MTU AKINITUMIKIA NA ANIFUATE

Biblia kwa kina No Comments

MTU AKINITUMIKIA NA ANIFUATE

Yohana 12:26 “Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu”.

Nakusalimu katika jina kuu lipitalo majina yote mbinguni na duniani, jina la YESU KRISTO WA NAZARETHI. Karibu tujifunze maneno yake ya uzima.

Watu wengi wanataka kumtumikia Bwana Yesu, lakini hawataki kumfuata. Wanataka wamtumikie na huku wanaendelea na mambo yao ya kando kando, wanaendelea na uasherarati wao, ulevi wao, uhuni wao, uvaaji wao wa kidunia, na mambo mengine yanayokinzana na mapenzi ya Mungu.

Lakini Bwana Yesu anasema mtu akitaka kunitumikia na anifuate, kwahiyo ukitaka kumtumikia kwa namna yoyote ile…huna budi kumfuata.

Utamfuataje?

Yeye mwenyewe alisema..

Mathayo 16:24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, MTU YE YOTE AKITAKA KUNIFUATA, NA AJIKANE MWENYEWE, AJITWIKE MSALABA WAKE, ANIFUATE”.

Umeona kanuni ya kumfuata YESU. Kama hujajikana nafsi bado hujamfuata na hivyo utumishi wako ni bure.

Sasa nini maana ya kujikana nafsi na kujitwika msalaba?

Kujikana ni kukataa mapenzi yako na kukubali kufuata yale ya Mungu, haijalishi yatakuwa hayakupendezi au hayakufai kwa wakati huo namna gani.

Pale ambapo, Mungu anataka ufanye hivi, na wewe unaona nafsi yako haitaki kukifanya, kwasababu moja au nyingine. sasa kule kutii cha Mungu na kukataa cha kwako huko ndiko kujikana nafsi.

Kwamfano Mungu anaposema wanawake wavae mavazi ya kujisitiri,(1Timotheo 2:9) na wewe ni mvaaji mzuri wa nguo zinazochora maungo na zile za kiume, sasa unapokubali kutii yale ya Mungu, ukaanza kuvaa magauni, bila kujali nafsi yako inakuambia utakuwa mshamba, au watu watakuambia hupendezi, huko ndiko kujikana nafsi.

Au pale Mungu anapokuambia, kiungo chako kimoja kikikukosea kikate, kuliko mwili mzima kutupwa jehanamu, na kama tunavyojua kiungo ni kitu kinachojishikamanisha na wewe. Na vitu vinavyojishikamanisha na maisha yetu ni vingi, vingine vizuri, vingine vibaya, sasa pale ambapo, pengine marafiki ulionao wanakukosesha, na kuchukua uamuzi wa kukata nao mazoea, na kuanza kutafuta marafiki wenye malengo na kimbingu na wewe, hapo ndipo umejikana nafsi.

Unapoacha, miziki ya kidunia, au kukesha kwenye muvi na kuchati kwenye mambo yasiyokuwa na maana, na kuutumia muda huo kumtafakari Mungu, au kumtafuta yeye, huko ndiko kujikana nafsi Bwana Yesu anakokuzungumzia.

Pia Kujitwika msalaba, ni ishara ya kukubali dhiki kwa ajili ya Kristo. Kumbuka msalaba ni kitu ambacho Yesu alikibeba na kwenda kusulubishwa kwa hicho. Sio kitu ambacho alikwenda kukilalia. Ni sawa na mtu leo hii akuambie jivike mabomu yako, uende sehemu ya kujilipua.

Hivyo na sisi ili tuwe wanafunzi wa Kristo kweli, na watumishi wake hatuna budi pia kukubali mashutumu na wakati mwingine kupitia dhiki kwa ajili ya jina lake. Hapo ndipo tutakuwa tumeonyesha tumeibeba misalaba yetu kweli kweli. Alama ya misumari yetu.

Hivyo jitathimini leo, je! umemfuata Yesu au unamtumikia tu!!. Unamsifu vizuri, unamtolea sadaka, unaposti maneno yake mitandaoni, unahuburi, unamtumikia kwa njia yoyote ile, kama hujamfuata fahamu kuwa kazi yako ni bure tu. Na siku ile Bwana alisema..

Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

[23]Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”. (Mathayo 7:21_23).

Amua sasa kuikana nafsi yako, acha udunia na tamaa zake na mfuate Bwana Yesu. Ndipo atatambua utumishi wako na Baba atakuheshimu.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *