NAO WALIOPOKEA NENO LAKE WAKABATIZWA.

  Biblia kwa kina, Uncategorized

Jina la Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele, Yeye ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Mungu Mkuu na Mwokozi Wetu, sifa na Utukufu ni vyake milele na milele, Amina.


Tunaposoma maandiko sehemu kadhaa wa kadhaa, tunagundua kuwa, watu wote waliohubiriwa injili na kumwamini Yesu Kristo, walibatizwa (Kufunua kwamba, ubatizo ni agizo muhimu sana na la lazima kwa mtu ye yote yule aliyeamini). 

Kwamfano; ile siku ya Pentekoste baada ya Mtume Petro kuwashuhudia watu kwa maneno Mengi, biblia inasema kuwa, wote waliopokea neno lake wakabatizwa.

Matendo 2:41 NAO WALIOPOKEA NENO LAKE WAKABATIZWA; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. 

Na tena, si hao tu, hata Krispo mkuu wa sinagogi na watu wa nyumba yake huko korintho na watu Koritho walioamini, walibatizwa.

Matendo 18:8 Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, WALIAMINIWAKABATIZWA

Kornelio na watu wa nyumba yake waliosikia neno la Bwana, Yule askari wa gereza na watu wa nyumbani mwake waliosikia neno la Bwana, Mwanamke Lidia na watu wa nyumba yake, n.k, wote hawa walibatizwa baada ya kuamini. Sasa  swali ni Kwanini watu wabatizwe? Jibu ni kwamba, tunabatizwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu baada ya kumkiri Kristo kuwa ni Bwana kama tu na Paulo na yeye alivyobatizwa na kupata ondoleo la dhambi zake (Matendo  22:16)

Lakini ibilisi kwa kujua madhara ya ubatizo huu kwa mtu aliyeamini, ameamua kuupotosha usifanyike kabisa, au kama ukifanyika, basi usifanyike ipaswavyo, yaani vinginevyo kabisa. Achilia mbali watu wanaopinga kabisa suala la ubatizo kwa kusema kuwa ni Fashion tu ya wakristo (Wakati ni amri, Matendo 10:48). Watu wanabatiza vinginevyo kabisa kwa kukosa ufunuo na ulewa wa maandiko wakitumia andiko hilo.

Matayo 28:19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, MKIWABATIZA KWA JINA LA BABA, NA MWANA, NA ROHO MTAKATIFU; 

Hapo tunaona Bwana anawaagiza wanafunzi wake wakabatize kwa jina la Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, kumaanisha kuwa, Baba analo jina, Mwana analo jina, na Roho pia analo jina. Lakini kabla ya kwenda kutazama jina la Baba ni lipi au la Mwana, inatupasa tufahamu kuwa, kitendo hicho cha kubatiza hakikuwa kigeni kwa wanafunzi, na wala hawakuanza kubatiza watu pale siku ya Pentekoste, la hasha! Mitume walianza kazi hiyo ya kubatiza watu tangu wakati walipokuwa na Bwana duniani.

Yohana 4:1 Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza, 

2 (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, BALI WANAFUNZI WAKE,) 

Umeona hapo? Hivyo Mitume walishakuwa na uzoefu na kufundishwa kubatizwa tangu walipokuwa wakitembea na Bwana. Lakini swali la kujiuliza ni hili? Kwanini tunaona mitume hao walibatiza kwa jina la Mwana tu! ambalo ni Yesu Kristo?

Matendo 10:48 AKAAMURU WABATIZWE KWA JINA LAKE YESU KRISTO. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha. 

Kama tulivyoona kuwa, mitume kubatiza hawakuanza baada ya Yesu kupaa, hapana! Bali tangu walipokuwa nae, hivyo basi, walivyombatiza Kornelio na watu wengine wote kwa jina Yesu Kristo, ndivyo walivyokuwa wakibatiza tangu awali walipokuwa na Bwana.


Sasa jina la Baba ni lipi? Na la Mwana ni lipi? Na la Roho Mtakatifu ni lipi?


TUKIANZA NA JINA LA MWANA.

Jina la Mwana hakuna asiyelitambua (labda kama sio Mkristo). Jina la Mwana ni Yesu Kristo, jina ambalo ni Kuu na lenye nguvu kupita majina yote, jina ambalo Bwana kwa hilo alisema tutatoa mapepo (Marko 16:17), na wala hapana jina jingine chini ya Mbingu litupasalo sisi wanadamu kuokolewa kwalo, kwa jina hili mitume walitoa mapepo, walihubiri kwa nguvu, walifufua wafu na kuwaponya viwete.

Matendo 4:10 jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa KWA JINA LA YESU KRISTO WA NAZARETHI, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, KWA JINA HILO mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu.

11 Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni.

12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, KWA MAANA HAPANA JINA JINGINE chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. 

JINA LA BABA.

Tumekwisha kuona kuwa, Jina la Mwana ni Yesu Kristo, jina ambalo ni Kuu na lenye nguvu, na kwa jina hilo la Yesu Kristo, mataifa wanahubiriwa habari ya toba na ondoleo la dhambi.

Luka 24:46 Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; 

47 na kwamba mataifa yote watahubiriwa KWA JINA LAKE habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. 

Na Jina hili la Mwana, ambalo ni Yesu Kristo, Maandiko yanatuambia kuwa, alilirithi, yaani kutoka kwa Baba.

Waebrania 1:4 amefanyika bora kupita malaika, KWA KADIRI JINA ALILOLIRITHI LILIVYO TUKUFU kuliko lao. 

Hivyo, kama Mwana alilirithi jina hilo Kuu na Tukufu kutoka kwa Baba, basi pia Jina la Baba Ni Yesu Kristo, na kwa jina hilo la YESU KRISTO, kila goti litapigwa, la vitu vyote vya Mbinguni na duniani 

Wafilipi 2:9 Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, AKAMKIRIMIA JINA LILE LIPITALO KILA JINA

10 ILI KWA JINA LA YESU kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; 

ROHO MTAKATIFU.

Tumeshaona jina la Mwana ni Yesu Kristo, ambalo alilirithi kutoka kwa Baba, na Bikira Maria alipata mimba Kwa uweza wa Roho, hivyo Baba ndiye Roho, Mwenye jina  hilo la Yesu Kristo ambalo Mwana alilirithi.

Na ndio maana ukisoma maandiko utaona watu wote walibatizwa kwa jina hilo la Yesu Kristo na wala si vinginevyo.

1 Wakorinto 1:13 JE! KRISTO amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? AU JE! MLIBATIZWA KWA JINA LA PAULO?

14 Nashukuru, kwa sababu sikumbatiza mtu kwenu, ila Krispo na Gayo; 

15 mtu asije akasema kwamba MLIBATIZWA KWA JINA LANGU

Ndugu, ikiwa ulibatizwa kwa jina jingine lolote lile tofauti na jina LA YESU KRISTO, liwe la Branham, Mchungaji wako au kiongozi wako, basi fahamu kuwa ulibatizwa kimakosa, unachopaswa kufanya ni kutafuta ubatizo sahihi na wa kimaandiko kwa sababu Bwana Yesu aliwaambia Mitume wake hivi…

Luka 10:16 AWASIKILIZAYE NINYI ANISIKILIZA MIMI, NAYE AWAKATAAYE NINYI ANIKATAA MIMI; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma. 

Na Mtume Petro alisema hivi.

Matendo 2:38 Petro akawaambia, Tubuni MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 

Kumaanisha kwamba, unapokataa agizo hilo la kubatizwa kwa jina la Yesu Kristo, maana yake umemkataa Bwana Mwenyewe.

Bwana akubariki, Shalom.

Tafadhari washirikishe na wengine wa ujumbe huu.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

JE! KAMA BWANA YESU NDIYE MUNGU, KULE MLIMANI ALIENDA KUMUOMBA NANI? (Luka 6:12)


BASI ‘BWANA’ NDIYE ROHO.


NI BWANA GANI HUYO AMBAYE MANABII WALITABIRI KWA JINA LAKE NA KUTESWA KWA AJILI YAKE?


FAHAMU NINI MAANA YA MUNGU NI ROHO (Yohana 4:24)


JE! NI LAZIMA MTU AFAHAMU LUGHA YA KIEBRANIA ILI AWEZE KUELEWA MAANDIKO?

LEAVE A COMMENT