Mihimili mikuu (4) ya mkristo katika safari yake ya wokovu.

Ili mkristo yeyote aweze kusimama, na kuwa na ustawi mzuri wa maisha yake ya kiroho, basi hana budi kuhakikisha mambo haya manne yamesimama vema ndani yake.

  1. Neno la Mungu
  2. Maombi
  3. Ushirika
  4. Kuangaza Nuru

Tukisoma kitabu cha matendo ya Mitume sura ile ya pili utaona, pindi tu wale watu walipoamini Injili ya mitume na kubatizwa, hawakukaa hivi hivi tu, kwamba ndio basi wameshaokolewa, wanasubiri kwenda mbinguni, hapana, bali utaona mara moja hawakukawia bali walizitimiza nguzo hizo kuu tatu (3) za kwanza, yaani Kujifunza Neno la Mungu, kuendelea katika sala na maombi, na kudumu katika ushirika.

Matendo 2:41 Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.

42 Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.

Sasa, ni vema tutazame kwa undani kidogo, ni kwa namna gani tunapaswa na sisi tuenende katika kanuni hizo; .

1.) Tukianza na Kujifunza Neno la Mungu:

Kama tunavyojua, chakula ndicho kinachomfanya mtu akue katika mwili, asipokula atakufa, au akila lishe duni, atadumaa asikue ipasavyo. Vivyo hivyo katika roho pia, Neno la Mungu ndio, chakula chetu(Mathayo 4:4). Ili roho yako ikue huna budi kujifunza Neno la Mungu kila siku.

Ikiwa utasema upo ndani ya wokovu, halafu kinapita kipindi kirefu, hujasoma Neno na hauoni shida yoyote ndani yako, ujue umeshakufa kiroho siku nyingi.. Mtu aliye hai kiroho, ni lazima aone njaa, asipoishibisha roho yake, ni lazima ajifunze Neno la Mungu.

Mungu hawezi kukutumia au kumwelewa anapozungumza na wewe kama huna Neno la Kutosha ndani yako, Shetani huwezi kumshinda kama Neno halijajaa ndani yako. Utachukuliwa tu na kila aina ya mawimbi ya adui.

Biblia inasema..

Wafeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;

14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu”.

2) MAOMBI.

Maombi ni kama mafuta kwenye gari, Sikuzote gari likipungukiwa mafuta haijalishi litakuwa ni zuri namna gani, haliwezi kwenda popote, sivyo? Vivyo hivyo katika roho ili usonge mbele katika safari yako ya wokovu, huna budi kuwa mwombaji.

Ukiwa mwombaji unajikinga na majaribu mengi ya ibilisi.

Mathayo 26:40 “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?

41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.

Kiwango cha chini Bwana alichotupa cha kuomba ni Saa moja kwa siku kama tunavyosoma hapo juu..

Hivyo anza kujijengea utaratibu wa kujifunza kuomba kila siku, ongeza dakika tano kila siku, katika uombaji wako, na ghafla utashangaa kwa siku unaweza kuomba hata saa moja na zaidi bila ugumu wowote.

Lakini usipokuwa mwombaji, ni ngumu sana kuyakwepa majaribu na mawimbi ya shetani. Safari yako ya wokovu itakuwa ni ya kusua sua sana.

3) USHIRIKA.

Ushirika, ikiwa na maana kukutanika na watakatifu wengine ili kufanya ibada, ambapo ndani yake, kuna kumsifu na kumwabudu Mungu, kuumega mkate, kutawadhana miguu, kujengana kiroho n.k.. Hili ni jambo la msingi sana. Bwana alisema..

Waebrania 10:25 “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”.

Wapo watu wanasema mimi kivyangu vyangu inatosha..Ni kweli wokovu ni wewe binafsi, lakini si vyote utavitimiza peke yako. Utamuhitaji mwenzako, na vilevile mwenzako atakuhitaji wewe. Chuma hunoa chuma, haiwezekani chuma kikajinoa chenyewe..(Mithali 27:17) Vilevile biblia inasema kamba ya nyuzi tatu haikati haraka (Mhubiri 4:12), na walalapo wawili watapata joto, Je! Mmoja atatolea wapi joto?

Hivyo ikiwa umeokoka hivi, karibuni tafuta ndugu unaoona wamesimama vema katika imani, kaungane nao katika ushirika, katika kuumega mkate, katika kumsifu Mungu na kumwimbia, usibaki peke yako peke yako nyumbani, Ni hatari sana katika maisha ya kiroho.

4) KUANGAZA NURU.

Kuiachia nuru yako imulike kwa wengine, Bwana Yesu alisema..

Luka 11:33 “Hakuna mtu awashaye taa na kuiweka mahali palipositirika, au chini ya pishi; bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuuona mwanga”.

Hapa ndipo linakuja jambo la kuwashuhudia wengine pia  habari njema, kuwaonyesha wengine kuwa umeokolewa, au  kusambaza kazi ya Mungu, , kuitumia karama yako kwa Bwana, kama ni kumwimbia, kama ni kufundisha, n.k.

Kwahiyo ukizingatia kanuni hizo nne, basi uhakika wa kumaliza safari yako salama duniani upo, tena yenye mafanikio makubwa. Hivyo anza kutendea kazi pale ulipokuwa unazembea, na Bwana awe pamoja nawe daima.

Bwana akubariki.


Mada zinginezo:

KAZI NYINGINE YA MAANDIKO MATAKATIFU KWA WAFUASI WA YESU KRISTO (SEHEMU YA KWANZA).


UMEMWAMINI YESU KRISTO KWA NAMNA GANI?


Nini maana ya mstari huu? “Na amani ya Kristo iamue miyoni mwenu” (Wakolosai 3:15)


Nini maana ya mstari huu “Nimesulubiwa pamoja na Kristo?” (Wagalatia 2:20)

2 thoughts on - Mihimili mikuu (4) ya mkristo katika safari yake ya wokovu.

LEAVE A COMMENT