Wakamshinda kwa damu ya Mwanakondoo,

Maswali ya Biblia No Comments

 

Shalom, Karibu tujifunze Neno la Mungu,

Leo kwa Neema za Bwana tutakwenda kuangalia ni namna gani tunaweza kushinda au kuleta majibu ya haraka pale tunapoitumia damu ya Yesu Kristo,

Kwasababu watu wengi hasa waliookoka wamekuwa wakiita sana damu ya Yesu katika mambo yao mengi, pengine hata kwenye kuomba kwao lakini majibu ya kile walichokitarajia yanakuwa ni madogo au wasione kitu kabisa…

Tunapoizungumzia damu ya Yesu Kristo/ Jina la Yesu,tunazungumzia ile mamlaka iliyopo ndani yake, nayo ni mamlaka ya uweza na nguvu yenye kufanya mambo yote..

Kipindi hicho na mimi nilikuwa mmoja wapo Katika hili jambo, kinywani mwangu nilikuwa siachi kuitaja au kuomba bila kuitamka damu ya Yesu, ijapokuwa sio jambo baya ila usipojaa maarifa zaidi ya kutosha ya Neno la Mungu, utajikuta unabaki pale pale 

Embu tusome..

Ufunuo wa Yohana 12:11

[11]Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na KWA NENO LA USHUHUDA WAO; AMBAO HAWAKUPENDA MAISHA YAO HATA KUFA.

Ukisoma hilo andiko kuanzia juu utaelewa ni habari inayomzungumzia shetani jinsi alivyotupwa chini baada ya kushindwa, pamoja na malaika zake (mapepo)

Lakini ukisoma huo mstari wa kumi na moja anakupa uelewe ni kwa namna gani waliweza kushinda ,kwasababu na wao pia waliitumia damu ya Yesu ndo mana wakashinda ,na kufanikiwa kumtupa shetani chini,

Tutaangalia Vipengele viwili vilivyohorodheshwa kwenye huo mstari..

1, NA KWA NENO LA USHUHUDA WAO

Hawa walifanikiwa kumshinda shetani sio tu kwa kuiita damu ya Yesu,bali kupitia Neno la ushuhuda, walitumia ushuhuda wa maisha yao wanayoishi kila siku na kufanikiwa kuleta ushindi,

Ikiwa na wewe leo unataka uone ushindi kwenye maisha yako, usiridhike tu kuiita,damu ya Yesu,damu ya Yesu, asubuhi mpaka jioni unaiita tu, unaweza ukaona matokeo ila yasiwe yote, lakini kichukue hiki walichokifanya hawa,  walitumia ushuhuda wa maisha yao, jinsi Mungu anavyowapigania, anavyowalinda, amewapa pumzi, walikaa na kutafakari wema wa Mungu anaowatendea kila siku wakaona wanayo sababu ya kuendelea mbele katika imani, hivyo wakafanikiwa kuangusha chini mitego yote ya adui,

Utakuta mtu ni mkristo,ameokoka,anakuambia Bwana ni Mwokozi wa maisha yake lakini ngoja alale njaa siku moja au apitie magonjwa kidogo, tayari na wokovu kashaacha, ataanza manung’uniko, bila kukaa na kuanza kutafakari ushuhuda tu wa maisha yake jinsi unavyoweza kumpa nguvu, angekaa na kutafakari toka amezaliwa ni mangapi Mungu kamuepusha mpaka hapo amefika, amekulisha mara ngapi vyakula vizuri ukawa na hiyo afya, ni magonjwa mangapi ameyazui juu yako,ungemshukuru na kumtukuza Mungu kila wakati,

Lakini kwasababu hatutaki kutafakari shuhuda Mungu anazotutendea maishani mwetu ,ndipo tunajikuta kitu kidogo tu tunakuwa wepesi kumuacha Mungu au hata wokovu kabisa, Daudi alilijua hilo wakati anachukua maamuzi ya kwenda kupigana na Goliati ndo mana aliweza kumuagusha, alitumia ushuhuda mdogo tu wa yale Mungu aliyomtendea wakati anachunga kondoo za baba yake,

1 Samweli 17:34-37

[34]Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi,

[35]mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua.

[36]Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.

[37]Daudi akasema, BWANA aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na BWANA atakuwa pamoja nawe.

Lakini ushuhuda mkubwa zaidi unaoweza kutupa ushindi na zaidi ya kushinda ni NENO LA MUNGU, maandiko yanasema ushuhuda wa Yesu ni roho ya unabii,

Ufunuo wa Yohana 19:10

[10]Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.

Litumie Neno la Mungu kwenye Maisha yako likupe ushindi juu ya maisha yako, pamoja na kuzishinda hila mbovu zote za adui..

2,AMBAO HAWAKUPENDA MAISHA YAO HATA KUFA

Waliweza kupata ushindi sio tu kwa ushuhuda wa maisha yao, hapana,bali pia kwa kutokuyapenda maisha yao hata kufa, ni jambo lingine lililowaongezea ushindi zaidi kwa adui shetani..

Bwana Yesu anasema,Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.

Kutokuyapenda maisha yao hakumaanishi hawakupenda kuishi tena, hapana, bali hawakupenda yale mambo yanayoonekana ni mazuri Katika ulimwengu lakini kumbe yapo kinyume na Neno la Mungu,

Pale walipokuwa na sababu za kwenda kula anasa kwa kujirusha kwenye disko wao hawakufanya hivyo, walipoitwa kwenye bar ili wale na kunywa,wao hawakupenda hivyo, waliposemwa vibaya kwa kuambiwa wamekuwa wabibi kwa kuvaa nguo zenye heshima wao bado waliendelea na utakatifu,maana yake wameyachukia maisha yao ili wampendeze Mungu,wamekubali kuziangamiza nafsi zao kwa ajili ya Bwana,

Maandiko yanasema

1 Yohana 2:15

[15]Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

Ikiwa unataka kuwa mshindi, jitenge mbali na mambo ya ulimwengu huu, umeokoka lakini mtu akikutazama hautofautiani na yule anayeonekana anajiuza, Bwana anasema,ukiipenda dunia,hata kumpenda Mungu sahau kabisa, yasalimishe maisha yako kwa Mungu,kwa kuishi maisha yanayompendeza ndivyo utakavyoona ushindi wako, lakini unataka umshinde shetani na huku fashion za kidunia unazo, usengenyaji,ni mlevi,ni mzinzi, shetani ndiye atakayekushinda.. lakini ukijitenga mbali na mambo ya ulimwengu na kuishi kulingana na Neno lake,utamwona Bwana akikushindia sana..

Shalom..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *