NA MANENO YA MANABII YAPATANA NA HAYO, KAMA ILIVYOANDIKWA.

  Siku za Mwisho, Uncategorized

Jina la Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristo lipewe sifa milele na milele, Yeye ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Aliyeko na Aliyekuwako na Atakayekuja, Mwenyezi. Amina.


Lipo jambo la kujifunza katika habari ile tunayoisoma ya watu wa tohara walioleta mafundisho MENGINE KABISA KATIKA INJILI YA KRISTO juu ya watu wa mataifa kutahiriwa, na jambo lenyewe ninalotaka tujifunze ni jinsi gani mitume walivyoweza kulihakiki na kuthibitisha ukweli na uongo wa jambo hilo. Tunajifunza kwamba, mitume hawakutumia mawazo yao na akili zao kuthibitisha na kuhakiki jambo hilo, mitume hawakwenda pale kwenye msalaba au mti (vyo vyote ulivyokuwa) ambao ulisimikwa na kuanza kutafuta-tafuta kwa fufukua fukua pale, na wala hawakutumia hisia zao binafsi kuthibitisha Neema ya Wokovu kwa watu wa mataifa na kutahiriwa kwao bali WALITUMIA MAANDIKO MATAKATIFU na kuona kwamba, jambo hilo la kutahiriwa kwa watu wa mataifa halina ulazima wowote na linapatana na maneno ya Manabii kama ilivyoandikwa.

Matendo 15:13 Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni.

14 Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake.

15 NA MANENO YA MANABII YAPATANA NA HAYO, KAMA ILIVYOANDIKWA,

16 Baada ya mambo haya nitarejea, Nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, Nami nitaisimamisha; 

17 Ili wanadamu waliosalia wamtafute Bwana, Na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao; 18 Asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele. 

Umeona hapo? Sasa tabia hii inapaswa kuwepo pia kwa kanisa la Kristo sasa hivi katika siku hizi za mwisho, kwani habari hiyo haikutangulia kuandikwa tu kama hadithi fulani, basi! Bali kwa lengo la kutufundisha sisi ili kwa saburi na faraja ya maandiko hayo tuwe na tumaini.

Warumi 15:4 Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini. 

Leo hii kuna mafundisho MENGINE MENGI KABISA ya kishetani na ya roho zidanganyazo yaliyoingizwa na ibilisi katika imani ya kikristo kama tu ilivyokuwa kipindi kile cha mitume, (kwa sababu kama ibilisi alijaribu kuingiza uongo huo katika injili ya Kristo wakati wa mitume unategemea vipi ashindwe na sasa?). 


Utaambiwa, Mwanamke kuwa askofu au mchungaji hakuna shida, Ubatizo kwa mtu aliyeamini hauhitajiki si lazima sana, kuashiriki meza ya Bwana haina haja, kutawadhana miguu Kristo hakumaanisha tufanye hivyo. Ndugu Mkristo, unapaswa kuhakiki mafundisho na mawazo kama hayo ili uone kama yanaendana na maandiko matakatifu na sio kupokea pokea tu, leo hii utaambiwa na nabii Hellen G White kwamba, nimeona amri ya kushika sabato ndio kubwa kushinda zote, na inang’aa sana kama jua, na wewe unakubali tu, mpendwa, nenda kwenye maandiko uone kama yanasema amri inayong’aa kama jua na kubwa kushinda zote ni sabato.


Ukiambiwa na kiongozi wako kipofu kuwa Mariamu ni kimbilio la wakosefu, usikubali tu, nenda kachunguze biblia yako uone kama Mariamu ni kimbilio la Wakosefu na sio Yesu Kristo.


Utaambiwa Kristo anarudi siku fulani, au Kristo anarudi saa fulani, uza nyumba uza mali, na wewe unakubali kubali tu wakati maandiko yanasema hakuna mtu haijuaye siku wala saa (isipokuwa Mungu tu, Yesu Kristo). Utambiwa Kristo kazaliwa Tarehe 25 December na wewe unakubali tu, nenda kwenye maandiko yako uone kama yanasema hivyo.


Sisi kama kanisa la Kristo hatuna budi kuhakiki na kuona kama vitu hivyo vinaendana na maandiko matakatifu kama mitume walivyofanya, kwa sababu Roho Mtakatifu hawezi jichanganya kamwe, iwe katika maona au mafundisho yoyote yale.


Hata katika biblia, manabii katika agano la kale na mitume katika agano jipya hawakupingana hata kidogo, kwanini?wote walikuwa na Roho Mmoja, Paulo hakupingana na Isaya, na wala Habakuki hakupingana na Yuda, kwa mfano; hata katika maono aliyoyaona mtume Yohana hayakupingana na maandiko, mlango aliouna mtume Yohana ukifunguka mbinguni katika manona yake (Ufunuo 4:1), ndio malango huo huo aliouona Yakabo Mwana wa Isaka (Mwanzo 28:16). Mfumo wa madhabu ya Mbinguni aliyoiona mtume Yohana kwenyewe maono yake, ndio huo huo aliouona nabii Musa kule mlima sinai (kutoka 25:40). Yerusalemu mpa aliyoiona mtume Yohana ikishuka kutoka mbinguni, ndio hiyo hiyo aliyoiona nabii Isaya, kiti cha enzi kimoja na alichokiona Isaya Mbinguni ndicho alichokiona nabii mikaya, Danieli na ndicho alichokiona mtume Yohana (na mmoja ameketi juu yake).


Hivyo basi, Ni lazima turejee kwenye maandiko na tuone kama yote tunayofundishwa na kufundisha yanapatana na maandiko kwani hiyo ndio taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu na sio mawazo binafsi.

Tafadhari washirikishe na wengine wa ujumbe huu.

Bwana akubariki, Shalom.

+255652274252/ +255789001312


Mada zinginezo:

MAKANISA NA MAFUNDISHO YA UONGO YANAYOPOTOSHA WATU WENGI NYAKATI HIZI ZA MWISHO (sehemu ya 07)


Tabia moja ya unafiki unayopaswa kuiepuka.


Je! Agizo la Bwana kwa mitume wake la kufufua wafu lilikuwa ni kwa baadhi ya mitume tu?


INJILI YA KRISTO HAIENDI NA WAKATI


JE! KAMA BWANA YESU NDIYE MUNGU, KULE MLIMANI ALIENDA KUMUOMBA NANI? (Luka 6:12)

LEAVE A COMMENT