Maana ya ubatizo wa Moto

Maswali ya Biblia No Comments

Yohana aliwabatiza watu kwa maji lakini alisema atakapokuja Bwana Yesu atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto, huu ubatizo wa moto maana yake ni nini? Na sote  tunatambua kuwa moto hufanya kazi kuu tatu.

Ya kwanza ni:

Kuunguza na kuteketeza vitu visivyofaa kama vile takataka. Hapa ni pale Mungu anapozichoma dhambi zote zilizo ndani ya mtu na ndipo mtu anafikia hatua ya kukosa kabisa hamu ya kutenda dhambi ambazo amewahi kuzifanya, pengine alikuwa anavuta sigara anaacha hapati tena kiu ya kuvuta, alikuwa mlevi ghafla kiu ya pombe inaisha, alikuwa mzinzi lakini anaacha na kiu ya kuzini inaondoka, alikuwa anasengenya wenzie lakini anaanza kusikia hatia ndani yake, alikuwa anavaa nguo za nusu utupu lakini ghafla anaona aibu kuzivaa na mambo mengine kadha wa kadha yasiyofaa.

Ya pili :

Moto huimarisha kitu kigumu ili kiwe kigumu na kipate kuimarika zaidi,mfano dhahabu hupitishwa kwenye moto ili ing’ae zaidi. Hapa Roho Mtakatifu humpitisha mtu katika moto ili apate kuimarika zaidi. Mfano, wafuaji huyeyusha madini ndani ya moto mkali na badae huganda na kuleta mng’ao mzuri zaidi lakini kwa macho ukiyaangalia utaona yanapitia mateso makubwa kwa kuwekwa katika moto mkali lakini wanapomaliza kuyachoma yanakuwa na ubora zaidi ya yalivyokuwa mwanzo

(tunaona hata matofali ya udongo huchomwa kwanza kabla hayajatumika kujenga nyumba).

Jambo hili hututokea na sisi watoto wa Mungu, tunapompokea Roho Mtakatifu, Mungu huruhusu tupite katika moto wa MAJARIBU ili imani zetu ziimarike hata yakija mambo magumu tusianguke kwa wepesi.

Kuna wakati tunaona mtu aliyeanza safari ya wokovu pale tu anapomkiri Yesu na kumuamini vitu huanza kubadilika, ghafla ndugu zake wanamchukia na hata kumtenga kabisa, mwingne atapata misiba, magonjwa, anguko la kiuchumi n.k. Hata wakina Ayubu, Yusufu waliyapitia hayo, Mungu anapoyaruhusu hayo ni kwa ajili ya kumuimarisha na sio kumuumiza, na Mungu humpa neema mtu huyo wakati wote anapopitia hayo ili aweze kushinda kwa sababu hataki tujaribiwe kupita uwezo wetu.

1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili”.

1Petro 1: 6 Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;

7 ili kwamba KUJARIBIWA KWA IMANI YENU, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.”

Na huu ndo ubatizo wa moto, Mtu yoyote aliyeamua kumfuata Kristo lazima aupitie. Ubatizo wa maji na wa moto tunaoupitia sisi, mitume na manabii waliupitia pia na hata Bwana wetu Yesu Kristo aliupitia.

Hatua ya tatu 

Ni kuchochea ,moto unapowashwa tunategemea utachochea kitu fulani,kwa mfano kuna moto huwekwa ndani ya bunduki ukiwashwa husababisha risasi ifyatuke. Hata moto ukiwekwa chini ya sufuria yenye maji, yale maji lazima yatachemka.

Ndivyo ulivyo moto wa Roho Mtakatifu ukishuka ndani ya mtu, mtu huyo hawezi kukaa atatoka kwenda kuwaambia wengine habari za Kristo. Jambo kama hili lilitokea ile siku ya Pentekoste mitume waliupokea ubatizo wa moto na hapo hapo wakaanza kuieneza injili kwa haraka.

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *