Barazani pa Mungu ni wapi?

Maswali ya Biblia No Comments

Shalom.

Yeremia 23:18 “Maana, ni nani aliyesimama katika baraza la Bwana, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu, na kulisikia”

Tufuatilie mtiririko wa habari hii kwa kuendelea mpaka 22, ili tupate taarifa sahihi zaidi..

“19 Tazama, tufani ya Bwana, yaani, ghadhabu yake, imetokea; ni dhoruba ya kisulisuli; itapasuka, na kuwaangukia waovu vichwani.

20 Hasira ya Bwana haitarudi, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtalifahamu neno hili kabisa.

21 MIMI SIKUWATUMA MANABII HAO, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.

22 Lakini kama wangalisimama katika BARAZA YANGU, ndipo wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya, na uovu wa matendo yao.”

Bwana anazungumzia habari ya Manabii wa Uongo, kuwa walijitungia nabii zao wenyewe kwa kuwafanya watu wastarehe katika dhambi badala ya kutubu na kuacha; walikuwa wakiwatabiria watu kuwa ni Amani na Bwana hajakasirika, lakini haikuwa kweli.
Ndipo Sasa anasema kupitia nabii wake Yeremia kuwa Manabii hao wa Uongo hawakuketi barazani pake! Bali walijitungia nabii zao wenyewe.

Hivyo basi Barazani pa Mungu palikuwa ni mahali [pa kiroho] ambapo Bwana alikutana na watumishi wake na kuwapa Ujumbe.

Tuangalie uhalisia wake kwa kuangalia pia na Manabii wengine, tukianza na Isaya..

Isaya 6:1 “ Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.

2 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka…………….

6 Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu;

7 akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa”.

8 Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.

9 Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione”

Mifano mingine ni Manabii kama Danieli, Ezekia, Musa n.k ambao aliketi pamoja nao Barazani pake na akawapa Ujumbe kwa ajili ya watu wake [kwa kipindi hicho] yaani Israeli

Tunaona pia barazani pa Mungu anaketi pamoja na malaika zake na kuwatuma, pia Malaika za shetani Huweza kuhudhuria ili kuwashtaki wateule

Nyakati 2:18 “Mikaya akasema, Sikieni basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kuume na wa kushoto.

19 Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

20 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani?

21 Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo”

Lakini katika Agano jipya hili tulilopa Mungu anafanya Baraza lake pamoja na wanadamu kupitia Roho Mtakatifu, hamna tena uhitaji wa nabii Fulani kwenda huko na kutuletea ujumbe Bali sote twamsikia akinena kupitia Roho Mtakatifu ndani yetu

Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

14 Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari”.

Tuangalie na waraka kwa Warumi..

Warumi 10:6 “Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini), …….

8 Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo”

Ndio sababu ni muhimu sana kupokea Roho Mtakatifu maana ndiye Baraza la Mungu. Ndio maana wasio kuwa nae huyo Roho hao SI wake Mungu(warumi 8:9). Roho Mtakatifu anatenda kazi kwa Aliyemwamini Bwana Yesu na kuoshwa dhambi kwa damu yake [Yesu], na kwa ubatizo sahihi wa maji mengi kwa jina lake Yesu Kristo [matendo 2:38]

Ubarikiwe

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *