WALE WALIO WA TOHARA WAKASHINDANA NAYE.

Biblia kwa kina, Uncategorized No Comments

Jina la Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele, Yeye ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Mungu Mkuu na Mwokozi Wetu, sifa na Utukufu ni vyake milele na milele, Amina.


Tunaposoma habari ya mtume Petro (baada ya kutoka katika nyumba ya Kornelio), na wale ndugu waliokuwa Yerusalemu, kuna jambo kubwa na la umuhimu sana ambalo sisi kama kanisa la Kristo tunapaswa kulifahamu katika neema ya wokovu tuliyopewa na Mungu,  kwa sababu, habari hiyo iliandikwa kwa ajili yetu sisi, ili kutufundisha kama mtume Paulo alivyosema katika..

Warumi 15:4 KWA KUWA YOTE YALIYOTANGULIA KUANDIKWA YALIANDIKWA ILI KUTUFUNDISHA SISIILI KWA SABURI NA FARAJA YA MAANDIKO TUPATE KUWA NA TUMAINI

Sasa hebu tusome kwa ufupi maandiko kisha tujifunze jambo muhimu kama kanisa la Kristo.

Matendo 11:1 Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu.

2 Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, WALE WALIO WA TOHARA WAKASHINDANA NAYE

3 wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. 

Baada ya mtume Petro na ndugu wengine sita kurudi Yerusalemu kutokea yafa (kwa Kornelio), baadhi ya watu katika kanisa la Yerusalemu, walishindana na mtume Petro kwa kumwambia, kwanini aliingia katika nyumba ya mataifa na kula nao (kitu ambacho si sawa kulingana na tamaduni zao). Lakini kama tunavyojua, kile kitendo cha mtume Petro kwenda kwa watu wa mataifa (kwa Kornelio), hakujitakia, bali alienda kwa ufunuo, ambao hata yeye mwenyewe haikuwa ni rahisi kuuelewa hapo mwanzo wakati anapewa.

Matendo 10:11 akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; 

12 ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani.

13 Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule.

14 LAKINI PETRO AKASEMAHASHABWANAKWA MAANA SIJAKULA KAMWE KITU KILICHO KICHAFU AU NAJISI.

15 Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi.

16 JAMBO HILI LIKATENDEKA MARA TATU; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni. 

Lakini swali la kujiuliza ni hili, kwanini watu wa kanisa la Yerusalemu walishindana na mtume Petro juu ya jambo hilo? Na hasa ukizingatia kwamba, kanisa lote la Yerusalemu (akiwepo na mtume Petro), walibatizwa kwa ubatizo mmoja, walidumu katika imani mmoja, walikuwa na Roho Mtakatifu Mmoja, na pia walitumia vyuo vya manabii na torati moja, lakini kwanini walishindana na mtume Petro kwa wakati ule? (Hapo ndipo funzo lilipo). 


Jibu ni kwamba, mtume Petro alijaaliwa kupata ufunuo wa jambo hilo kabla ya ndugu wengine wa la pale Yerusalemu. Haikujalisha kama wote walikuwa na imani moja, au wote walikuwa wana tumia maandiko ya torati na manabii, hiyo haikujalisha hata kidogo, jambo hilo halikufunuliwa kwao kama kanisa kwa wakati ule bali kwa mtume Petro, na ndio maana waliona jambo hilo kuwa ni kama kitu kigeni kulingana na tamaduni zao za ijapokuwa lilikuwepo kwenye vyuo vya manabii.

Ila ashukuriwe Mungu, jambo hilo lilithibitika kati yao na wakamtukuza Mungu, na hatimaye ufunuo ule ukaenea hadi kwa ndugu wengine katika matifa mengine waliotawanyika ambao hawakulifahamu jambo hilo kabla.


NINI TUNAPASWA KIJIFUNZA.


Na sisi pia kama kanisa, watu tuliobatizwa katika ubatizo mmoja, tuliopokea Roho Mmoja, na tunao soma vitabu vya maandiko au biblia moja, Inawezekana kabisa Mungu akamfunulia jambo mtu mmoja kwanza kama alivyofanya kwa Petro na kanisa la Yerusalemu, na jambo hilo likawa lipo kinyume kabisa na tamaduni zetu au hisia zetu ambazo tunazo kila siku katika maisha yetu kama watu wa Yerusalemu (kwani Kristo ni Yeye Yule Yule, Jana na Leo na hata milele).


Haijalishi hata kama wote tunasoma biblia moja au tuna Roho Mmoja, Mungu anaweza mfunulia jambo mtu au watu katika kanisa, na wengine wasilione kwa wakati huo pasipo kujali wao ni akina nani, kwa sababu hata Kanisa la Yerusalemu walikuwapo mashemasi, wainjilisti, manabii kama wakina Yuda, Agabo na Sila, lakini hawakufunuliwa hilo isipokuwa Mtume Petro.


Hivyo basi, likitokea jambo kama hilo katika kanisa, ni wajibu wa wale wengine (ambao hawajafunuliwa), kusikiliza, kutafakari, na kuthibitisha katika maandiko ili kuona ukweli kwa sababu neno la Mungu ndio kitabu cha kutusahihisha na sio kushindana na mtu aliyefunuliwa kama wale wa tohara walivyoshindana na mtume Petro.

Bwana akubariki, Shalom.

Shea na kanisa la Kristo ujumbe huu.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

NA MANENO YA MANABII YAPATANA NA HAYO, KAMA ILIVYOANDIKWA.


NAO WALIOPOKEA NENO LAKE WAKABATIZWA.


JE! NI LAZIMA MTU AFAHAMU LUGHA YA KIEBRANIA ILI AWEZE KUELEWA MAANDIKO?


INJILI YA KRISTO HAIENDI NA WAKATI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *