
LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA SIMAMA, UTUOKOE.
Ulishawahi kuwa na watu ambao wanakutafuta tu wakati wa shida ili uwasaidie..kisha baada ya hapo hawana habari tena na wewe, mpaka tena wapate shida wanakutafuta, kama ndio, basi kuna hali Fulani ulijisikia ambayo sio nzuri, ni kweli wapo ambao mazingira yanawabana washindwe kukutafuta nyakati nyingine, lakini wapo ambao wewe kwao ni mtu wa kuwatatulia tu matatizo, Habari nyingine na wewe hawana..
Sasa hiyo hali ndiyo ambayo Mungu anapitia sasahivi kwa watu wengi duniani, biblia inasema..
Yeremia 2:27 “waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana WAMENIPA MIMI VISOGO, wala hawakunielekezea nyuso zao; LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE”.
Umeona, wanadamu wengi sasa kinachowapeleka kwa Mungu, si kingine Zaidi ya kuomba, wafunguliwe, kuomba waponywe, kuomba wafanikishwe kiuchumi, kuomba kazi, n.k.
Lakini ukiangalia mahusiano waliyonayo na Mungu ni hafifu sana au hakuna kabisa.. wanaenda kanisani kwasababu ya matatizo yao tu, wakishatoka huko wanakuja kuendelea na maisha yao ya dhambi.
Leo hii tembelea mahospitalini uone jinsi watu wanavyojua kuomba, kwa jicho la kawaida utawahurumia sana na kuona kwamba wanastahili kuponywa kwa jinsi wanavyoomba kwa bidii, huwezi kudhania kuwa huyo mtu akitoka hapo anaweza kurudia njia zake mbaya, lakini acha atoke hapo apone tatizo lake, anampa Mungu kisogo.. anaendelea na miungu yake, na ulevi wake, uzinzi wake n.k kisha akipata tena shida anamtafuta Mungu.
Kuna mtu aliwahi kunipigia simu hapo nyuma, akanieleza tatizo lake akaniambia mtumishi nahitaji maombi nimefika muda wa kujifungua lakini sioni uchungu, nakaribia kumaliza mwezi sasa..nikamjibu haina shida tutaomba na Bwana atakusaidia, lakini wakati tunaendelea kuongea..hapo hapo Roho Mtakatifu akasema na mimi, akaniambia mwambie huyo mama atajifungua kesho, lakini baada ya hapo anitafute. Nikamwambia mama, kesho utajifungua lakini Mungu anasema na wewe kwamba ukishajifungua na kupata nguvu umtafute. Akanijibu sawa, hapo hapo tena Roho Mtakatifu akaniambia na jina la huyo mtoto nikamjuza mama.. naye akaniambia kuna jina ndugu zake walikuwa wamepanga kumpa, nikamwambia Roho Mtakatifu amesema huyo mtoto aitwe kwa jina hili.
Kesho yake mama atajifungua kama Roho Mtakatifu alivyonena na mimi ule ule muda, lakini ikapita muda kidogo nikawa namtafuta yule mama simpati, ikapita kama miezi mitano..akaja akanitafuta, nikamtambua maana sikufuta namba zake, nikamwambia mtoto anaendeleaje akaniambia vizuri Mungu ni mwema, lakini mtumishi nina shida na mume wangu naomba uniombee, nikamuuliza unakumbuka ujumbe wa Roho Mtakatifu? Akanijibu hapana naomba unikumbushe tena samahani. Kwakweli nguvu ziliniisha nikakosa cha kusema, nikakata simu. baadaye nikamtafuta. Lakini Roho Mtakatifu akaniambia watu hawa wanafumba macho yao wenyewe sawa sawa na Mathayo 13:15. Lakini pia WAMENIPA MIMI VISOGO, wala hawakunielekezea nyuso zao; LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA SIMAMA, UTUOKOE.
Ndivyo ilivyo kwa watu wengi, wanamfanya Mungu kama mganga wa kienyeji, kwamba wanamtafuta tu nyakati za shida. Lakini hawataki kuwa na mahusiano naye, hawataki kumtii, hawataki kuacha uvaaji wao wa kikahaba, hawataki kuacha udunia.
Hawana muda wa kusoma Neno lake ili wajue mapenzi yake ni nini katika Maisha yao, mtu kumaliza hata dakika 20 kila siku katika kutafakari Neno la Mungu hawezi, kuomba kunamshinda, kwenda ibadani ni mara moja kwa mwezi, ikizidi sana mara mbili, na hata akienda ni ili Mungu amjibu lile ombi lake alilomuomba lakini sio kumwabudu katika Roho na Kweli.
Anachokiona kirahisi kwake, ni kwenda kununua maji ya upako na mafuta, ili amwage kwenye biashara zake, ili mambo yake yaende sawa.. Au pale anapopitia hali mbaya sana ya magonjwa ndipo anapomfuata Mungu ili amsaidie,. Hapo ndipo atafunga na kuomba, na kusoma Neno kila siku kwa bidii..Lakini siku nyingine zote anaishi maisha ya dhambi.
Ndugu, kama upo miongoni mwa kundi hili, hebu leo funguka kupitia ujumbe huu. Maana Mungu anakupenda ndio maana amekukutanisha na ujumbe huu.
Tuache sasa kumfanya Mungu awe sehemu ya kututatulia matatizo yetu tu, ili hali Maisha yetu hayaendani na wokovu. Tuanze sasa kumtafuta Mungu nyakati zote, tuhakikishe tunayatenda mapenzi yake, tuonyeshe bidii zetu kwake, kwamba tunampenda sio kiunafiki, bali kwa mioyo yetu kweli. Tunamtafuta sio atufanye kuwa mabilionea, bali atufanye kuwa wana wake kama Yesu Kristo. Na ndio sasa hata hayo mengine atasaidia bila hata kutumia nguvu wala kumwomba..
Kumbuka katika nyakati hizi za mwisho, watakaokwenda kwenye UNYAKUO, sio kila mtu asemaye ninamwamini Mungu tu, halafu basi,..Bali ni watu wayatendao mapenzi ya Mungu kikamilifu sawasawa na Neno la Kristo.
Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”
Maran atha (Bwana Yesu anarudi).
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.