Moja ya kazi ya ibilisi duniani ni kutaka kuwafanya wanadamu wadumu katika dhambi na kujifariji katika hizo, na kitu ambacho ibilisi anakitumia ili kuwafanya watu wadumu katika dhambi si kingine zaidi ya maandiko matakatifu, kumbuka, ibilisi haji na kitabu cha fizikia, au sayansi, au jiografia ili kukupotosha, bali anakuja na maneno ya maandiko matakatifu kabisa na kukupotosha huko, hii inamaanisha kuwa, endapo tusipotaka kukaa chini na kuwa waombaji kwa Mungu ili atufunze neno lake, na badala yake tutegemee watu fulani na kusikia kutoka kwao, hapo itakuwa ni rahisi sana kupotezwa.
Tabia hii ya kutokutaka kusoma maandiko kwa msaada wa Roho Mtakatifu na kuyaelewa ni sababu moja wapo ya sisi wakristo kupotea kama Bwana Yesu alivyosema..
Matayo 22:29 Yesu akajibu, akawaambia, MWAPOTEA, KWA KUWA HAMYAJUI MAANDIKO wala uweza wa Mungu.
Leo tutatazama moja ya amri kuu ya Bwana wetu na Mungu wetu, Yesu Kristo, ambayo ibilisi anaitumia hiyo ili kuwafanya watu washindwe kumwamini Kristo na kumpatia maisha yao kutokana na kutokuelewa maandiko, na amri yenyewe ni UPENDO.
Yohana 13:34 Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.
Sasa hivi ukimwambia mtu suala la wokovu, atakwambia matendo mema ndio yatakayokupeleka mbinguni, au Imani yako ndiyo itakayokuponya, tena mwingine atakuuliza, je! Unaifahamu amri kuu ya MAPENDO? Je! Unaitimiza? Pasipo kufahamu kuwa, Bwana aliwalenga watu gani alipotoa amri hiyo na upendo wa namna gani alioumaanisha hapo.
Kufahamu kuna aina ngapi za upendo na upendo maana yake ni nini? Tutumie ujumbe kwa namba +255 789001312 au hii +255 755 251 999 ili uweze kutumiwa somo lake.
Kwa kawaida, hata boyfriend na girlfriend wanaoishi katika uzinzi huwa wana upendo wa dhati na wanapendana sana, au hata yule mtu anayekula rushwa kazini kwake, huwa anawapenda sana watoto wake na familia yake yote kwa ujumla nyumbani ijapokuwa anakula rushwa, au hata wanywaji wa pombe na walevi huwa wanapendana sana na tena wananunuliana mpaka pombe wao kwa wao, halikadharika, hata wezi nao wao kwa wao, magaidi, makahaba, wavutaji sigara na wachawi pia. Hawa wote wanao upendo baina yao kwa wao, lakini nyuma yake bado wanafanya mambo yasiyompendeza Mungu.
Sasa je! Ni kweli Bwana Yesu alitoa amri hiyo ya upendo kwa watu wa namna hiyo na kuwaamuru wawe na upendo wa aina hiyo? Au watu wanaoishi maisha hayo lakini bado wanao upendo ndani yao wataingia katika ufalme wa Mungu? Jibu ni hapana, kwani biblia ipo wazi kabisa
1 Wakorinto 6:9 Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,
10 wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi.
Lakini amri hii ilimrenga nani hasa? Walengwa wa amri hiyo walikuwa ni wale waliomwamini Bwana Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao, watu waliooishi maisha ya utakatifu na kujitenga na dhambi ndani ya Kristo, watu hawa ndio Kristo anawaamuru wapendane wao kwao (yaani watu waliomini) na kuwapenda wengine ambao hawajaamini.
Hivyo ukijiona wewe bado hujatubu dhambi zako na kumwamini Kristo katika maisha yako na kubatizwa katika maji mengi na kwa jina lake sawasawa na matendo 10:48 matendo 2:38 matendo 19:5 na matendo 8:16 na unakazana kusema amri kuu ni mapendo, na wakati bado ni mzinzi, mnywaji pombe na mlevi, unapokea na kutoa rushwa, ni mwizi, mtukanaji, mwenda kwa waganga, mfanyaji masturbation na mtazamaji wa pornography, msengenyaji na mwongo, unatembea nusu uchi kwa kuvaa mavazi yanayoonesha maungo yako barabarani, unawaomba watu waliokufa (machukizo kwa Bwana) na unayasujudia masanamu ya Maria, Yesu, na Yosefu Kama ishara ya kumwabudu Mungu, basi fahamu kuwa, umeshadanganywa na ibilisi juu ya amri hiyo ya mapendo, Kama unafanya hivyo vyote ukitegemea upendo ndio utakuokoa, basi fahamu kuwa umeingia katika udanganyifu wa ibilisi, unachotakiwa kufanya ni kudhamiria kwa dhati moyoni mwako kuacha yote hayo na kutubu, Kisha kwenda kubatizwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako na ndipo huo upendo wako utakuwa na faida na wa thamani mbele za Mungu.
Tafadhari washirikishe na wengine ujumbe huu
Bwana akubariki, shalom.
+255652274252/ +255789001312
Mada zinginezo:
Mjumbe wa agano la kwanza alikuwa ni nani?
BASI WAKIWAAMBIA, YUKO JANGWANI, MSITOKE; YUMO NYUMBANI, MSISADIKI.
Je! Ni sawa kuwa na sala au maombi maalum kwa Malaika fulani kibiblia?
ITAMBUE NA KUIFANYA HUDUMA YA YOHANA MBATIZAJI KATIKA UKRISTO WAKO.