Jina la Bwana Yesu libarikiwe. Karibu tujifunze maneno ya Mungu yenye uzima.
Tusome…
Isaya 29:16 Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyazi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichomfinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?
Bila shaka kama we ni msomaji wa biblia naamini si mara ya kwanza kukutana na andiko hili, ila leo nataka tukaangalie tena kwa sura nyingine Roho Mtakatifu atusaidie kulielewa zaidi ya tunavyofahamu,
Bwana anaanza hapo kwa kusema NINYI MNAPINDUA MAMBO, Je! umewahi kufikiri kwamba ni mambo gani hayo ambayo sisi tunapindua? Kama ukisoma andiko lote utagundua kuwa Mungu analenga kuhusu uumbaji wake, ndio maana anajifananisha na Mfinyazi na sisi tunafananishwa na udongo, Mwanzoni nilikuwa nikisoma hilo andiko nilikuwa nachukulia tu kawaida japo nilikuwa nalielewa kwa kiasi fulani, ila Bwana alipokuja kunielewesha zaidi nipolielewa niliogopa sana…
Kwani Bwana anaongelea jambo ambalo linafanyika hususani katika hiki kizazi chetu, na wewe leo Bwana akupe neema upate kuelewa andiko hili na uone namna watu walivyopindua uumbaji wa Mungu na jinsi Bwana anapoonyesha hisia kali kuhusu jambo hilo, hebu rudia rudia kusoma hilo andiko huku ukitafakari, usisome tu juu juu kimazoea kwamba uliwahi kusoma,
Bwana anauliza, Je! Mfinyazi ahesabiwe kuwa kama udongo;
Maana yake mtu anapobadilisha ule mwonekano wake ambao Mungu alimuumbia, labda ni ngozi yake, nywele zake, kucha zake, na viungo vingine alivyopewa na Mungu, halafu yeye akaenda kugeuza na kuumba kwa mwonekano mwingine kwa lengo la kutafuta uzuri, au lengo lolote atakalokusudia… tafsiri yake ni kumfanya Mungu awe kama udongo na mwanadamu kuwa Mungu,
kwamba mwanadamu sasa ndiye awe mfinyazi na Mungu awe ni udongo! Hebu tafakari hilo jambo vizuri, Ndio hapo sasa Mungu anaendelea kuuliza…
“….kitu kilichomfinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?
Dada, mama, we ambaye umepindua uumbaji wa Mungu kwa kigezo tu cha kutafuta kuonekana na wanadamu wenzako, kwa kigezo tu cha kutafuta kukubaliwa na wanaume, kwa sababu ya kutaka kuonekana mrembo, na sababu zingine unazosijua wewe, hebu leo tafakari mara mbili mbili tena na ujue kabisa Mungu hafurahishwi na hayo mapambo,
Mungu hafurahishwi kabisa na hizo hereni masikioni mwako, Mungu hafurahishwi na hiyo rangi uliyoweka kwenye kucha, hizo vipodozi unazotumia kubadilisha rangi ya ngozi yako Mungu hazifurahishwi, hizo lipustick, wanja, na hizo nywele za bandia unazotumia kuweka kwenye mwili wako Mungu hazifurahii, chochote kile ambacho unajitia kwenye mwili wako na kubadilisha mwonekano wako Mungu alivyokuumbia aiza kwa kuongeza au kupunguza…
fahamu kuwa unamchukiza Mungu sana, kwani ni sawa na kumfanya yeye kuwa udongo, halafu wewe uwe Mfinyazi, ni sawa nakumwambia Mungu kuwa huna ufahamu, hujui kuumba, huna lolote, ulitakiwa kuniumba hivi na hivi, ulitakiwa uniumbie ngozi nyeupe, kucha nyekundu, nywele ya rangi hii, ulitakiwa uniumbie na hereni masikioni mwangu ili nipendeze maana nikiwa sina hereni sijapendeza, ulitakiwa uniumbe na mdomo mwekundu, n.k,
Kwahiyo kazi yako ina kasoro nyingi, uumbaji wako haujakamilika, wewe hujui kuumba ipasavyo, ngoja nikuoneshe namna ya kuumba, yaani ni kumtukana Mungu kabisa na kumdhihaki na Neno la Mungu linasema “Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna(Wagalatia6:7).
Siku hizi za mwisho watu wanadanganyika kwa elimu ya shetani inayosema Mungu haangalii mwili bali anaangalia roho, wengine wamedanganywa na kuambiwa tunaishi katika neema na tumekombolewa na Yesu, ni kweli tumekombolewa na damu ya Yesu msalabani, ila unachopaswa kuelewa ni kuwa Kristo alikuja kutukomboa na kututoa kwenye utumwa wa dhambi ambao unasababishwa na tamaa za mwili, hebu tusome maandiko haya..
Warumi 8:1 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.
2 Kwa sababu sheria ya Roho ya uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.
3 Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili;
4 ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.
5 Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho.
6 KWA KUWA NIA YA MWILI NI MAUTI; BALI NIA YA ROHO NI UZIMA NA AMANI.
7 KWA KUWA ILE NIA YA MWILI NI UADUI JUU YA MUNGU, KWA MAANA HAITII SHERIA YA MUNGU, WALA HAIWEZI KUITII.
8 WALE WAUFUATAO MWILI HAWAWEZI KUMPENDEZA MUNGU.
9 Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.”
Neno la Mungu linasema hapo katika mstari wa mwisho “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho…..”
Kwanini leo hii biblia inakuambia “kujipamba kwako, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;
4 bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole, na utulivu iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. (1Petro3:3)
na tena Mungu anazidi kuliwekea msisitizo neno hili katika ”1Timotheo2:9-10″ kuwa mwanamke hapaswi kujipamba kwa nje, yaani kusuka nywele, kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi ya thamani, Lakini utaona mtu pamoja na kusoma au kuambiwa hilo andiko bado hataki kuachana na mapambo ya mwili, bado hataki kuacha kusuka, bado hataki kuvaa hereni, mikufu, na kupamba uso kwa mekaup, kutia wanja, kuweka rangi mdomoni (lipustick), kwenye kucha, n.k, unadhani ni kwanini anakuwa mguu kutii hilo neno la Mungu?
Kwanini anabaki tu kujitetea kwamba Mungu anaangali roho, na andiko limesema ”kujipamba kwenu, kusiwe kwa nje..” na sio kujipamba kwenu kusiwe kwa roho. Jibu tunalipata hapo tukirudi kwenye andiko hilo la Warumi 8:9 linasema..
“Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho…”
Kwahiyo tatizo la kukataa kitii maagizo ya Mungu, kukataa kuacha kuweka mapambo kwenye mwili wako ambao utapelekea kupindua uumbaji wa Mungu, na kukosoa kazi ya Mungu, hili tatizo ni kwasababu ya kukosa Roho wa Mungu ambaye angekuongoza ili usifuate mwili, kwasababu mwisho wa kufuata mwili ni mauti,
na ukija kuangalia sababu ya kutaka kujipamba ni nini? Ni kutafuta tu uzuri zaidi ya huo aliokupa Mungu, leo hii ukiambiwa kwanini unajitia hayo mapambo kwenye mwili wako na biblia imekukataza, ni wazi kuwa unatafuta uzuri, kupendezesha mwili, uonekane kuwa unapendeza, watu wakusifie kwasababu ya urembo huo wa bandia, unatamani kuonekana na watu,
kwasababu ukweli macho ya wanadamu yanatazama nje, ili wakusifie, wauone uzuri wako watatazama jinsi unanyoonekana kwa nje, hawawezi kuona roho yako halafu wakuambie umependeza, au wakuone we ni mzuri, Kwahiyo ili uwaridhishe inakubidi ujipambe kwa nje ili wakuone, utie huo mkorogo, upake hiyo rangi, usuke, utoboe sikio lako na uweke hizo hereni, n.k,
kusudi tu uonekane na wanadamu wenzako, unaweza ukajitetea kuwa hautafuti kuonekana na watu ila unataka tu ujiweke mzuri, upendeze, na pia yamkini na ukasema kwani Mungu hataki nipendeze! Kwani kupendeza kuna shida gani, kuvaa tu hereni kuna tatizo gani, kusuka tu kuna shida gani, maadamu tu namwanini Yesu siendi kufanya uasherati, usengenyaji, situkani, siibi, n.k, ila bado hiyo sio sababu ya kuhalalisha mapenzi yako, na kutupilia mbali maagizo ya Mungu, ukija na sababu yeyote ile bado tu tutarudi kwenye neno la Mungu kuwa “KUJIPAMBA KWENU KUSIWE KWA NJE,..”
Na hilo ni agizo halina mjadala, wewe ambaye hutaki kutii haijalishi utajiteteaje! utatafuta maandiko kadha wa kadha, utakuja na sababu zako, utasema namwanini Yesu, na huwa ananijibu nikiomba, huwa anasema nami, huwa naonaga maono, Mimi naimbaga kwaya, nahudhuria kanisani kila week, natoa sadaka zote, nawahurumia maskini, yatima, nashuhudia habari za Yesu,
nafanya hiki na kile, ila bado haibatilishi agizo la Mungu, Mungu anakataza mapambo kwa wanawake wa Kikristo, labda uchague kuungana na wanawake wa kidunia ambao wamepindua kabisa uumbaji wa Mungu, kama hutaki kuacha kujipamba, hutaki kuacha kusuka, kuvaa hereni, wigi, kutumia mekaup n.k, ni vyema tu ukaungane na hao wa kidunia na huku ukijua kuwa ziwa la moto lipo tayari kwa wote waliomdhihaki Mungu na kupindua uumbaji wake.
Ila kama utabaki kujiita mkristo na hutaki kuishi kulingana na neno la Mungu fahamu kuwa unajidanganya mwenyewe, unasema we ni mkristo na huku hauna tofauti na watu wa kidunia unajidanganya, huo sio ukiristo, ukiristo ni kutembea na Roho wa Kristo, kuliishi Neno, kutii na kupenda maagizo yote ya Mungu, hivyo we ambaye bado unasema ni mkristo na huku hutaki kutii maagizo ya Mungu, hupendezwi na maagizo ya Mungu, unataka kuishi vile unavyotaka, hauna tofauti na watu wa kidunia wasiotaka kujua kuwa kuna Mungu aliyewaumba,
Nakushauri dada yangu, mama utubu kwa kumaanisha kabisa, achana na hiyo fikira yako ya kusema Mungu anaangali roho tu, amua kubadili mtazamo wako usije ukapotea, Mungu anaangali roho kweli kwa mtazamo wako ila haangalii roho chafu, usiangailie wingi wa watu wanaojihita wakristo na huku wameacha neno la Mungu, usiangailie kabisa mtu yeyote, usiangailie hata mchungaji wako, Askofu wako, usiangailie kanisa lako, dhehebu lako, angalia Neno la Mungu na ulifuate, sasa umejua ukweli yamkini ulikuwa hujui, chukua sasa hatua ya kutubu kwa kuondoa mapambo yote ndani ya mwili wako, tupa kabisa au choma moto, ili usivirudie tena kuviweka kwenye mwili wako, kama umesuka fumua haraka, baki katika uasili wako(natural) vile Mungu alikuumba
Fahamu kuwa si Kwamba Mungu hataki upendeze, ila tayari Mungu amekuumba ukiwa mzuri, vile ulivyo ndio unapendeza, Kwahiyo ukiweka vitu vingine kwenye mwili wako ili kutaka kupendeza zaidi ya hapo maana yake unakosoa uumbaji wa Mungu kwamba haujakamilika, usifanye hivyo maana ni hatari sana kwa roho yako, maanisha sasa kutubu na Mungu ni wa rehema atakupokea, baada ya kutubu nenda katafute ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa JINA LA BWANA YESU ili upokee Roho Mtakatifu sawa sawa na Neno la Mungu katika (Matendo 2:38)
Ambaye huyo Roho wa Mungu atakusaidia kushinda dhambi na tamaa zote za mwili, na kuishi katika mapenzi ya Mungu (utakatifu), na wewe ambaye bado hujampokea Bwana Yesu na unaishi maisha unayoyataka, tambua kuwa bado Mungu anakuhitaji, mgeukie sasa Muumba wako kabla siku zilizo mbaya hazijakufikia, kabla mwili wako haujatenganishwa na roho yako, mwili wako kurudi mavumbini na roho yako kumrudia Mungu aliyeitoa sawa sawa na (Mhubiri12:1-7),
Tambua kuwa huo mwili wako ambao unajifurahisha nayo katika starehe na anasa za kidunia, fahamu leo kuwa hiyo ni nyumba ya Mungu, fahamu kuwa mwili wako ni hekalu la Mungu.. maandiko yanasema hivyo,
1Wakorintho3:16 Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
Umeona hapo anasema hekalu la Mungu ambalo ndio huo mwili wako ni takatifu, na anasema mtu akiliharibu hekalu la Mungu Mungu atamharibu mtu huyo.(kwenye ziwa la moto) ukisoma pia sura ya 6 katika hicho hicho kitabu cha Wakoritho, Mungu anasema..
1Wakoritho6:19 Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;
Unaona hapo, anasema ninyi si mali yenu wenyewe, maana yake mwili wako sio mali yako tu pekee yako, yupo aliyeumba huo mwili, na hata sasa anaumba, ndio maana leo ukikata kucha zako baada ya siku kadhaa zitaota tena, ukinyoa nywele zinaota tena baada ya muda, yupo aliyekutengeneza ndiye Mungu aliyekuumba na anayeendelea kukuumba leo
Na hivyo unapaswa umkumbuke na umgeukie ufanye mapenzi yake ambayo ni kuishi katika utakatifu (1Wathesalonike 4:3 Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mweupukane na uasherati; 4 kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;)
Yamkini umegeuza nyumba ya Mungu (mwili wako)kuwa nyumba ya biashara ya kupatia kipato pale unapojiuza ili upate kushibisha nafsi yako, kuwa nyumba ya makahaba pale unapotembeza uchi kwa kuvalia mavazi ya kikahaba (suruali, vimini n.k)
unapofanya huo uasherati, unapofanya huo usagaji, unapoweka kila aina ya rangi, vilevile umegeuza kuwa bar pale unaponywesha hizo vilevi, na kila aina ya uchafu, sasa kumbuka Mungu alishasema mtu akiliharibu hekalu lake (mwili wake) na yeye atamharibu mtu huyo.. mgeukie Muumba wako kabla hujaenda kuangukia katika hukumu ya Mungu, kuzimu ipo, ziwa la moto lipo, dhamiria kutoa mwili wako iwe dhabihu iliyo hai takatifu, na ya kumpendeza Mungu…”
Warumi 12:1 Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndio ibada yenu yenye maana.
2 Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.
Matendo 2:37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na Mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
Mgeukie Bwana Yesu.
Bwana akusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.