
Tunapataje ondoleo la dhambi?
Karibu tujifunze biblia.
Swali: Naomba kufahamu hatua ya kupata ondoleo la dhambi maishani mwangu.
Swali nzuri sana. Biblia imetoa kanuni ya kupata ondoleo la dhambi ambayo tunaisoma katika..
Matendo ya Mitume 2:38 “Petro akawaambia, TUBUNI, MKABATIZWE kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, MPATE ONDOLEO LA DHAMBI ZENU, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
[39]Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.”
Umeona hapo, kanuni ni KUTUBU na KUBATIZWA KWA JINA LA YESU KRISTO.
Sasa nini maana ya kutubu?
Tofauti na inavyodhaniwa na wengi kuwa kutubu ni kuomba msamaha, lakini kiuhalisia kuomba msamaha kunakuja baada ya kutubu.
Kutubu maana yake ni “Kugeuka” yaani kuacha kile ulichokuwa unakifanya.
Maana yake unapojigundua kuwa wewe ni mkosaji, jambo la kwanza ni “Kuacha kile ulichokuwa unakifanya” kisichokuwa sawa. Kisha ndipo unakwenda kuomba msamaha.
Hakuna mtu anayekwenda kuomba msamaha kabla hajaacha kile alichokuwa anakifanya.
Umemwibia mtu, au boss wako, je unaweza kwenda kumwomba msamaha huku bado unamwibia?
Jibu ni la!. Cha kwanza utakachokifanya ni kuacha kwanza wizi, kisha ndipo unakwenda kumwomba Msamaha. Maana yake matendo yako ndiyo yatakayoelezea kama umetubu kweli au la!, Na si maneno.
Na kwa Mungu ni hivyo hivyo, haangalii wingi wa maneno yetu, wala wingi wa machozi yetu, wala wingi wa majuto yetu, bali wingi wa Matendo yetu!.
Kwa Mungu “Matendo” ni Alama kubwa sana kuliko hata “Maombi”. Mtu anayetenda sana ni rahisi kufanikiwa zaidi na yule anayeomba sana bila kutenda.
Yakobo 2:17 “Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake”.
Kadhalika na Toba ni matendo si maneno.
Leo kuna watu wengi wanaoshindwa na dhambi, ambao hawawezi kuacha ulevi, uzinzi, kujichua, kuiba, kusengenya n.k. Na hawajui tatizo ni nini?.
Tatizo ndio hilo, walitangulia kuomba msamaha kabla ya kuamua kuacha matendo yao.
Kwahiyo kama leo unataka kupata ondoleo la dhambi zako, basi hatua ya kwanza ni wewe kuamua kuacha hizo dhambi kwa vitendo.
Maana yake kama ni ulevi unaacha kwa akili zako, kama ni uzinzi ni vivyo hivyo unaamua kuacha mara moja, unafuta namba zote za watu unaofanyanao uzinzi na unawaambia umeokoka, unafuta picha zote chafu na miziki za kidunia kwenye simu yako, unaacha kuvaa mavazi ya kihuni na kikahaba kama modo, crazy, vimini, suruali kwa mwanamke, na zile zinaonyesha maungo yako kuanzia juu mpaka chini na mapambo yote ya kidunia kama hereni, vipini, lipustiks, wanja, nywele bandia, kucha bandia, rangi ya kucha, unaamua kuchoma moto bila kujihurumia. Na dhambi zote UNAACHA kwa vitendo.

Baada ya hapo, hatua ya pili unaenda kubatizwa kwa kuzamishwa kwenye maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kama maandiko yanavyoelekeza, na baada kufanya hivyo kwa kudhamiria kabisa, basi dhambi zako zote zitakuwa zimeondolewa. Na Roho Mtakatifu ataingia ndani yako kukusaidia kuishi pasipo kurudia tena hizo dhambi ulizotubia. Na pia atakupitisha kwenye madarasa yake ili akuimarishe kiimani.
Je Umetubu??..Yaani umegeuka na kuacha njia zako mbaya?. Kumbuka baada ya wewe kuamua kuacha njia zako mbaya ndipo Bwana kupitia Roho wake Mtakatifu anakuongezea nguvu ya wewe kuweza kushinda dhambi, kwasababu Roho Mtakatifu ni msaidizi, maandiko yanasema hivyo, (kumbuka tena, Yeye ni msaidizi na si mtendaji). Watendaji ni sisi, yeye kazi yake ni kutusaidia, kutuongezea nguvu
Sasa jiulize atamsaidiaje mtu ambaye hajaanza kufanya chochote??, Utamsaidiaje mtu aliyechoka kutembea na ilihali hata hiyo safari yenyewe hajaianza?.
Isaya 40:29 “[Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo”.
Ni maombi Yangu leo utaamua kumgeukia BWANA YESU KRISTO kwa kumaanisha kutubu dhambi zote.
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.