Je! Tunapaswa kushika sabato kulingana na Isaya 66:23?

SWALI: Shalom, jina la Bwana wetu na Mungu wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele. 

Isaya 66:23 inasema…

[Isaya 66:23]  Na itakuwa, MWEZI MPYA HATA MWEZI MPYA, NA SABATO HATA SABATO, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema Bwana. 

Je! Kulingana na andiko hilo, wakristo tunapaswa kushika sabato? Kwa sababu tunaona hata katika utawala ujao wanadamu watakuwa wakishika hiyo na kwenda kuabudu mbele za Mungu siku ya sabato?


JIBU: Andiko hilo limekuwa likitumiwa na baadhi ya watu kuwapotosha wale ambao bado hawaja fahamu maandiko matakatifu kutokana na, ama uchanga wao katika Ukristo, au uvivu wa kusoma maandiko matakatifu binafsi na kumwomba Roho Mtakatifu, hivyo kupelekea kuchukuliwa na kila aina ya mafundisho ya namna hiyo na mengine mengi mno kama, vile kujiepusha kula vyakula fulani fulani, kuwaomba wafu na kuyasujudia masanamu, kubatiza watoto wachanga n.k mafundisho ambayo hayapo kwenye maandiko bali kutoka kwa adui.


Turudi katika mada. Watu hao husema, Sabato ni lazima ushikwe kwa sababu hata katika utawala ujao itakuwa ikishikwa kama tulivyosoma katika Isaya 66:23. Sasa je! Hilo ni kweli? Jibu ni hapana. Hao ni viongozi vipofu wanaowaongoza vipofu kwa kutokutaka kujifunza kutoka kwa Roho Mtakatifu Kama Bwana alivyosema katika….

[Matayo 15:14] Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili. 

Tukisoma kitabu cha Zekaria 14:16, biblia inasema….

[Zekaria 14:16] Hata itakuwa, ya kwamba kila mtu aliyesalia wa mataifa yote, waliokuja kupigana na Yerusalemu, ATAKWEA MWAKA BAADA YA MWAKA ILI KUMWABUDU MFALME, BWANA WA MAJESHI, NA KUISHIKA SIKUKUU YA VIBANDA.

Sasa je! Kwa andiko hilo si tunapaswa tushike sikukuu ya vibanda pia? Manake nabii Zekaria anasema itakuwapo pia katika utawala ujao na watu wataenda kumwabudu Mungu? 

Umeona hapo? Tukishika sabato kwa sababu itakuwapo pia katika utawala ujao, basi hatuna budi pia kushika na sikukuu ya vibanda kwa sababu itakuwepo pia katika utawala ujao, na sikukuu ya mwandamo wa mwezi pia kama maandiko yalivyosema katika hiyo Isaya 66:23

[Isaya 66:23]  Na itakuwa, MWEZI MPYA HATA MWEZI MPYA, na sabato hata sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema Bwana. 

Hivyo, sikukuu zote za wayahudi ikiwemo mwandamo wa mwezi yaani mwezi mpya, sabato, sikukuu ya vibanda, baragumu n.k ni vivuli na vilikuwa vinamfunua Yesu Kristo katika agano jipya, na wala mtu asikuhukumu wewe kwa hivyo

Wakolosai 2:16  Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au MWANDAMO WA MWEZI, AU SABATO; 

17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. 

Sasa ukitaka kufahamu ni kwa namna gani vilimfunua Kristo, basi, tutumie ujumbe kwa namba hii +255 789001312 au hii +255 755 251 999

Hivyo, kwa kuhitimisha ni kwamba, ukitaka kushika sabato kwa  sababu ya andiko hilo, basi huna budi pia kushika na sikukuu ya vibanda, na ya mwandamo wa mwezi, na ya mikate isiyo tiwa chachu, na ya baragumu. Sasa Kristo alikuja kufanya nini kama unataka kuishi kwa vitu hivyo? Basi fahamu kuwa umetengwa na neema yake kama Maandiko yanasema.

Wagalatia 5:4 Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. 

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Bwana akubariki, Shalom.

 +255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

Sabato zilizowekwa na wanadamu ni zipi? 


Je! Ni kweli Bwana Yesu alishika sabato kuninganana luka 4:16?


Siku sahihi ya kuabudu ni ipi, siku ya sabato ni lini?


KAMA YOSHUA ANGALIWAPA RAHA, ASINGALIINENA SIKU NYINGINE BAADAE. 


Biblia imeruhusu ubatizo wa vichanga? (kulingana na matendo 16:33)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *