
YONA NDANI YA MERIKEBU
Yona 1:5 “Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. LAKINI YONA ALIKUWA AMESHUKA HATA PANDE ZA NDANI ZA MERIKEBU; AKAJILAZA, AKAPATA USINGIZI”.
Yona alikuwa mmoja wa manabii wa Israeli wakati wa utawala wa Yeroboamu Mfalme wa Israeli, ambaye Mungu alimtumia sana kutoa unabii kadha wa kadha katika Israeli, kama tunavyomsoma katika (2Wafalme 14:21-25). Lakini ilifika wakati BWANA akataka kumtuma kwa watu wa Mataifa, Mji wa NINAWI uliokuwa mji mkuu wa Taifa la ASHURU ambalo kwa wakati ule lilikuwa ni moja ya ngome yenye nguvu duniani ndilo lililokuja baadaye kuhusika kuwachukua wana wa Israeli utumwani (2Wafalme 18:11),
Hivyo mji wa NINAWI uliokuwa mji mkuu katika Ashuru ulijaa maovu mengi sana, mfano wa Sodoma na Gomora, mpaka kufikia wakati Bwana kutaka kuuangamiza mji wote na watu wote waliokuwepo kule, lakini Mungu alivyo wa rehema hawezi kufanya jambo lolote kabla hajawaonya kwanza watu wake, ili pengine waghahiri uovu wao wasiangamizwe, na ndivyo alivyofanya kwa kumtuma YONA nabii katika mji ule Mkubwa uliokuwa mbali sana na taifa la Israeli.
Lakini tunasoma habari haikuwa hivyo kwa nabii YONA, badala ya kwenda NINAWI mji wa ASHURU alioagizwa na Bwana, yeye akaamua kuubuni mji wake yeye alioupenda ili akakae huko, ndipo akakimbilia TARSHISHI mji uliokuwa nchi ya Lebanoni ili tu AJIEPUSHE NA MAPENZI YA MUNGU.
Lakini alisahau kuwa ili afikie malengo yake hana budi kupitia “NJIA YA BAHARI”.. Hivyo akaamua kupanda Merikebu zinazoelekea Tarshishi, Na kama tunavyosoma habari alipokuwa katikati ya safari yake bahari ilichafuka na mambo yakaanza kuharibika.
Bwana aliyaruhusu yote haya yampate YONA ili kutuonya sisi kwamba tusipotaka kuenda katika njia ambayo Mungu kaikusudia tuiendee, yatatukuta kama hayo hayo. Kama biblia inavyosema
1Wakoritho 10: 11 “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ILI KUTUONYA SISI, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.”
LAKINI SWALI NI JE! NJIA YA BAHARI NI SALAMA ALIYOICHAGUA YONA?
Kibiblia BAHARI inawakilisha nini?…Ili kufahamu jambo hili ni vizuri tujue ni kitu gani kimo humo ndani yake .tukisoma.
Ufunuo 13: 1 “KISHA NIKAONA MNYAMA AKITOKA KATIKA BAHARI, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru.
2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.”
Unaona hapo?.
Kumbuka YONA anawakilisha kundi la wakristo wasiotaka kudumu katika mapenzi ya Mungu (yaani VUGUVUGU).leo wanaenda na Mungu, kesho wanaenda katika akili zao, leo anafanya ibada kesho anakula rushwa. N.k. Sasa Kama vile nabii YONA alivyokimbia uso wa Mungu na kuelekea njia ya BAHARINI na hatimaye kumezwa na yule SAMAKI MKUBWA, vivyo hivyo na kundi hili la wakristo wasiotaka kutengeneza mambo yao sasa vizuri na Mungu, hawajui kama wanakimbilia baharini pasipo wao kujua, ambapo kule kuna Yule mnyama mwenye vichwa saba na pembe kumbi ameandaliwa kuwameza.

Na bahari inawakilisha nini?
Tukirudi kusoma Ufunuo 17: 15 Kisha akaniambia, YALE MAJI ULIYOYAONA, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha.” Kumbuka huyu kahaba anayezungumziwa hapa ameketi juu ya Yule mnyama aliyetoka baharini ambaye tumemsoma katika Ufunuo 13.
Kwahiyo bahari au maji mengi inawakilisha mahali penye mkusanyiko wa watu wengi, hivyo Yule mnyama anatoka mahali penye mkusanyiko wa watu wengi, mahali ambapo amekubaliwa na wengi, tukizungumza katika roho leo hii mfumo wa mpinga-kristo unatenda kazi katikati ya mataifa, na dini nyingi za uongo.
Kama vile Yona alivyoiacha njia ya Mungu na kuchagua Njia ya BAHARI akidhani kuwa ni salama, vivyo hivyo na wakristo wa leo walio vuguvugu, wanamsahau Mungu na kushikimana na mambo maovu ya ulimwengu huu, nabii Yona ALISINZIA pale alipoona kuna utulivu mwanzoni mwa safari yake, kadhalika kundi hili la wakristo vuguvugu wanasinzia kwasababu wanajiona wapo salama, wanaona hata wakifanya hivyo hakuna dhara lolote wanatakalolipata lakini hawajui kuwa kuna mnyama ameshaandaliwa kwa ajili yao chini ya Merikebu yao. Pale PEPO zitakapovuma ndipo watakapotambua kwamba hawapo salama, wakati huo unyakuo umeshapita, ndugu unajiona upo salama katika ulimwengu, hata ukitenda dhambi unaona hakuna dhara lolote linalokupata, angali unafahamu kabisa moyoni mwako umeukimbia uso wa Mungu na unayoyafanya sio sahihi na bado unajiita Mkristo, hujui kwamba ni NEEMA ya Mungu tu, imekushikilia dhidi ya Yule Mnyama utubu, ugeuze njia uepuke madhara yaliyopo mbeleni ambayo yapo karibuni kuupata ulimwengu mzima. Ipo siku NEEMA inayokushikilia itakwisha na moja ya siku hizi PEPO ZITAANZA KUVUMA BAHARINI. Kama biblia inavyosema katika..
Danieli 7: 1 “Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danieli aliona ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo.
2 Danieli akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, HIZO PEPO NNE ZA MBINGUNI ZILIVUMA KWA NGUVU JUU YA BAHARI KUBWA.
3 Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali”………
Wanyama hao Nabii Danieli alionyeshwa, watatu wa kwanza walishapita na Yule wa mwisho wanne, ndiye aliyeko sasa chini ya MERIKEBU(NEEMA), na moja ya hizi siku pepo zitamwamsha kutenda kazi.
Hichi kipindi kipo karibuni kutokea, Yule mnyama sasa anatenda kazi katika siri na watu wa Mungu wanasinzia hawaoni kuwa wapo katika hatari, wanadanganyika na utulivu uliopo sasa hivi kama vile nabii Yona alivyodhani lakini biblia inasema
1Wathesalonike 5: 2 “Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile MWIVI ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa”.
Ndugu usileweshwe na ulevi wa hii dunia hata kulala usingizi, Bwana yupo karibu kulichukua kanisa lake BIBI-ARUSI WA KWELI anayedumu katika Neno lake na UTAKATIFU, Na hatua za unyakuo zimeshaanza Bwana anawakusanya watu wake toka kila mahali, watu ambao macho yao yapo mbinguni, duniani wao ni kama wapitaji tu, hao ndio watakaofunuliwa siri za unyakuo lakini wengine wote ikiwemo wakristo vuguvugu, hawatajua lolote isipokuwa kumtazamia Yule mpinga-kristo mnyama atokaye baharini. Utajisikiaje siku ile wenzako wapo mbinguni kwenye KARAMU YA MWANA-KONDOO na wewe upo katika dhiki kuu na zaidi ya yote watakuja kutawala na Kristo milele na milele kama wafalme na makuhani wa Mungu na wewe upo kwenye ziwa la moto??. Ni vizuri utengeneze mambo yako sasa hivi kabla siku ile haijafika. Tubu ukabatizwe kwa Jina la BWANA YESU upate ondoleo la dhambi zako na uanze kuishia wokovu..
Mungu akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.