USISHIKAMANE NA BINTI ZA MATAIFA

Biblia kwa kina No Comments

USISHIKAMANE NA BINTI ZA MATAIFA

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia kwa pamoja.

Tukisoma biblia, kipindi Isaka anambariki Esau, baada ya kumbariki alimwagiza asitwae mke kati ya binti za Kanaani, bali aende huko Padan-aramu akajipatie mke katika nyumba ya Labani ndugu wa mama yake. Tunasoma..

Mwanzo 28:1 “Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani.

[2]Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako.

[3]Na Mungu Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mkutano wa makabila.

[4]Akupe mbaraka wa Ibrahimu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, Mungu aliyompa Ibrahimu.

[5]Basi Isaka akampeleka Yakobo, naye akaenda Padan-aramu, kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mshami, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau”.

Sasa, tukiendelea kusoma tunaona Yakobo alimtii baba yake Isaka na akafunga safari kuelekea Padan-aramu na kama tunavyojua ile safari Mungu alimfanikisha, na baadaye alikuja kuwapata Lea na Raheli, lakini tukirudi kwa Esau, yeye tayari alikuwa ameoa wake kati ya wale binti za kimataifa, lakini tunasoma Isaka hakupendezwa na hao binti za Kanaani.

Mwanzo 28:6 Esau akaona ya kwamba Isaka amembariki Yakobo na kumpeleka Padan-aramu, ili ajitwalie mke huko, na katika kumbariki akamwagiza, akasema, Usitwae mke wa binti za Kanaani,

[7]na ya kuwa Yakobo amewatii babaye na mamaye, akaenda Padan-aramu.

[8]Esau akaona ya kuwa binti za Kanaani hawakumpendeza Isaka, baba yake.

[9]Basi Esau akaenda kwa Ishmaeli akamtwaa Mahalathi, binti Ishmaeli mwana wa Ibrahimu, ndugu wa Nebayothi, kuwa mkewe pamoja na wakeze aliokuwa nao.

Na jambo hilo halikumpendeza tu Isaka peke yake, bali pia na Rebeka mamaye hakufurahishwa na jambo hilo la Esau kuoa binti za kimataifa.

Mwanzo 27:46 Rebeka akamwambia Isaka, Rohoni mwangu sina raha kwa sababu ya hao binti za Hethi. Kama Yakobo akitwaa mke katika binti za Hethi, kama hawa BINTI ZA NCHI, maisha yangu yatanifaidia nini?

Ni nini tunajifunza hapo?

Binti za kimataifa mpaka leo wapo, na sisi kama watoto wa Mungu, Baba yetu hapendezwi na sisi kushikamana na hao binti za nchi.

Binti za nchi ni madhehebu yote pamoja na dini za kipagani. Hatupaswi kushikamana nao kabisa..kwa maana hakuna ushirika kati yetu na sisi, hivyo Mungu wetu anatuambia tutoke kati yao tukajitenge ili tuwe salama.

Ufunuo wa Yohana 18:1 Baada ya hayo naliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake.

[2]Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza;

[3]kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake.

[4]Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.

[5]Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake.

Huyo Babeli mkuu anayezungumziwa hapo ni yule mama wa makahaba ambaye amezungumziwa pia katika..

Ufunuo 17:1 Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi;

[2]ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake.

[3]Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.

[4]Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.

[5]Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI.

Sasa, huyu kahaba mkuu..biblia inamuita MAMA WA MAKAHABA, ikimaanisha anayo mabinti ambayo wao nao wanafanya ukahaba kama mama yao. Hao ndio binti za nchi ambayo hatupaswi kushikamana nao, (yaani madhehebu yote) ili wasituchafue kama Dina alivyoshikamana nao na mwisho wake naye akafanywa kama kahaba.

Mwanzo 34:1 Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi.

[2]Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri.

Biblia imetuonya katika hichi kipindi cha mwisho tujitenge na ile dini ya Babeli, Mungu ametuita kuwa bikira safi, na ni bikira safi tu asiye na mawaa ndiye atakayeingia katika karamu ya mwanakondoo, Wakristo wengi sasa tunasema sisi ni wakristo lakini sio ukristo halisi wa kwenye biblia ambao ulihubiriwa na mitume, lakini ukristo uliopo sasa ni madhehebu, embu tujiulize je! Kristo amegawanyika, au Bwana Yesu akirudi leo atachukua dhehebu gani aliache dhehebu gani? kwahiyo ni wazi kabisa kuwa udhehebu sio ukristo, maana palipo na madhehebu pana mapungufu, lakini ukristo hauna mapungufu. Kwahiyo unapoacha kuwa mkristo sawa sawa na maandiko na kujifungia na kufuata miiko au taratibu za dhehebu fulani, hata kama haviendani na maandiko, na kuweka neno la Mungu kando kama taa yako ya kukuongoza hapa duniani, huko ndiko kufanya ukahaba/ uasherati wa kiroho kwa maana ingekupasa kulifanya lililo sahihi lakini ukageukia mafundisho mengine, Hivyo basi madhehebu yote Mungu ameyahukumu, na ndiyo yaliyoibeba ile chapa ya mnyama ndani yake. Na ujumbe wa sasa kwa wakristo wote ni huu. “Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake”,  

Unapousikia ujumbe huu, ufanye hima utoke, na sio utoke kwa miguu au ubadilishe kanisa, hapana bali utoke kwa kuutafuta ukweli na kuoana na neno la Mungu, ujazwe Roho wa Mungu. na Roho ndiye atakayekuongoza katika kuijua kweli yote, sio dhehebu wala shirika lolote la dini wala kanisa, tafuta uhusiano wako binafsi na Yesu Kristo na ndipo utakapokuwa bikira safi.

TAFUTA ROHO MTAKATIFU, EPUKA KAMBA NA UTAMBULISHO WA MADHEHEBU.

Ukiulizwa wewe ni dhehebu gani, sema mimi ni mkristo usione haya Bwana Yesu alisema katika marko 8:38″Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”. Uvae ukristo umfuate Yesu usiuvae udhehebu utakupeleka jehanum.

Hebu jifikirie tangu upo katika dhehebu lako umejifunza kuhusu kumjua Yesu kiasi gani?..unamjua Mungu kiasi gani,Neno unalifahamu na umelishika kiasi gani?..je umekuwa mtakatifu kiasi gani?..una uhakika kwa kiasi gani kwenda mbinguni?..Je umeshawahi kutenga muda mwenyewe pasipo kuambiwa kusoma maandiko?, au kusali au kwenda kuwahubiria wengine habari njema…

Kama hujawahi kufanya hayo na zaidi ya hayo na bado unajiisifia dhehebu…tenga muda ujitafakari tena ndugu yangu…Usijisifie dhehebu, Rudi katika Neno la Mungu ambalo ndio katiba yetu. Unyakuo umekaribia sana, Kristo anakaribia kuja na Mpinga-Kristo kashatengeneza mazingira yake yote ya kufanya kazi zake.

Mungu akubariki!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Na Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *