
HATARI YA KUWA VUGUVUGU.
Bwana Yesu alisema kupitia Mtume Yohana..
Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, YA KUWA HU BARIDI, WALA HU MOTO; ingekuwa HERI kama ungekuwa baridi au moto16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, NITAKUTAPIKA UTOKE KATIKA KINYWA CHANGU ”.
Kama tunavyosoma, adhabu iliyonenwa hapo ya mtu atakayekuwa vuguvugu ni KUTAPIKWA,..Na mtu akishafikia hiyo hatua, basi hawezi kurudi nyuma kuokolewa tena, mtu huyo anakuwa tayari kashatengwa na uso wa Mungu milele, Ulishawahi kuona mtu yeyote akirudia kula matapishi yake tena?, Ni jambo lisilowezekana kabisa, yale matapishi sio chakula tena, ni sawa ni kinyesi tu, hata kuyatazama utaona kinyaa, na ndivyo ilivyo kwa mtu Yule aliye vuguvugu. Na ndio maana Bwana alisema ni heri uwe moto au baridi kuliko kuwa hapo katikati kwasababu mtu wa namna hiyo akishatapikwa kurudiwa tena ni ngumu.
UVUGU UVUGU NI AGENDA YA SHETANI!!.
Shetani anachofanya yeye sasa na majeshi yake, ni kuhakikisha kwa nguvu zote watu wanakuwa VUGUVUGU, yaani anahakikisha kuwa mtu anamfahamu Mungu, lakini amchanganye kidogo na mambo ya giza, anafanya juu chini mtu aende kanisani, baadaye akitoka aende disco, hataki awe ni mtu wa disco tu siku zote na asiende kanisani kabisa hata siku moja, hataki mtu awe ni wakidunia tu siku zote na hata siku moja hana habari na Mungu, anataka vyote vifanyike kwa pamoja kwasababu anajua Mungu kasema ni HERI mtu awe BARIDI kabisa kuliko VUGUVUGU.
Shetani anajua mtu aliye baridi kabisa pengine huko mbeleni akisikia ukweli kidogo anaweza kubilika hivyo hawezi kuweka tegemeo lake kubwa kwa mtu wa namna hiyo kuliko Yule aliye vuguvugu.
Na hapo ndipo anatilia mkazo, na kashafanikiwa kuwaweka watu wengi katika hali hiyo, mtu awe anajiita mkristo lakini bado ni mlevi, aende kanisani lakini bado anaenda kwa waganga wa kienyeji, kabatizwa katika ubatizo sahihi lakini bado anavuta sigara, anaimba kwaya lakini bado ni mwasherati, analipa zaka lakini bado anatoa hongo, anatabiri na kunena kwa lugha lakini bado anavaa mavazi ya kiasherati, anavaa vimini, suruali, kaptura, anapaka wanja, anahudhuria maombi lakini bado ni msengenyaji na bado anajiita mkristo, unafunga na kusali na babo unaishi na mwanamume au mwanamke ambaye hamjafunga ndoa, ni mshirika wa kwaya na bado umeachana na mke wako au mume wako..Hapo ndipo shetani anapotilia nguvu nyingi.
Shetani sasa hivi hatumii nguvu nyingi sana kuwafanya watu wawe BARIDI, yaani kuwafanya watu wasimjue Mungu kabisa, au kuwafanya wawe wa kidunia kabisa wasitake kujua Mungu au kanisa ni nini! Hapana, hatumii nguvu kubwa kuwafanya watu wasimsikie Yesu Kristo kabisa, yaani waendelee kuabudu miti, n.k. hapana hatumii nguvu kubwa huko kwasababu anajua hapo pana HERI pengine huko mbeleni neema ya Mungu ikipita juu ya huyo mtu kidogo tu anaweza kubadilika na kuwa MOTO..
Hivyo anachofanya yeye sasa na majeshi yake, ni kuhakikisha kwa nguvu zote watu wanakuwa VUGUVUGU,
MBINU ANAYOITUMIA SHETANI KUWAFANYA WATU WAWE VUGUVUGU.
Sasa shetani ili kulifanikisha jambo hilo,aliwatia mafuta watumishi wake kuwafanya watu wawe BARIDI, pamoja na kuwa VUGUVUGU, wale wanaowafanya watu wawe baridi ndio hao waganga wa kienyeji, na vikundi vya kishetani, pamoja na watu waovu wa ulimwengu huu, lakini hao kama tulivyosema sio wabaya sana, Wapo watumishi wengine wa uongo waliochaguliwa na shetani mahususi kwa kuwafanya watu wawe vuguvugu…Hawa ndio wale mbwa mwitu Bwana aliowasemea katikakati ya kondoo,.
Mathayo 7: 15 “Jihadharini na MANABII WA UONGO, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? “
Unaona hapo? Hawa wanabeba biblia kama wewe, wanajiita watumishi wa Mungu, na njia pekee ya kuwagundua si kwa kuwatazama bali ni kwa matunda yao,..kwa kutazama jamii ya watu wanaowazalisha(ndio matunda yao), utaweza kufahamu hao watumishi ni wa aina gani…kama ni vuguvugu,moto, au baridi…
Ukiona umedumu kwa muda mrefu katika mafundisho yao, na hujaona mahali popote unagusiwa juu ya hatma ya maisha yako ya kiroho kuhusu mbinguni na kuzimu, ufahamu kuwa upo katika sehemu ya hatari zaidi kuliko ungeenda kujiunga na vikundi vya kichawi au vya waganga wa kienyeji,..ukiona haugusiwi habari za mbinguni kila siku ni biashara tu na mafanikio, upo katika eneo la hatari kuandaliwa kutapikwa na Bwana.,ukiona mahali hapo haugusiwi habari za kutubu dhambi na kuishi maisha matakatifu, badala yake unahubiriwa injili za faraja tu, huku maisha yako ya kiroho yanaporomoka kila siku fahamu kuwa upo mahali pa hatari sana, inusuru roho yako.
Ukiona mahali ambapo huubiriwi misingi ya imani ya kikristo, yaani ubatizo wa maji tele, na ubatizo wa Roho Mtakatifu badala yake ni kupewa tu maji, na chumvi, na sabuni, kama njia ya kufunguliwa, kwasababu biblia inasema mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuingia ufalme wa mbinguni (Yohana 3) jua tu upo katika eneo la hatari, ukiona mahali Neno la Kristo halipewi kipaumbele au muda mrefu kuhubiriwa fahamu kuwa unatengenezewa mazingira ya kuwa vuguvugu, ukiona upo mahali hauhubiriwi usafi wa mwili wako na roho yako, haufundishwi umuhimu wa kujisitiri kwa mwanamke,(1Timotheo 2:9) unakwenda kanisani na vimini, na hauambiwi chochote, ujue kuwa upo katika mikono ya watumishi wa shetani..
Dhumuni la shetani ni kukuweka chini ya mikono yao ili uendelee kuwa vuguvugu, ufikie kipindi Fulani utapikwe na Bwana.Hata kama watafanya miujiza kiasi gani jiepushe nao Bwana Yesu alisema..
Mathayo 7: 22 “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.
Na ndio maana Bwana anasema ni HERI KUWA MOTO, AU BARIDI kuliko kuwa VUGUVUGU, kwa maana nyingine adhabu ya mtu atakayekuwa vuguvugu huko aendako itakuwa ni kubwa kuliko ya Yule aliye baridi kabisa.
Ndugu hii injili unayoisikia kila siku, na hutaki kubadilika, unasema wewe ni mkristo lakini ukiangalia maisha yako na maandiko ni mbalimbali, umejiweka katika eneo la hatari zaidi, shetani anakufurahia kukuona katika hali hiyo, akisubiria hiyo siku Bwana atakayosema basi yatosha! Ili utapikwe, shetani anataka awe na uhakika wewe unakuwa wake milele. Hataki kukupoteza kwa namna yoyote ile na ndio maana anataka uendelee katika hali yako ya UVUGUVUGU. Ujione upo sawa na Mungu kumbe haupo sawa, ujione unempendeza Mungu kumbe unamchukiza n.k, Ni mara ngapi umesikia sauti ya Mungu ikisema na wewe ndani ya moyo wako na hutaki kubadilika?.
Ndugu maneno ya Bwana YESU ni kweli na amina, hasemi UONGO wala HATANII akisema atakutapika ni kweli atakutapika, hivyo mgeukie leo Bwana kikamilifu kama hujafanya hivyo toka katika kamba za kidini na madhehebu zinazokulewesha kukufanya ujione ni mkristo kumbe sio, tafuta kweli ya Neno la Mungu kwa gharama zote. Hili ndilo SHAURI la BWANA YESU KWAKO NDUGU wa Kanisa hili la Laodikia.. kumbuka hili ndilo kanisa la mwisho kati ya yale 6 yaliyopita na hakutakuwa na lingine la nane. Hivyo mwisho umekaribia mno.
Amua leo kutengeneza maisha yako na Bwana Yesu kwa kumaanisha kabisa kubadilika na kuacha uvugu uvugu wa kishetani.
Marban atha (Bwana Yesu anarudi)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.