Shalom
Mwongofu au aliyeongoka ni aliyebadilika mwenendo, hivyo ongoka ni “geuka”, biblia ya kiingereza imetumia neno “be converted”..
Mathayo 18.3 “akasema, Amin, nawaambia, MSIPOONGOKA na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni”.
Pia limetumika katika Marko…
Marko 4: 11 “Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano,
12 ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije WAKAONGOKA, na kusamehewa.”
Ikimaanisha wao (wanafunzi) wamejaliwa kuzielewa Siri za Ufalme, lakini wao walio nje yaani wenye mioyo migumu(Wasio amini) husikia yote kwa mifano, lakini ikiwa WATAONGOKA watasamehewa.
Neno hili limetumika pia katika nyaraka..
1Timotheo 3.6 “Wala asiwe mtu ALIYEONGOKA karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.”
Mtume Paulo akiwa anampa Timoteo Maagizo kuhusu vigezo vya kiongozi wa kanisa kuwa asiwe yule aliyeongoka karibu, yaani aliyebadili mwenendo wake karibuni ili asije akaingia katika mitego ya ibilisi kwa uchanga wake wa kiimani.
KUOKOKA/WOKOVU. Nini maana ya kuokoka?
Kuokoka/kuokolewa au wokovu ni kutolewa katika hatari fulani na mtu anayeokoa au Mwokozi. Tunapokuja katika Ukristo Wokovu ni kuokolewa kutoka hukumu ya dhambi Ambayo ni mauti, na Mwokozi ambaye ni Bwana wetu Yesu Kristo aliyefanyika dhabihu ya dhambi kwa ajili yetu [MWOKOZI].
Kama alivyosema malaika wa Mungu kuhusu mtoto atakayezaliwa..
Mathayo 1:20-21
20 “Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
21 Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake YESU, maana, YEYE NDIYE ATAKAYEWAOKOA WATU WAKE NA DHAMBI ZAO.”
Ndio maana unapoamini(kwamba Yesu ni Mwokozi wako) Unaokoka.
Mtume Paulo katika nyaraka pia anaandika..
Warumi 10:9 “ Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, “”utaokoka””.
10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”.
Pia katika Marko anasema AAMINIYE na KUBATIZWA ataokoka, asiyeamini atahukumiwa (Marko 16:16).
Kama tulivyoona kuwa kuokoka pia ni kuhusianishwa na yule aliyekuokoa. Kumekuwa na upotovu kuwa unapokiri kwa kinywa tu, basi unakuwa Umeokoka, lakini SI kweli, wokovu Halisi unahusishwa na kuamini kile alichokifanya Mwokozi. Hivyo wengine wamekuwa ni wasio na geuko la dhati ndani yao yaani hawajahusishwa na Mwokozi, lakini wanasema wameokoka kutokana na kuongozwa tu Ile sala ya Toba.
Biblia inasema kwa kinywa mtu “hukiri” hata kupata “wokovu”, tunaweza kuona kama mtu anaweza kukiri pia inawezekana “kukana”
Sasa tunawezaje kumkiri Kristo?
Tunamkiri Kristo kwa maisha yetu ya Imani, kuamini kwamba alikufa kwa ajili ya dhambi zako msalabani, Kisha unabatizwa kwa Jina lake Yesu Kristo, Kisha kuishi maisha yanayodhihirisha kuwa umekombolewa na Kristo.
Tunaokolewa kwa Imani, SI Kwa matendo, matendo huja kama matunda, baada ya kuamini. Wengine wanahisi wataokoka au watampendeza Mungu kwa matendo yao mazuri bila kumwamini Yesu Kristo.
Tusome..
Warumi 3:27-28
27″ Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani.
28 Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa IMANI PASIPO MATENDO YA SHERIA.”
Hivyo mtu anakuwa tayari kuuchukua msalaba wake kwa kukubali kudharauliwa au kutengwa kwa ajili ya Kristo, si kwa lazima au kwa hofu, la! Bali ni kwa sababu ya upendo wa Kristo kufa kwa ajili dhambi zake na kufufuka na ushindi siku ya tatu. Hapo ndipo mtu anamkiri Yesu kwa wazi au kwa nje..
Kama Yesu alivyowaambia watu wa makutano
Mathayo 10:32 “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
33 Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
34 Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.
35 Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; 36 na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.
37 Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.
38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili”
Wokovu huu pia hupatikana mtu akiwa hai duniani, hakuna wokovu baada ya kifo hapa duniani au hakuna wokovu unaopatikana Mbinguni..
2 Wakoritho 6: 2 “Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama SIKU YA WOKOVU NI SASA)”.
Hivyo hatuna budi kujithibitisha kuwa tumeokoka tukiwa duniani na kwenda Mbinguni ni kuthibitishwa tu na si kuokolewa Tena. Matunda ya wokovu hudhihirika hapa duniani tungali hai na si Mbinguni.
Amina.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.