
JE UNAJUA NI NINI KITATOKEA MUDA MFUPI BAADA YA UNYAKUO?
Bwana Yesu Kristo asifiwe. Karibu tujikumbushe mambo ya msingi yatupasayo kufahamu katika nyakati hizi za hatari..
Baada ya Unyakuo kupita maisha yataendelea kama kawaida, lakini kutasikika tetesi tesi kuwa kuna watu wanaripotiwa kupotea katika mazingira yakutatanisha.
Hakutakuwa na furugu kama inavyojulikana na wengi kuwa unyakuo utakuwa ni tendo la ghafla. kufumba na kufumbua mamilioni ya watu watatoweka, watu watakuwa wakikimbia mabarabarani, ulimwengu mzima utataharuki, ndege zitaanguka, ajali nyingi zitatokea duniani, amani itapotea ghafla na watu watakuwa wakilia na kuomboleza, wakimwona mpinga kristo akipanda kutoka kuzimu kuleta uharibifu duniani kote.
Ndugu haitakuwa hivyo, kulingana na biblia unyakuo utakuwa ni siri, hakutatokea vurugu wala ajali mabarabarani, kama kukitokea vurugu mpinga-kristo atafanyaje kazi sasa hapo?.
Na nani atashawishika kupokea chapa ya mnyama?
Ni dhahiri kuwa hakuna atakayeshawishika kwasababu watu wote watamjua mpinga-kristo amefika, na unyakuo hapo utakuwaje wa siri tena?? lakini siku hiyo wengi hawatamjua mpinga-kristo wala chapa yake kwasababu hatakuja akiwa na mapembe, atakuwa ni mtu anayeheshimika, na kukubalika na dunia, atakuja na kivuli cha amani, na atapendwa na wengi, na atakuwa mtu wa kidini, na anashika biblia, lakini ndani yake ni utendaji kazi wa shetani wenyewe, atawadanganya wengi waipokee ile chapa, na ni muhimu pia kufahamu namba 666 sio chapa ya mnyama, hilo ni jina la mnyama na sio chapa yake, chapa yake ni kitu kingine kabisa.
Ikiwa namba 666 ndio chapa yake, watu wengi pia siku hiyo wataikataa, lakini siku hiyo mamilioni ya watu wataipokea kwasababu hawataijua, Hivyo ni kuwa makini sana na hizi nyakati.
Bwana Yesu alisema siku ya kuja kwake, inafanana na siku zile za Nuhu, Siku zile mpaka Nuhu anaingia kwenye Safina hakuna mtu yeyote alitambua kuwa tayari Mungu ameshaihukumu dunia.. mpaka zikapita siku saba, nyingine ndipo mvua ya gharika ikashuka kwenye dunia.,
Mathayo 24:38 “Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,
39 WASITAMBUE, HATA GHARIKA IKAJA, IKAWACHUKUA WOTE, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
40 Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa
41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu”.
Unaona? Leo hii, kama wewe sio “bibi-arusi” wa kweli wa Kristo, nikimaanisha, kama sio mkisto aliyesimama katika wokovu kweli kweli, usitazamie utatambua lolote siku Kristo anarudi kuwanyakua watakatifu wake. Kwasababu hata Bibi-arusi wake mwenyewe hatojua siku hiyo itakavyokuwa sembuse wewe?..
Na ndio maana aliwaambia mpaka na wateule wake, kwamba wajiweke tayari, waifanye kazi yake, watimize wajibu wao walioitwa hapa duniani wa kuitangaza injili yake, kwasababu saa wasiodhani ndio atakayokuja.
Hakuna mtu atakayeitambua siku hiyo, itakuja ghafla tu bila hodi, hakuna dalili yoyote itakayotutambulisha, itakuwa kama tu ilivyo leo, au jana, wakati ambapo watu wanapanga mipango yao ya kimaisha, wanalijenga taifa lao, wanauza pombe, na kufanya biashara hapo hapo, Unyakuo unapita , mmoja anatwaliwa mmoja anaachwa..
Watu wengi sana wataingiwa na butwaa, wakisema mbona Bwana hakutupa taarifa au kiashirio fulani, mbona, angani hakukuonekana chochote, mbona tulitazamia jambo Fulani kwanza tulione, ndio unyakuo upite, imekuwaje, amesharudi, wakati watu wengine hawajahubiriwa bado injili. Lakini ndio hivyo tayari watakatifu wameshaondolewa.
Na watakaofahamu na kusadiki ni wale wanawali wapumbavu ambao walikuwa wanajua kuwa Bwana anarudi na wameona dalili zote lakini hakuwa makini kujiweka tayari…watu wengine wa mataifa (wasioamini) hawatasadiki jambo hili kwakuwa hawakuwahi hata kusikia kuwa kuna tukio kama hili linakuja..
Wao watakuwa wakwanza kukubaliana na mfumo wa monga Kristo (yaani chapa yake) kwasababu baada ya watu wachache kutoweka katika mazingira yakutatanisha… dunia itadanganywa kuwa ni mambo ya kisayansi tu au ni viumbe kutoka katika sayari za mbali (allens) wamehusika kuwatowesha watu na watu wataamini, hivyo maisha yataendelea kama kawaida.
Hivyo ndugu, wakati huo upo karibu sana..ridhika na dalili tunazoziona, kwasababu hakutakuwa na nyingine Zaidi ya hizo zilizoandikwa kwenye biblia. Usidhani malaika atatokea hapo mawinguni kutuhubiria injili kwamba kesho Yesu ndio anarudi.
Kama utakosa unyakuo, basi ujue, utakuwa katika majuto na vilio na kusaga meno kusikokuwa kwa kawaida. Majuto hayo, unaweza ukayaona sio kitu leo kwasababu bado hayajakukuta, lakini subiri siku hiyo ikufikie, hutatamani uishi. Hicho kiburi cha uzima ulichonacho leo, siku hiyo kitayeyuka chote, utamtafuta Mungu hutamwona. Utalia hakuna atakayekusikia, makanisa yatakuwa hayana faida yoyote kwako. Hakuna chochote kitakuwa na maana kwako, kwasababu hata pesa hazitafanya kazi wakati huo.
Ndugu, ndani ya hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho bado unayo nafasi ndogo sana ya kutubu, Tubu leo kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako, na Kristo atakupokea, kumbuka muda tuliobakiwa nacho ni mfupi sana, kulingana na dalili zilizotabiriwa unyakuo utatokea muda wowote kwani dalili zote zimekwisha timia mpaka sasa… hivyo huu sio wakati wa kukimbizana na mambo ya dunia na kubweteka..ni wakati wa kujihakikisha umepokea wokovu wa kweli. Na wakovu wa kweli ni ule kuishi maisha ya utakatifu na kuongozwa na Roho Mtakatifu kila siku, na hili linawezekana tu baada ya mtu kuamua kuikana nafsi yake nakuchukua msalaba na kumfuata Yesu kwa gharama zote
Bwana Yesu atusaidie
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.