwako, hajaondoa dhambi zako, huwezi kuurithi uzima wa milele. Fungua moyo wako leo hii utubu akuoshe dhambi zako ikiwa upo tayari kufanya hivyo, basi wasiliana nasi kwa namba zetu chini kwa ajili mwongozo wa sala ya toba.

Bwana akubariki.

Kwa mawasiliano zaidi +255693036618/+255789001312

Jiunge pia na Channel yetu ya  WhatsApp. 

“ NURU YA UPENDO” Kwa kubofya hapa>> WhatsApp: https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Masomo mengine:

Je! Ni kweli Ibrahimu na sara walikuwa ni ndugu wa baba mmoja? (Mwanzo 20:12), Na kama ni ndio, kwanini Mungu aliruhusu ndugu hao kuoana?

USIWE WEWE MWENYE KUASI.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *